Ndugu wasomaji wa safu hii na gazeti hili, nawasalimu kwa salamu za upendo. Hongera kwa kuwezeshwa na Mungu kuuona mwaka huu mpya wa 2015. Pasipo kujali hali zenu katika maeneo yote; ninaamini lipo tumaini kwa mwaka huu.

Ni takribani wiki nne (tangu mwaka jana mwishoni) sikuwamo safuni. Sababu kubwa ya kuadimika kwangu ilikuwa ni kujipa muda wa kutafakari kazi yote niliyoifanya kwa mwaka uliopita na kujipanga kwa ajili ya mwaka huu mpya.

 

Katika kipindi ambacho sikuwapo hewani, nilikuwa na kazi ya kutathmini makala moja baada ya nyingine kati ya zote nilizoandika mwaka uliopita, kupitia maoni yote ya wasomaji waliowasiliana nami pamoja na kutengeneza mpango kazi wa mwaka huu.

 

Lakini pia niliutumia muda huo kwa ajili ya kupumzika na kupumzisha ubongo. Kimsingi, kuandika makala (hasa hizi za kiuchambuzi); na ikiwa lengo ni kuwa na makala bora; inahitaji kufikiri na kuumiza kichwa kweli kweli. Kuandika kila wiki makala yenye mawazo mapya kwa mwaka mzima ni kazi inayohitaji bidii, muda na akili nyingi.

 

Ndiyo maana mwanzilishi wa kampuni ya Ford na mbunifu wa magari ya Ford, Henry Ford, amepata kusema hivi, “Kufikiri ndiyo kazi ngumu kuliko zote duniani, ndiyo maana ni wachache tu wanaojishughulisha nayo.”

 

Kuna wakati ambao kuandika sentensi moja yenye uhakika katika makala inahitaji niwe nimepitia vitabu hata vitano achilia mbali majarida, vipindi vya televisheni na mitandao mbalimbali ya intaneti! Maana yake ni kwamba kabla sijaandika wazo fulani ni lazima nijiridhishe, nilitafiti na kuona wengine wanasema nini, nijue uhalisi wake kwa sasa (current status of the issue), ndipo mimi nione ninasimama wapi.

 

Kwa jinsi hii utagundua kuwa kuandika makala si suala la kuchukua kompyuta na kuanza kubofya, la hasha! kuna kusoma kwingi, kuna kutafiti kwingi, kuna kufuatilia kwa kina, lakini kubwa kuliko yote kuna kufikiria namna ya kupanga na kuwasilisha mawazo na maarifa ninayoyapata kwa kusoma na kutenda.

 

Kwa mfano, mwaka uliopita, nimesoma vitabu 49 (arobaini na tisa)  na kati ya hivyo chenye kurasa chache ni kurasa 51 kiitwacho, “Breaking the cure of Poverty” kilichoandikwa na Dk. C Willium Gwilian. Katika hivyo 49, chenye kurasa nyingi kilikuwa cha 'The Antiques of the Jews' ambacho kina kurasa 2190 (elfu mbili mia moja na tisini); ambacho kimeandikwa na Flavius Joephus na kutafsiriwa (kwenda Kiingereza) na Willium Whiston.

 

Kati ya nilivyosoma vimo pia vya 21 'Success Secrets of Self made millionaires' cha Brian Tracy, 'How successful People Think' cha John C. Maxwel, 'Maximize Your Destiny' cha David O. Oyedepo na vingine. Lakini kipo kitabu cha 50 ambacho nimekisoma na kukirudia mara kwa mara, kiitwacho “Ni wakati wako wa Kung'aa” ambacho kimeandikwa na mimi mwenyewe.

 

Unaweza kushangaa inakuwaje nasoma kitabu changu mwenyewe? Ukweli ni kwamba kuna wakati ninapopitia hata makala zangu nilizoziandika mimi mwenyewe, huwa ninazishangaa sana; kwa sababu kuna mambo huwa najifunza.

 

Kwa hiyo, hata katika kitabu changu licha ya kukiandika; ninapokipitia kila wakati kuna jambo najifunza ama linaimarika ndani yangu. Ukiacha vitabu hivyo pia nimekuwa na utamaduni wa kusoma magazeti na majarida yahusuyo biashara kutoka duniani kote ili niwe 'current'.  Kwa mfano, kila wiki ni lazima nisome gazeti la 'The East African' hasa katika kurasa za biashara ili nijifunze mwenendo wa biashara za Afrika Mashariki.

 

Lakini pia kupitia mtandao wa intaneti ni lazima nisome kila toleo la gazeti la 'Forbes' ili kutambua kinachoendelea katika ulimwengu wa biashara duniani pote. Ipo mitandao mingine mingi ambayo ni lazima nidumu kuipitia kwa ajili ya kujiongeza.

 

Kwa upande wa televisheni vipo vituo viwili vilivyojikita mahsusi kwa masuala ya biashara na uchumi pekee; ambavyo huwa navifuatilia kwa ukaribu sana; Bloomberg TV na CNBC TV. Mchungaji mmoja amepata kusema kwamba, “Ikiwa chaneli hizi zinashika nyumbani mwako, basi Mungu yumo nyumbani mwako, kwa sababu hutakosa mawazo ya kibiashara na wala hutakuwa nyuma hata kidogo katika ulimwengu wa kibiashara, kiuwekezaji na kiuchumi.”

 

Blomberg L.P kampuni inayomiliki Bloomberg TV pamoja na utitiri wa vyombo vingine vya habari inakadiriwa kwamba ndiyo inayoongoza kwa kumiliki sehemu kubwa ya taarifa za biashara dunia nzima. Hivyo unaweza kuuona umuhimu wa kufuatilia vyombo hivi.

 

Kwa nini nimeeleza rekodi zangu binafsi kuhusu kujifunza? Kuna mambo makubwa mawili. Mosi, mtakumbuka kuwa mwaka jana niliandika makala kadhaa zinazosisitiza umuhimu wa watu (hasa wanaotaka kuwa na uchumi imara) kutafuta taarifa na maarifa chanya. Nilisema wanaofanikiwa siku zote wanayo namna fulani ya kufikiri inayowasaidia.

 

Tena nikasema fikra (zozote) ni matokeo ya taarifa unazozijaza ubongoni mwako. Hivyo, kupitia rekodi yangu hii (ya vitabu ninavyovisoma, TV ninazoangalia, magazeti ninayopitia n.k) unaweza kupata picha ya taarifa gani uanze ama uendelee kuzijaza ubongoni mwako.

 

Jambo la pili ni kwamba ninataka ufahamu kuwa safu hii imejengwa juu ya misingi imara ya utafiti kupitia kusoma kwa bidii, kutenda kwa bidii, kutazama kwa umakini na kupembua kwa uangalifu mkubwa. Hata kama ni mtu mmoja tu aliyenufaika na safu hii kwa mwaka mzima wa 2014, hiyo kwangu mimi ni furaha na ushindi kwani ninatambua kuwa kujitaabisha kwangu si bure!

 

Akiwepo mtu mmoja tu aliyebadilisha fikra kwa makala zangu, anatosha sana kuamsha sherehe na shangwe kubwa kule mbinguni kwa Mungu. Ingawa siandiki kwa manufaa ya kifedha, thawabu zitokanazo na “mbingu kufurahi” najua hazitakosa kunimiminia baraka kila upande maishani mwangu.

 

Mwaka 2015 tena ninaendelea na kazi ya uchambuzi kupitia makala ambayo mara zote mimi naitazama kuwa “Ni utume wa kuwaonesha watu njia ziwapasazo kupita kiuchumi.” Hii siyo kazi rahisi sana, kwa sababu huwezi kuwaonesha wengine usikokujua, ni lazima uwe na uhakika nako ndipo uwaambie watu twende ama nendeni.

Nilijifunza kuandika makala kupitia mambo ya siasa (niliandika makala yangu ya kwanza mwaka 2006 nikiwa kidato cha tano). Wanaofuatilia makala zangu tangu zamani wanakumbuka kuwa nilikuwa nikiandika sana kuhusu siasa. Baada ya kujitathmini nikagundua kuwa kuandika siasa nimevamia mraba wa wengine kwa sababu mraba wangu mimi ni huu wa uchumi na biashara.

Hadi leo ninachambua kwa uhuru sana habari hizi za biashara na uchumi kuliko siasa au mambo mengine. Leo hii ukiniambia niandike makala ya kiasiasa ninaweza kuandika lakini ninaamini haitapendwa na wengi.

Haitapendwa kwa sababu; ili makala ya siasa ionekane 'bomba' [ni lazima] iwe na sifa mojawapo ama zote katika tatu. Mosi ibebe skendo, pili ibebe malalamiko au ibebe ukosoaji wa 'za uso'.

Tangu niwepo katika mraba wa biashara na uchumi nimepoteza kabisa roho ya malalamiko, nikitazama mwenendo wa nchi naangalia mambo(issues) na siyo watu; kwa maana hii ndio maana ninasema nikiandika makala ya siasa inaweza isiuze.

Nimekupa mfananisho huo ili kukazia jambo nililolisema hapo juu ya kwamba ili uwaoneshe watu njia ya kuiendea kiuchumi inabidi uwe umeshaijua. Siasa zina uelekeo wake na biashara na uchumi vina mwelekeo unaojitegemea.

Ili uchambuzi ninaouleta hapa uwe na tija ni lazima uwe umeanza kunisaidia mimi mwandishi kwanza. Nikisema utamaduni wa kuweka akiba ni jambo zuri, maneno hayo yanakuwa na nguvu zaidi ikiwa tu na mimi ninajiwekea akiba. 'Pointi' yangu ni kwamba, mimi binafsi nimejenga utamaduni na malengo ya kuandika mambo niliyoyathibitisha walau kwa vitendo na utafiti wa kina.

Nafahamu mengi sana kutoka vitabuni lakini siwezi kuandika kila kitu kwa sababu yapo mengi sana ambayo nimegundua hayana tija (unapplicable)

Ukweli ni kwamba nikikuelekeza biashara ambayo nimeshawahi kuifanya inakuwa na msaada mkubwa kwako kushinda biashara ambayo nimeisoma tu vitabuni.

Nikikuelekeza mfumo wa kufikiri ulionisaidia unakuwa na matokeo mazuri zaidi kwako kuliko kuandika nadharia pekee kutoka vitabuni. Kwa jinsi hii mwaka huu, 2015, nimeweka lengo la kuandika makala zitakazowainua watu kiuchumi kwa vitendo. Kwa jinsi hii mwaka huu nategemea kuzalisha wafanyabiashara wapya na kuwakuza wanaoendelea. Hii ndiyo kazi niliyonayo mwaka huu.

Lengo hili litakwenda sambamba na kuwatembelea wasomaji wa safu hii mikoani. Safari zangu hizi siziiti kama semina bali ninaziita kama mazungumzo. Siendi kufundisha bali nakwenda kujadiliana na kushirikishana maarifa, ujuzi na uzoefu katika maeneo ya biashara, uwekezaji na uchumi wa kifamilia.

Naamini msomaji kuna kitu unakifahamu ambacho mimi sikifahamu nami huenda ninacho usichokifahamu, tunapokutana kama wawili ama kama kundi ni lazima tutoke hatua moja kwenda nyingine.

Safari za awamu ya kwanza nitaanzia mkoani Lindi, kisha nitakwenda Dodoma, Geita na kumalizia Dar es Salaam. Kuna maeneo nitaonana na mtu mmoja mmoja (walionialika) na kuna mahali nitakutana na makundi ya wanavyuo, wana-Saccos, wafanyakazi, wanaojiandaa kustaafu, wafanyabiashara na vijana wa vyama vya siasa.

Kote huko itakuwa ni 'nondo' za biashara, miradi na uchumi. Popote ulipo nitakakofika waweza kuwasiliana nami kwa ajili ya ratiba ili ukiwa na nafasi ama ukitaka kundi lako (ama wewe) kuungana na kuzungumza nami; upate nafasi hiyo. Natazamia kushirikisha na kujifunza mambo mengi katika safari hizi; hivyo usisahau kunialika katika mji, biashara, taasisi, kampuni ama kikundi chako.

stepwiseexpert@gmail.com, 0719 127 901

1217 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!