Uongozi wa Pori la Maswa mkoani Simiyu, unatuhumiwa kupokea fedha kutoka kwa wafugaji na kuruhusu mifugo kuingizwa katika pori hilo.

Baadhi ya wafugaji wamelalamika kukamatwa na askari wa wanyamapori, ilhali wakiwa wameshawapa fedha ili wawaruhusu kuingiza na kulisha mifugo ndani ya pori hilo.

Matukio ya askari na baadhi ya maofisa wa pori hilo kuhongwa na wafugaji, yanatajwa kuwa ya kawaida, na hivyo kuliweka pori hilo katika hatari ya kutoweka.

“Juzi wenzetu wanane walikamatwa, lakini watatu wakaachiwa huru baada ya kuwasuta askari kuwa iweje wawakamate wakati wamewalipa? Wanne wamepelekwa mahakamani, tunataka tujue kwanini wachukue fedha zetu halafu watubughudhi,” amesema mmoja wa wenye mifugo ambaye tunalihifadhi jina lake.

Kutokana na madai ya askari kuhongwa, mwishoni mwa wiki askari wa wanyamapori, aliye katika Kituo cha Nyasosi (jina tunalihifadhi kwa sasa), alituhumiwa kumkata panga askari mwingine wa kampuni binafsi aliyetajwa kwa jina la Mbogoma.

Chanzo chetu cha habari kimesema: “David alimkata panga Mbogoma akimtuhumu kuchukua mgawo wa fedha zilizotolewa na wafugaji kwa kiongozi wa askari wanyamapori. Kweli fedha hizo zilitolewa akapewa (jina tunalo) halafu akaondoka. Yule askari wanyamapori wa Kituo cha Nyasosi alifika na kumvamia Mbogoma akimtaka ampe pesa zilizoachwa na (anamtaja ofisa wanyamapori).

“Huyu askari wa kampuni binafsi hahusiki na lolote, lilikuwa ni suala la kumuonea. Hili suala lilifikishwa polisi na mipango ilikuwa ikifanywa ili kesi hiyo ifutwe.”

Vyanzo mbalimbali vya habari vimesema baadhi ya viongozi wa Pori la Maswa ndiyo wanaowatuma askari wao kukusanya fedha kutoka kwa wafugaji na kuwaruhusu kuingiza mifugo porini.

Imeelezwa kuwa viongozi wa Maswa wanapopokea fedha hizo, nao huchukua sehemu na kuzipeleka kwa baadhi ya viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii walio makao makuu.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa kwenye mgawo huo ni wale waliowahi kufanya kazi Maswa na wanajua vema ‘mchezo’ wa uchotaji fedha kutoka kwa wafugaji.

Duru za uchunguzi zinaonesha kuwa maeneo kadhaa ya kampuni za uwindaji wa kitalii yameathiriwa na hujuma hiyo, ingawa kampuni ya Mwiba inatajwa kutoathiriwa.

“Mifugo haiwezi kuingizwa Mwiba kwa sababu wao wanataka wawekezaji wenzao vitalu vyao viharibike kwani walivitaka lakini wakavikosa. Kwa sababu hiyo, ng’ombe, mbuzi na kondoo wanaingizwa kwenye vitalu vingine. Kwa sasa kuna maelfu ya mifugo Maswa. Askari wa Pori wanapokea pesa wanaachia wafugaji wafanye wanavyotaka, hali ni mbaya kweli kweli,” kimesema chanzo chetu.

Mkuu wa doria, Shirima, na Meneja wa Pori la Maswa, Ayoo, hawakupatikana kuzungumzia tuhuma zinazowagusa askari na baadhi ya viongozi wakuu wa Pori hilo.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Kanyata, ameulizwa na JAMHURI juu ya tuhuma za kuwapo mtandao wa rushwa kwa askari wa Pori la Maswa, hadi kwa baadhi ya maofisa wizarani, naye akajibu kuwa hana taarifa hizo.

“Kwanza mimi si msemaji wa wizara, nadhani ingekuwa vizuri ukawasiliana na mzungumzaji ili akujibu,” alisema.

Hata hivyo, alisema asingeweza kujibu lolote kwa kuwa hadi anaulizwa (Aprili 30 usiku) alikuwa hajapata taarifa zozote za kuwapo kwa tukio la askari kukatwa mapanga kwa vurugu zilizosababishwa na hisia za ‘kunyimwa’ mgawo wa rushwa iliyotolewa na wafugaji.

“Sijapata maelezo yoyote kutoka huko Maswa, mimi najua askari wangu walioko huko wanafanya kazi vizuri tu. Wanakamata wafugaji na kuwafikisha mahakamani. Kazi yetu ni kutenda haki,” amesema Kanyata.

1326 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!