Sagara: Katiba izuie wastaafu kurejeshwa kazini

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Amos Sagara (pichani chini), amependekeza Katiba mpya izuie wastaafu kurejeshwa katika utumishi wa umma.

Sagara ambaye ni Diwani wa Kata ya Sirari, ametaka pia mabadiliko ya Katiba yaruhusu ardhi iendelee kuwa mali ya Serikali badala ya kumilikiwa na mtu moja moja.


Anapenda kuona Serikali inakuwa na vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo vinavyozingatiwa na chama chochote cha siasa kinachokabidhiwa madaraka ya nchi.


Pia anataka Katiba ijayo iwe na kipengele kinachoruhusu madiwani na wenyeviti wa serikali za vijiji kulipwa mshahara waweze kuongeza ufanisi katika majikumu yao.


Sagara ametoa maoni hayo katika mahojiano na JAMHURI Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Wastaafu wasipewe kazi serikalini

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa halmashauri, Katiba ijayo itakuwa na manufaa kwa umma ikiwa itafuta dhana ya wastaafu kuteuliwa kufanya kazi serikalini.


“Hii tabia ya kuteua wastaafu kuwa wakuu wa wilaya, mikoa, wabunge na wenyeviti wa bodi mbalimbali ikatazwe kwenye Katiba mpya,” anasema Sagara.


Anafafanua kuwa tabia hiyo haipaswi kuendelea kupewa nafasi nchini kwa vile inasababisha vijana wengi wasomi kukosa ajira serikalini.


“Watu wakifikisha umri wa kustaafu kazi serikalini waachwe wakapumzike na kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali, nafasi zao wapewe vijana wasomi, wapo wengi tu katika nchi hii wanaohitaji ajira.


“Ufanisi unapungua katika ofisi nyingi za Serikali kwa sababu ya wazee wastaafu ambao kimsingi wameshachoka kufanya kazi kutokana na umri wao mkubwa,” anaongeza.

Serikali iendelee kumiliki ardhi

Uamuzi wa Serikali kumiliki ardhi, kwa mujibu wa Sagara, unastahili kuendelea kuhalalishwa kikatiba kuwezesha kila mwananchi kuwa na haki ya kupewa ardhi mahali popote nchini.


“Suala hili ni muhimu kupewa nafasi kwenye Katiba mpya, kwamba ardhi iendelee kubaki kuwa mali ya Serikali kwani kuimilikisha kwa mtu mmoja mmoja kutawanyima watu haki ya kupewa ardhi nje ya maeneo yao ya kuzaliwa,” anafafanua.

Vipaumbele vya Serikali

“Mabadiliko ya Katiba yawe na kipengele kinachobainisha kwamba lazima Serikali itangaze vipaumbele vya maendeleo ya nchi na ambavyo lazima viheshimiwe na chama chochote kinachokuwa madarakani.


“Utaratibu huu utasaidia kuepusha mazingira ya kisiasa yanayoingilia na kukwaza utekelezaji wa mipango ya kitaifa ya maendeleo,” amesema Sagara na kuongeza:


“Vipaumbele hivyo vilenge pia kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumiwa vizuri ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za kijamii kama vile elimu na afya kwa wananchi wote.”

Madiwani walipwe mshahara

Sagara anaamini kuwa madiwani na wenyeviti wa serikali za vijiji na mitaa wataongeza ufanisi wa kazi zao ikiwa wataanza kulipwa mshahara baada ya hatua hiyo kupata baraka za Katiba mpya.


“Mshahara utawaongezea viongozi hawa [akiwamo yeye Sagara] morali wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi yakiwamo ya kuhamasisha shughuli za maendeleo katika maeneo yao ya uongozi,” anasema kiongozi huyo.


Serikali kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea kukusanya maoni ya makundi mbalimbali ya wananchi kuwezesha uundaji wa Katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.