.Amtuhumu kuwa ni kibaraka wa Waarabu

.Adai Seif akipewa nchi, ataiuza asubuhi

.Rais Dk. Shein amsifu Sadifa hadharani

.CUF waijia juu Polisi, wadai Sadifa ni…

 

 

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Khamis Sadifa Juma, ametangaza hadharani vita ya kupambana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.

Vita ya Sadifa ni kumzuia Maalim Seif asishinde urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar utakaofanyika Oktoba, mwaka huu ambapo wakati wa sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, Sadifa alisisitiza, “Kamwe Maalim Seif hatakuwa Rais wa Zanzibar.”

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika Maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi, Sadifa anasema, “Zanzibar ni ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, kamwe haitarudi kwenye utawala wa usultani.

“Kuna mtu mmoja, anaitwa Seif Shariff Hamad. Huyo anajitangazia nafasi ya kutaka kushindana na Rais wa sasa, Dk. Shein, akitaka kuingia Ikulu na kuwa Rais. Mimi namwambia asahau.”

Sadifa anasema kwamba amemsikia Maalim Seif akitangaza hilo kwenye mikutano mbalimbali ya kutangaza mipango na sera za chama chake cha CUF, lakini akamtaka asisumbuke kwani hataweza baada ya kushindwa mara nne.

“Baada ya kushindwa mara nne atakuwa na jipya gani?” anahoji Sadifa na kuongeza: “Harakati zote za Maalim Seif kutaka kuingia Ikulu ya Zanzibar ni mipango ya kurejesha nchi kwa wasio na asili ya Zanzibar.”

Anasema, “Seif ataiuza nchi hii asubuhi. Anataka kurejesha utawala wa kisultani hapa. Hilo haliwezekani. Tumetafiti sana kupata ukweli kwa kile anachodai kwamba ‘tunataka nchi yetu’, kumbe ana maana ya wakoloni wanaitaka tena Zanzibar. Mapinduzi ya mwaka 1964 ni matukufu, yatalindwa,” anasema.

Mbunge huyo wa Donge visiwani Zanzibar anayemtuhumu Maalim Seif kuwa ni kibaraka wa Waarabu wanaotajwa kuwa na hila ya kurejea Zanzibar, alimwambia Rais Dk. Shein kwamba asihangaike na Makamu huyo wa Rais.

“Nilimwambia Dk. Shein na nasema tena huyu niachieni mimi. Nitapambana naye. Maalim Seif ni saizi yangu na katu hawezi kumfikia Dk. Shein,” anasema.

Ujumbe wa Sadifa ulimfurahisha Dk. Shein akasema, “Kijana ameongea maneno mazuri sana, yenye busara,” na kuendelea akisema Serikali itakuwa tayari kupambana na mtu au kundi lolote litakalothubutu kudhihaki au kukejeli Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.

Anasema umadhubuti wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ni ule ule wa mwaka 1964, hivyo ameonya kuwa Serikali haitamvumilia mtu atakayechezea Mapinduzi.

Anasema kwamba unafiki wa watu hao hujidhihirisha kutokana na vitendo vyao kwa kuwa wanayoyasema ni mambo tofauti na yale yaliyomo kwenye mioyo yao na kuwataka wananchi wa Zanzibar kuwa macho na watu hao.

Akizungumzia shutuma dhidi ya Maalim Seif, Naibu Mkurugenzi wa CUF wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya, anasema, “Sadifa tumemsikia, hatumshangai kwa sababu ni mtu ambaye hana nidhamu.”

Anasema kwamba Maalim Seif ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ na Katibu Mkuu wa CUF, hivyo ana hadhi ya mtu mzazi na uongozi uliotukuka, “Sasa kitendo cha kumuita mtu fulani anajiita Seif Shariff ni kukosa nidhamu.”

Kadhalika msemaji huyo wa CUF analitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kukaa kimya inapotokea kiongozi akadhihakiwa hadharani. “Hivi wangekuwa CUF wanamshambulie vile Dk. Shein huyo kiongozi angefunguliwa makosa ya uchochezi, lakini kwa CCM polisi iko kimya.

“[Kuna] mambo mawili ambayo yanatufanya CUF tusishangae sana kwa jeshi kukaa kimya juu ya Sadifa. Kwanza ni pengine ni vizazi vya CCM vya sasa ambavyo vinakuzwa ndani ya chama na kukosa nidhamu kwa wakubwa na viongozi, lakini pia taarifa za Sadifa mwenyewe kuhusu afya yake ya akili.

“Sadifa alikuwa mwanajeshi, jiulize kilimshinda nini huko? Lakini kuna hili la kuambiwa kwamba ni kichaa, nalo ni vyema mkalifuatilia na kuhoji. Hatushangai kumvaa Maalim Seif kwani kuna kipindi wakati wa urais wa Amani Karume aliwahi kumzomea.”

Madai kwamba Sadifa ana matatizo ya akili analijibu mwenyewe akisema hajawahi kuugua ugonjwa wa akili (kichaa) kama anavyozushiwa na wapinzani wake.

Anasema kuna watu wameandaliwa na mafisadi hali kadhalika viongozi wa upinzani ili wamchafue alimradi tu wajipatie umaarufu, lakini “Si kweli kwamba nimewahi kuugua kichaa.”

“Hawaniwezi watu hawa wanatapatapa tu, lakini ukweli nishasema hao si wanasiasa ni wana si hasa. Watatulia wenyewe, mimi sina muda wa kujibizana tena, ila ujumbe umefika,” anasema.

Kuhusu ugonjwa wa kichaa, anasema hizo ni taarifa za kitabibu, hivyo ni vyema kwa wale wote wanaodai hivyo kuonesha ushahidi wa vyeti vya madaktari ambavyo vinathibitisha madai yao.

 

By Jamhuri