MFANYABIASHARA, James Rugemalira anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha amewataja aliodai ni wezi wa fedha za Escrow katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kama alivyosema awali kwamba anawafahamu.

Watu hao amewataja mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba,  baada ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Ruswa (Takukuru), Leonard Swai,  kueleza kwamba upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Baada ya kuelezwa hayo, wakili wa utetezi, Michael Ngalo, ameomba upande wa mashtaka uharakishe upelelezi wa kesi hiyo na kama hawawezi waiondoe mahakamani.

Baada ya kuelezwa hayo, Rugemaliraa alinyoosha mkono ambapo alidai yeye ni mgonjwa wa kansa kwa miaka tisa sasa na amekuwa akipatiwa matibabu nchini India, lakini kwa sasa ugonjwa huo umejitokeza kwa njia ya uvimbe katika sehemu za siri.

Akiiambia mahakama kuhusu suala la aliodai ni wezi, Rugemalira alidai alishawasilisha nyaraka za ushahidi kwa Takukuru kwamba ‘mwizi’ aliyeisababishia serikali hasara ni Standard Chartered Tanzania Ltd na Standard Chartered Hong Kong ambao waliisababishia  hasara ya Sh. trilioni 37.

Pia amedai kuwa watu hao aliowaita wezi hao ndiyo wamemuibia hata kwenye kampuni anayoisimamia ya VIP ambayo inawadai Sh. trilioni 16.

Naye mshtakiwa mwingine ambaye ni mmiliki wa IPTL, Harbinder Singh Sethi, aliiambia mahakama hiyo kuwa tatizo lake la ugonjwa linajulikana, pia yupo tayari kutoa ushirikiano wowote zikiwemo nyaraka ili kubaini ukweli wa kesi hiyo.

Baada ya kueleza hayo, wakili Swai alidai kuwa ni kweli Rugemalira aliwasilisha taarifa ofisini kwao na wanazifanyia kazi kisha watatoa majibu.

Akitoa ufafanuzi, Hakimu Simba alisema afya za washtakiwa ni muhimu hivyo wafanyiwe uchunguzi, pia ameutaka upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi kwa wakati, ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 19, mwaka huu.

 

By Jamhuri