Naandika makala hii dakika chache baada ya kufika jijini Accra, Ghana. Nimetoka Dar es Salaam jana na juzi nilisikia maneno aliyozungumza Mheshimiwa Rais John Pombe Mafuguli, alipopata fursa ya kutembelea Pemba kushukuru wapigakura.

Nikiri kwanza kwamba Rais wetu anafanya jambo zuri sana. Kwa wanadamu tulio wengi, ni rahisi mno kuomba. Tukiishapata, huwa hatukumbuki kurejea kushukuru. Natumia fursa hii kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kulifahamu hili na kuamua kwa dhati kupita kuwashukuru wapigakura kwa kumchagua kuwa Rais wa Tanzania, mwaka 2015.

Ukiacha hilo, lipo hili la pili. Septemba 1, ilikuwa siku waliyopanga kuandamana wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa maelezo kuwa wangeandamana kutetea demokrasia. Tulishuhudia askari wakifanya mazoezi barabarani, ndege zikirushwa angani, na ikapatikana sababu mujarabu, kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilikuwa linaandhimisha miaka 52 tangu kuanzishwa kwake.

Sitanii, nalipongeza JWTZ kwa kutimiza miaka 52 na kwa kuadhimisha miaka hiyo kwa mtindo wa aina yake wa kufanya usafi nchi nzima. Wiki iliyopita, niliandika katika safu hii nikiwaomba Chadema kusitisha maandamano. Nilijua gharama kubwa iliyokuwa inaelekea kutokea kwa maisha ya Watanzania. Nampongeza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa kutanguliza utaifa na kusitisha maandamano hayo.

Hata hivyo, Mbowe alisema wamesogeza mbele maandamano hayo kwa mwezi mmoja hadi Oktoba Mosi. Amesema alishauriwa na viongozi wa dini na watu wa kada mbalimbali kusitisha maandamano hayo na amekubali kufanya hivyo. Viongozi wa dini wameahidi kuzungumza na Rais Magufuli kuona mustakabali wa jinsi ya kufanya siasa nchini.

Sitanii, Rais Magufuli muda wote amekuwa akisema bayana kuwa anamwamini Mungu. Sina shaka kuwa anawaamini pia wawakilishi wa Mungu hapa duniani; viongozi wa dini. Mbowe ameliambia taifa kuwa Rais Magufuli uligoma kukutana na viongozi wa dini. Hatujasikia kauli yako wala ya msaidizi wako Jerrison Msigwa katika hili. Bado naamini kuwa hukuwahi kukataa wito wa viongozi wa dini na utakutana nao.

Nimemsikia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akisema Oktoba 1, iliyopangwa na Chadema kufanya maandamano ya UKUTA ikiwa viongozi wa dini watashindwa kufikia mwafaka na Rais Magufuli, eti kwao itakuwa siku ya kupanda miti. Sidhani kama tunahitaji kufanya uchokozi wa aina hii uliopitiliza. Yatupasa tutambue kuwa hata hao wapinzani ni binadamu. Wana nyama na moyo!

La pili na kubwa lililonifanya kuandika makala hii na kwa kumuomba radhi mapema Mheshimiwa Rais Magufuli, ni hii kauli aliyoitoa Pemba. Kwamba Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein ni mpole na akiona yamemshinda amjulishe atamaliza udhia ndani ya dakika 5, hilo Mheshimiwa Rais naomba usilitamke tena.

Maneno kama haya yanaweza kunyunyuzia mafuta kwenye moto. Naomba na kusisitiza. Maneno haya yangetamkwa upande wa pili, tungepata tafsiri mpya ya neno “uchochezi”. Sasa Mheshimiwa Rais sisi katika vyombo vya habari unatupa wakati mgumu. Unapotumia baadhi ya maneno yanayotumiwa na wengine yakawatia hatiani, jamii inachanganyikiwa.

Sitanii, Mheshimiwa Rais nayaeleza haya kwa maana kwamba mara kadhaa umesisitiza kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Sitaki mimi kuwa mpenzi wa shetani. Mitaani wanasema na kuhoji hayo. Wanakumbuka neno ulilotumia pale chuko kikuu dhidi ya baadhi ya wanafuunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, lilivyomtia hatiani kijana anayehangaika mahakamani. Watu wanahoji, iwapo mtu angetokea upinzani akatangaza dakika hata 20, si 5 kama ulizotamka wewe, iwapo angeendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Rais, Tanzania inayo matatizo mengi. Ulianza kujenga moyo wa watu kufanya kazi. Tunafahamu fika kuwa mamlaka unayo tena hujatumia hata asilimia 5 ya mamlaka uliyonayo kikataba. Hata hivyo, nguvu inayotumiwa na jeshi la polisi kupambana na kauli za wanasiasa, ingetumika nusu yake kusimamia uzalishaji au ujenzi wa madaraja, basi nchi hii ingegeuka ya maziwa na asali ndani ya muda mfupi.

Malumbano kati yako na wanasiasa, hayawezi kuwa na tija. Nakupongeza kwa kununua ndege mbili zinazotua hapo nyumbani mwezi huu. Nafarijika kusikia umeanza mchakato wa kununua meli katika Ziwa Victoria. Badala ya kuelekeza nguvu katika majukwaa ya siasa, nashauri umuinge Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa.

Mwalimu Nyerere kila aliposimama majukwaani, alikuwa akieleza viwanda alivyojenga. Kilimo cha korosho kinavyoendelea. Ukulima wa kisiasa. Ujenzi wa kiwanda cha baiskeli cha Swala. Alizungumzia ujenzi wa kiwanda cha magari cha nyumbu. Mheshimiwa Rais ulinaza hivyo hivyo, ila sasa kadri siku zinavyosogea naona unaingia zaidi kwenye siasa za majukwaani kuliko kitendo cha kuchapa kazi na kutukomboa kiuchumi.

Sitanii, naomba kuhitimisha makala hii kwa kukuomba uniwie radhi, ikiwa maneno haya hukuyapenda, ila nimeona nikuunge mkono kwa kuwa msema mweli nami nihesabiwe katika wapenzi wa Mungu. Mungu ibariki, Tanzania. Mungu ilinde amani ya nchi yetu.

2189 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!