Salaam wafanyakazi wote

Itakumbukwa katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei mosi mwaka huu, iliyofanyika kitaifa Uwanja wa Michezo CCM Kirumba, Mwanza, yalionekana na kusikika mambo mengi ikiwamo michezo, ngoma na nyimbo zilizosifu na kushauri utendaji bora wa kazi na kudumisha nidhamu ya kazi.
Mabango yalibeba ujumbe tofauti ukiwamo wa “utani” na ukweli kwa viongozi wa nchi pamoja na salamu za wafanyakazi kwa Serikali. Viongozi na wadau wa mashirika ya wafanyakazi, walitoa risala na salamu zao pia kwa Serikali na wafanyakazi. Ukweli ilikuwa sherehe nzuri na ya kufana.


Miongoni mwa viongozi waliozungumza na kutoa salamu kwa wafanyakazi nchini ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye aliwasifu na kuwapa kongole wafanyakazi nchini kwa utendaji mzuri wa kazi zao na kushirikiana naye katika kipindi chake chote cha uongozi na urais. Ama, Rais Kikwete anatarajiwa, kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, kuacha madaraka ya urais mwishoni mwa mwaka huu. Katika hotuba yake kwa wafanyakazi nchini, Rais Kikwete alizungumzia mambo mengi ya kitaifa yakiwamo ya madai na maombi ya wafanyakazi. Suala la walimu katika kielelezo chao “Shemeji Unatuachaje” alikiri kwa kusema kuwa mambo ambayo hajayatekeleza, atamnong’oneza rais ajaye kuyakamilisha.


Aliwaagiza makatibu wakuu wa wizara za Serikali kuacha ajizi katika kuanzisha Mabaraza ya Wafanyakazi. Wafanye hima ili Serikali iendelee kuwajibika kwa wafanyakazi. Aidha, alionesha upendo juu ya afya za wafanyakazi kwa kutangaza rasmi kuanzishwa kwa kurugenzi ya wauguzi nchini.
Rais Kikwete aliwaaga na kuwatakia kila la heri wafanyakazi katika kazi zao na kuwasisitiza bila kusahau kuweka mbele juhudi na maarifa wakiwa kazini, na kujenga moyo wa utu na upendo kwa wananchi. Wachukie, wakemee na wakatae kushiriki katika vitendo vya kikatili si njia halali wala ya busara kukata viungo au kumuua mtu mwenye ualbino kama ndiyo njia ya kupata mali.


Kabla ya mgeni rasmi Rais Kikwete kuzungumza na wafanyakazi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA),  Nicolaus Mgaya, alitoa salamu za wafanyakazi kwa Serikali. Katika salamu hizo alisema na namnukuu,”Kumekuwa na viashiria vya watu kuachiwa kutukuza udini, ukabila, ukanda na ufisadi. Watu kujilimbikizia mali na kuzidisha pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho. Vitu hivi vinatishia amani yetu na hakuna hatua zinazoonekana kuchukuliwa” mwisho wa kunukuu. Salamu hizo ni ujumbe kamili kwa Serikali na wananchi kuwa na hadhari kwani Taifa linaingizwa kwenye bahari ya mashaka na maangamizi iliyojaa uadui, chuki, na kisasi cha milele. Hiyo ni hali mbaya kwa maisha ya watu ambao kwa miaka nenda rudi hawajaonja wala kuvuta harufu ya uhasama.


Nchi yetu inaweza kupoteza sifa yake ya “Tanzania ni kisiwa cha amani” kwa sababu tu baadhi ya watu wanataka kujaribu kuonja sumu kama kweli inaua au la! Kwani udini, ukabila, ukanda na ufisadi ni vitu vinavyojengwa na matakwa ya mtu mwenyewe akiwa na nia ya kudhulumu, kunyonya na kufisidi mali za watu na Taifa ili kuwa maskini.


Hali ya ufisadi ina maeneo mengi ya kufisidi mali na rasilimali za Taifa na kuzaa ulofa na ukata ambao huchipua umaskini kwa wananchi walio wengi. Mafisadi wenyewe hufanya matumizi mabaya ya mali na kufanya uhayawani ambao huharibu mila na tamaduni za Taifa.
Ukanda hujengwa na wale watu wanaodhani na kuona kuwa wao ndiyo pekee wenye haki ya kuhodhi na kumiliki rasilimalli zilizomo ndani ya kanda yao na kupuuza watu wengine waliomo ndani au nje ya kanda hiyo. Ingawa waliomo ndani ya kanda hiyo wengi wao hukosa fursa ya kupata haki zao kwa sababu tu ya ufisadi wao. Huu si muamala mzuri si kwa wafanyakazi tu bali hata kwa wakulima na wafanyabiashara. Ni kitanzi.


Ukabila huleta ubaguzi na choyo katika kupata fursa za ajira hata za masomo. Uwezo na sifa za kupata kitu fulani, kutenda jambo jema au kupata mamlaka na uamuzi hukosekana. Watu wa kabila hilo hujiona bora kuliko watu wa kabila jingine. Dharau na kiburi hupata nafasi ya kutawala dhidi ya makabila mengine. Huo ni utengano na unyanyasaji wa kibinadamu.


Suala la udini kila kukicha linapata wafuasi wengi ndani na nje ya dini kwa sababu jamii haitaki kuangalia kiini cha udini. Udini si mtu kupenda na kufuata taratibu na ibada za dini yake, huo ndiyo wajibu wa imani ya dini yake.
Udini ni kitendo cha mtu yeyote kuzuia au kunyima dini nyingine au mtu mwingine kupata au kutekeleza haki na taratibu za dini yake. Kufanya upendeleo katika kugawa fursa za maendeleo ya jamii katika nyanja zote za kutoa huduma iwe za elimu, ajira, afya, mamlaka au uwezo wa uamuzi n.k. kwa mtu aliye katika dini yake na kumnyima mtu asiye wa dini yake hata kama ana sifa na uwezo katika nafasi itakiwayo. Hapo awali nimetamka “jamii haitaki kuangalia kiini cha udini”. Narudia kusema haitaki kwa sababu watu wanaofanya udini na kuzungumzia pamoja na kukemea udini ndiyo hao hao wanaotekeleza udini kwa kulinda maslahi yao. Wapo pia ambao hawajui maana ya udini na hivyo hujitia kundini kukemea ilhali wanatekeleza udini.


Udini nchini haukuanza juzi wala jana na leo. Ulianza tangu enzi za ukoloni na kupata fursa ya kutekelezwa kwa mapana tangu nchi hii ipate Uhuru wake. Kuanzia hapo mserereko wa udini umeendelea na kuleta madhara katika kupata tija na ufanisi wa kazi. Na hapo ndipo ndugu yangu Nicolaus Mgaya anapopiga kelele na kulitaka Taifa kuliangalia suala hili la udini kwa makini na kupatiwa suluhu. Kwani pato la mtu na uchumi wa nchi unaporomoka lau kama kuna mporomoko wa dunia wa uchumi.


Nasema udini una mapambio yake ambayo ni ukabila, ukanda na ufisadi. Viongozi wanajua kiini cha udini lakini wanahofu kupoteza maslahi yao watakaposema ukweli. Na sisi akina tata kabwela tunaogopa nguvu za dola kutua mwilini na pengine kupoteza maisha. Wapo waliojaribu kuukabili udini wamekiona kilichomnyoa kanga manyoya.


Hivi ni kweli viongozi wa dini na wasio wa dini hawajui kama wanalea udini? Watendaji wa shughuli za utoaji huduma kwa jamii hawajui au hawapokei maagizo ya kusimamia udini? Vitabu vinavyoandikwa kuhusu UDINI kweli vinaeleza nani muhusika na nani kiranja mkuu wa udini? Tunahitaji ukombozi wa kweli wa fikra ili tutoke hapa tulipo. TUTAFAKARI.