Uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaelekea ukingoni. Tayari viongozi wa nafasi mbalimbali kuanzia ngazi ya mashina hadi Taifa wameshapatikana. Tunawapongeza waliochaguliwa. Lakini pongezi zetu za dhati kwa kweli tunazielekeza kwa wale waliochaguliwa bila kujihusisha na vitendo vya rushwa.

CCM ndicho chama kinachoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa nafasi yake, uchaguzi mkubwa unaofanywa ndani yake unakuwa ukiwavuta watu wengi. Ndiyo maana haikushangaza kuona uchaguzi huu ukiwa na wafuatiliaji wengi, ndani na nje ya chama. Kwa mantinki hiyo, chochote kibaya kinachofanywa ndani yha CCM, kinaweza kuwa na taathira kwa chama chenyewe na Taifa kwa jumla.

 

Katika uchaguzi huu, kama mwingine uliotangulia, rushwa imeendelea si kuota mizizi tu, bali imeshakuwa mbuyu! Kwa mara nyingine wagombea ndani ya CCM wameshiriki vitendo vya rushwa bila aibu. Tunadiriki kusema wazi kabisa kwamba wagombea wengi walioshinda wametoa rushwa.

 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ni kama haipo. Pamoja na kujaribu kujitutumua na kutaka kuonekana kuwa inafanya kazi, kwenye uchaguzi ndani ya CCM, Takukuru imekuwa ikibweka tu! Haina uwezo wa kuwang’ata watoa na wapokea rushwa.

 

Rushwa imezungumzwa waziwazi karibu kila ngazi ya uchaguzi na karibu kila kata, wilaya, mkoa hadi ngazi ya Taifa. Watoa rushwa wamekuwa wakitamba bila hofu yoyote.

 

Uchaguzi ndani ya CCM umekuwa ni kipindi cha kuvuna (kwa wapigakura) na kugawa mavuno (kwa wagombea). Jambo hili haliwezi kukubalika kwa sababu linachafua mno Taifa letu. Uchafu huu unakuwa mbaya zaidi unapofanywa na chama tawala.

 

Kwa bahati mbaya, wapigakura nao sasa hawaoni haya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wagombea. Kwa ufupi ni kwamba wapigakura ndiyo wanaolazimisha kupewa rushwa ili wawachague wagombea.

 

Athari za dhambi hii ni kwamba CCM inapata viongozi wengi wachafu na wasiokuwa na uwezo. Wanapata aina hiyo ya viongozi kwa sababu kinachotazamwa si uwezo wa kiakili na uongozi wa mgombea, bali kiasi cha fungu la rushwa analosambaza kwa wapigakura.

 

Tunatoa msimamo wetu wa kulaani vikali tabia hii ya rushwa ambayo kama tulivyosema awali, sasa imekuwa mbuyu. Tunahitaji utashi wa kitaifa wa kuwa na viongozi na taasisi makini zitakazokuwa tayari kupambana na watoa na wapokea rushwa.

 

Kinachoonekana sasa ni kama vile uongozi wa juu wa CCM ndiyo unaohalalisha dhambi hii. Tunasema hivyo kwa sababu hata baadhi ya majina ya watoa rushwa yamepitishwa. Imani yetu ni kwamba kama kweli CCM itakuwa na viongozi makini watakaoamua kuishirikisha Takukuru kupamabana na watoa na wapokea rushwa, kansa hii itapunguzwa makali, si kwa CCM tu, bali kwa Taifa zima.

 

Kama wagombea wawili, watatu watakamatwa na kutolewa mfano wa kuvuliwa uanachama, na hata kufungwa gerezani, tunadhani hiyo inaweza kuwa hatua njema katika vita dhidi ya rushwa. Lakini kubwa tunalojiuliza ni hili, haya mabilioni ya rushwa yanatolewa wapi? Je, kuna viwanda vya kudurufu fedha? Je, hawa wanaotumia mamilioni kuupata ujumbe wa NEC, watafanya biashara gani hata waweze kurejesha walizotumia na kubaki na faida?

 

Wakati umefika sasa kwa jamii kushiriki mjadala wa kitaifa wa kubuni njia sahihi na halali za kukabiliana na rushwa. Hiki kinachoonekana ndani ya CCM ni aibu tupu.

1169 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!