DAR ES SALAAM

Na Regina Goyayi

Kauli iliyotolewa hivi karibuni na mtayarishaji mkongwe wa muziki nchini, Joachim Kimaryo, maarufu kama Master J,

imemuibua mtayarishaji ‘chipukizi’, S2Kizzy, akisema siku hizi mambo yamebadilika.

Hivi karibuni, Master J amekaririwa akisema watayarishaji wa muziki wa siku hizi ni chawa wa wasanii maarufu wa muziki.

Kauli hiyo inadaiwa kumlenga S2Kizzy ambaye amekuwa karibu sana na mwanamuziki Diamond, huku akisafiri naye mara kwa mara.

Akizungumza na JAMHURI, S2Kizzy anasema: “Kwanza hakuna mtayarisha chawa. Kwa ninavyofahamu kila mmoja hufanya kazi kulingana na mikakati na mipango yake.

“Miaka imekwenda sana na mambo yamebadilika. Hauwezi kukaa studio kumsubiri msanii aje. Siku hizi biashara ya muziki

ni kubwa, kwa hiyo unapoona fursa ni vizuri kuzifuata. Fursa haziwezi kuja zenyewe, sisi tunacheza na fursa.” 

Anasema ukaribu wake na Diamond Platinumz ni wa kikazi, na kwamba wamekuwa wakisafiri pamoja kwa ajili ya yeye

kumtayarishia nyimbo zake.

S2Kizzy anasema kupata nafasi ya kusafiri huku na kule kunampa uzoefu wa aina yake na kuwa safari ni ndoto kwa

watayarishaji wengi wa muziki.

“Hatuwezi kumvunjia heshima Master J. Huyu ni mkubwa wetu na ni mkongwe katika fani. Tunaheshimu kila kitu

anachokifanya na ana mchango mkubwa kwenye muziki. Lakini ukweli ni kwamba inawezekana asilimia 90 ya watayarishaji

wangetamani kupata nafasi kama hii kwa kuwa wanafahamu manufaa yake,” anasema S2Kizzy.

Anaongeza: “Leo hii mimi nisingekuwa nimeteuliwa kushiriki tuzo kubwa Afrika Kusini na Nigeria. Lakini ninapata nafasi hizi kwa kuwa wanaona ninafanya kazi na watu tofauti kama wasanii na mapromota.

“Yanatokea haya kwa sababu ya kufanya kazi na biashara ya muziki ipo. Hapa nimetoka ofisini kukufuata wewe, kwako hiyo

ni kazi ya nje ya ofisi; unapaswa unilipie gharama za kunitoa ofisini. Diamond hunilipa gharama kubwa zaidi nikimfuata

kuliko angekuja ofisini kwangu. Hata nikisafiri naye gharama huongezeka,” amesema.

S2Kizzy anasema kizazi cha sasa watayarishaji ni vijana ambao wamefanya kazi kubwa na kuleta mapinduzi kuliko ilivyokuwa zamani.

“Tunafanya vitu vikubwa ambavyo tuseme hata nyuma havikufanyika. Zamani ilikuwa ‘producer’ kuteuliwa kwenye tuzo kubwa, haikuwa hata ikifikirika. Hata pia hawakuwa na maendeleo makubwa kama sasa. Walikuwa wanaonekana wa

kawaida tu; wa kukaa ndani,” anasema.

By Jamhuri