Wizara ya Nishati na Madini imeingia kwenye mvutano na Mahakama baada ya mhimili huo kuamuru raia wa China aliyekamatwa akitorosha madini ya tanzanite, arejeshewe madini hayo kinyume cha sheria.

Habari zilizopatikana zinaonyesha kuwa raia huyo, Li Neag, alikamatwa Oktoba 17 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akiwa na karati 543.46 za madini hayo yenye thamani ya dola 120,348/80 za Marekani (Shilingi zaidi ya milioni 192).

 

Mchina huyo alikutwa akiwa na hati ya kusafiria ya nchi yake yenye namba E20203356 iliyotolewa Mei 7, mwaka huu. Alikamatwa saa 11 jioni akijiandaa kupanda ndege ya Precision yenye namba PW 732 kwenda Nairobi , Kenya.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Neag alinunua tanzanite hiyo katika duka maarufu la Cultural Heritage lililopo mjini Arusha.


Baada ya kukamatwa na maofisa wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), juhudi za kutaka kumnasua zilianza kufanywa na wamiliki wa Cultural Heritage kwa kushirikiana na baadhi ya polisi.


Hata hivyo, juhudi hizo ziligonga mwamba baada ya maofisa wa TMAA kushupalia jambo hilo, hasa kutokana na kuwapo matukio mengi ya utoroshaji rasilimali za nchi.


Hatua hiyo iliwezesha kufunguliwa kwa jalada namba KIA/RB/359/2013 katika Kituo cha Polisi KIA. Oktoba 18 mtuhumiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hai na kufunguliwa kesi yenye namba 321/2013 chini ya Hakimu aliyetambuliwa kwa jina la D.J. Mpelembwa. Baada ya kusomewa mashitaka, Mchina huyo alikiri kosa. Mahakama ikamtia hatiani kwa kumtaka alipe faini ya Sh 300,000 au atumikie kifungo cha mwaka mmoja jela. Mshitakiwa alilipa faini na kuachiwa.


Hata hivyo, katika uamuzi uliotia shaka, Mahakama iliamuru TMAA imrejeshee Mchina huyo madini yake; jambo ambalo limepingwa na Wakala kwa kuwa sheria inataka mtu anayetiwa hatiani kwa makosa ya aina hiyo alipe faini, au afungwe, au vyote (kifungo na faini kwa pamoja) na madini yataifishwe na Serikali.


Kwa mujibu wa kifungu 18(4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, mtu yeyote atakayekiuka sheria kuhusiana na umiliki na biashara ya madini akipatikana na hatia atatozwa faini ya kiasi kisichozidi shilingi milioni 10 au kifungo kisichozidi miaka mitatu, au adhabu zote mbili. Kwa kampuni adhabu iliyopo kwa mujibu wa sheria kwa kosa hilo ni kulipa faini isiyozidi shilingi milioni 50.


Aidha, kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kinampa mamlaka Kamishna wa Madini kutaifisha madini yaliyopatikana kinyume cha sheria, pamoja na vifaa vilivyotumika kuzalisha madini hayo.


Ni kutokana na sheria hiyo, TMAA wamekataa kumkabidhi Mchina madini aliyokutwa nayo kinyume cha sheria. Habari zilizopatikana zilisema TMAA walipanga kukata rufani jana kupinga amri ya Mahakama ya Hai ya kumrejeshea madini Neag.


Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kuna shinikizo kubwa kutoka kwa Cultural Heritage la kutaka madini hayo yaachiwe.


Hatua hiyo inatokana na ukweli kuwa kwenye stakabadhi, licha ya madini kuwa na thamani ya dola zaidi ya 120,000; ilionyeshwa kuwa thamani yake ni Sh milioni 89. Kati ya kiasi hicho, Neag alikuwa amelipa Sh milioni nane pekee. Hiyo ina maana kwamba endapo madini hayo yatataifishwa na Serikali kwa mujibu wa sheria, Cultural Heritage ndiyo watakaokuwa wameumia.


 

1389 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!