*CAG asema uvuvi huu ukiendelea miaka 15 ijayo litakuwa tupu

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ametoa ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2011/2012 na kutoa tahadhari kwamba endapo uvuvi haramu hautadhibitiwa katika Ziwa Victoria, miaka 15 hadi 20 ijayo samaki watakuwa wametoweka katika ziwa hilo kubwa katika Afrika.

Ifuatayo ni taarifa ya CAG kama alivyoitoa kwa waandishi wa habari mjini Dodoma, wiki iliyopita:


Kupungua kwa sangara katika Ziwa Victoria ni moja ya masuala katika nchi za Afrika Mashariki yanayopewa umuhimu. Katika miaka ya hivi karibuni, Ziwa Victoria limekabiliwa na uvuaji sangara na aina nyingine ya samaki kupita kiwango.

 

Uvuvi kupita kiwango miongoni mwa sababu nyingi, unathibitishwa na mwenendo wa kupungua kwa upatikanaji wa sangara, na wastani wa urefu unaotakiwa kwa sangara kuvuliwa.

 

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ina wajibu wa kuandaa, kutekeleza, kupelemba (ufuatiliaji) na kupitia marekebisho ya muundo wa sera na kanuni za uvuvi Tanzania. Pia, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hutekeleza sera hizo kupitia halmashauri husika.


Lengo la ukaguzi ni kuchunguza kama Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi imeratibu, imedhibiti uvuvi haramu na kufanya doria kwa ufanisi na tija, ili kukabiliana na tatizo la uvuvi wa sangara uliopita viwango katika Ziwa Victoria. Ukaguzi ulitumia taarifa za kipindi cha miaka mitatu kuanzia Juni 2008 hadi Desemba 2011. Pia taarifa zilikusanywa kutoka wilaya 15 zenye shughuli za uvuvi katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Mara.

Umuhimu wake

Uvuvi katika Ziwa Victoria ni shughuli kubwa ya kiuchumi na chanzo muhimu cha mapato kwa jamii husika na kampuni za kibiashara. Hali halisi ni kwamba jamii inayoishi kando ya Ziwa Victoria, inategemea uvuvi kama shughuli kuu za kiuchumi.

 

Licha ya umuhimu huo, kiwango cha samaki kinachotakiwa kubaki ziwani kimepungua kupita kiasi kwa miongo kadhaa. Tathmini ya kiasi cha samaki kinachotakiwa kubaki ziwani, iliyofanywa na Taasisi ya Uvuvi Ziwa Victoria (LVFO), inaonesha mwenendo wa kupungua kwa samaki sangara tangu mwaka 2000.


Kiwango cha chini cha samaki aina ya sangara upande wa Tanzania kinachotakiwa ziwani, kinakadiriwa kuwa takribani tani 391 katika eneo la kilomita za mraba 35,088 upande

wa Tanzania, wakati huo huo hazina ya sangara imekuwa ikipungua kupita kiasi kinachotakiwa kwa uvuvi endelevu. Kiwango hicho kinakadiriwa kuwa tani 200.

Tulichokiona

Kiwango cha samaki kipo chini ya kiwango kilichopendekezwa. Mwaka 2011, kiasi cha sangara waliokuwapo upande wa Tanzania inakadiriwa kuwa tani 165,439 na kiasi kinachotakiwa kubaki kwa uvuvi endelevu (kuendeleza kizazi) ni tani 64,141. Wakati kasi ya uvuaji wa sangara kwa mwaka inakadiriwa kuwa tani 101,298 ambako imezidi kiasi cha tani zinazotakiwa kubaki kwa uvuvi endelevu.

 

Ukaguzi umeona kuwa kuna kiasi kikubwa cha wavuvi na vyombo vya uvuvi havijasajiliwa. Asilimia 50 ya wavuvi na vyombo vya uvuvi katika Ziwa Victoria havikusajiliwa. Hii ni kutokana na hatua duni zilizochukuliwa ili kudhibiti kiasi cha sangara wanaovuliwa.

Pia ilibainishwa kuwa hakuna kiwango kilichowekwa kwa ajili ya uvuaji wa samaki/sangara kwa mwaka, kwa sababu ya aina ya uvuvi unaofanyika Ziwa Victoria, ambao ni uvuvi mdogo mdogo (artisanal fishing) uliochangia wizara kushindwa kuweka kiwango cha uvuaji.


Pia hakukuwa na kumbukumbu zinazoonesha uratibu na ufuatiliaji wa karibu, unaofanywa na maafisa uvuvi wa wilaya pamoja na kikosi cha doria kudhibiti shinikizo katika uvuaji wa sangara. Vilevile, hakukuwa na mfumo madhubuti kwa sehemu ya uvuvi udhibiti na doria (MCS unit) na halmashauri kuhakikisha kuwa wavuvi wanatumia zana za uvuvi zilizokubaliwa kisheria, na kudhibiti matumizi ya nyavu zenye matobo madogo ambayo yameongezeka kwa kasi mwaka 2011.

Uratibu/ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi

Ufuatiliaji wa karibu na ukaguzi wa shughuli za uvuvi umebaini kuwa vikundi vya usimamizi wa mialo “Beach Management Unit (BMU)” vina uwezo mdogo wa kugundua uvuvi haramu, usioripotiwa na kudhibitiwa. Hii ni kutokana kutoweka mipango ya jinsi ya kuendesha shughuli za uvuvi, kutopewa ushirikiano na halmashauri husika, na wizara kutofanya tathmini ya kutosha ya maendeleo ya BMUs.

Udhaifu huu unadhihirishwa kwa uwepo wa mialo isiyo rasmi. Takwimu za uvuvi katika mialo hazikusanywi kwa sababu kampuni binafsi zilizopewa kazi hiyo, lengo lao ni ukusanyaji wa mapato pekee na si takwimu za uvuvi. Pia kuwapo kwa ushirikiano duni kati ya viongozi wa serikali ya kijiji na viongozi wa BMU, na kukosekana kwa mafunzo ya msingi ya ukusanyaji wa takwimu kwa BMUs.

 

Wizara imeweka kipimo cha urefu wa sangara anayefaa kuvuliwa kuwa kati ya sentimita 50 hadi 85, ingawa hakuna kiwango cha juu cha kiasi cha sangara kuvuliwa kwa mwaka. Pia hakuna udhibiti wa kutosha wa uvuaji. Kumekuwa na udhibiti mdogo wa samaki wachanga.

Hatua dhidi ya uvuvi haramu usioripotiwa na kudhibitiwa

Ukaguzi umegundua kwamba kumekuwa na ongezeko la matumizi ya zana haramu katika Ziwa Victoria. Katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 na 2011/2012 ongezeko lilikuwa kutoka 6,415 hadi 146, 657 katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa (ya wakati huo).

 

Ongezeko hili limechangiwa na kuongezeka kwa matumizi ya kokoro kwa asilimia 368 kutoka 394 kwa mwaka hadi 145,302. Hii ni kwa sababu ya mahitaji makubwa ya samaki katika viwanda, jamii husika na ongezeko la soko la samaki wachanga katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Sudan Kusini na Burundi.

 

Wafanyabiashara haramu wa samaki hawafikishwi mahakamani kwa kiwango cha kuridhisha. Hii inadhihirishwa kwa asilimia ndogo ya kesi zilizofunguliwa. Kituo cha Uvuvi Doria katika Mkoa wa Mwanza, kesi nyingi hazikupelekwa mahakamani kwa sababu ya maafisa kutokuwa na ujuzi wa msingi wa namna ya kufungua kesi pamoja na kuendesha mashitaka.


Hata kwa zile kesi ambazo zilipelekwa mahakamani na kufunguliwa jalada, zilichukua muda mrefu kukamilika na gharama za uendeshaji kuwa kubwa. Hali hii inatokana na waendesha mashitaka kuchukua muda mrefu katika kufanya uchunguzi.

 

Uratibu wa taarifa za uvuvi haramu, kutoripotiwa na kutodhibitiwa kwa uvuvi, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ilikuwa na lengo la kuanzisha hifadhi data kwa ajili ya utoaji wa taarifa kwa wakati ifikapo Juni 2010.


Hata hivyo, wizara haikuweza kutekeleza lengo hilo la kuanzisha mfumo wa kushirikiana taarifa hizo, hali ambayo imesababisha ukusanyaji hafifu wa takwimu na taarifa za kiasi cha samaki wanaovuliwa, akiba iliyopo na taarifa za kiintelejensia kutokomeza uvuvi haramu. Pia hakuna muundo mzuri na unaofanya kazi katika mtiririko wa taarifa kati ya vikundi vya usimamizi wa mialo (BMUs) na halmashauri za wilaya na vituo vya uvuvi doria.

 

Kutoripotiwa na kutodhibitiwa kwa shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria havikutekelezwa ingawa vilikuwa kwenye mipango. Mipango hiyo haikuonesha itafanyika wapi na elimu hiyo kama itajikita katika masuala ya kudhibiti uvuvi haramu, usioripotiwa na kudhibitiwa.


Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi haijachukua hatua za dharura kuokoa hali ya kushuka kwa kiasi cha sangara katika Ziwa Victoria. Idara haijaweka mipango ya kuzuia uvuvi wa wazi (open access) ili kudhibiti kushuka kwa kiasi cha sangara. Pia, taratibu za leseni katika wilaya hazifuatwi ipasavyo, hivyo kusababisha wavuvi wengi na vyombo vya uvuvi kutosajiliwa na BMUs.


Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi imetekeleza kwa kiasi kidogo viwango vya udhibiti vilivyopo, ili kupunguza tatizo la uvuvi kupita kiasi.


Vituo vya Uvuvi Doria vimekuwa vikipokea kiasi cha asilimia 1.3 hadi 10.3 ya maduhuli yaliyokusanywa vituoni ili kuendesha shughuli za doria katika vituo vyao. Pia halmashauri hazina mfumo wa mgawo wa fedha kwa BMUs ambao umeathiri ukusanyaji wa takwimu za samaki wanaotua katika mialo na hivyo basi takwimu hizo hazikusanywi. Wizara nayo, haijachukua hatua za kutosha kusimamia kiasi cha sangara wanaovuliwa kwa mwaka.


Imebainika kuwa kuna utekelezaji dhaifu wa sheria za uvuvi katika halmashauri zote zilizotembelewa pamoja na Vituo vya Usimamizi, Udhibiti na Doria Uvuvi (MCS), kasi ya uvuvi haramu hailingani na kasi ya wavuvi haramu wanaokamatwa. Kituo MCS na wilaya Kanda ya Ziwa zinazojihusisha na uvuvi hazikuweka juhudi na kipaumbele katika kupambana na uvuvi haramu.


Kuna matukio ambayo vyombo vya uvuvi vikijihusisha na uvuvi haramu, lakini adhabu zinazotolewa ni kidogo kiasi cha kutoweza kuwa njia ya kutokomeza uvuvi haramu na kuwa fundisho kwa wavuvi haramu wengine.

Mapendekezo

Udhibiti uvuvi wa sangara ili kunusuru kiasi cha sangara kinachokadiriwa kuwapo kisitoweke. Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ihakikishe kwamba:

1. Uingiaji katika shughuli za uvuvi ziwani unadhibitiwa kwa njia ya usajili na utoaji wa leseni kwa vyombo vya uvuvi na wavuvi.

 

2. Kuwe na namna ya kujua kiasi cha sangara waliovuliwa na mtawanyo wa vyombo na zana za uvuvi zinazoingia ziwani.

 

3. Inatekeleza suala la msimu wa kufunga shughuli za uvuvi ili kulinda maeneo ya mazalia na maeneo ya makuzi ya samaki.

 

4. Ufugaji wa samaki unatiliwa mkazo ili kukidhi mahitaji yaliyopo

 

5. Kuwe na mgawanyo wa rasilimali ambao unazingatia vigezo vya ufanisi katika masuala ya kudhibiti uvuvi.

 

6. Ushirikiano kati yake na TAMISEMI unaboreshwa.

 

7. Kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama katika kushughulikia tatizo la kupungua sangara Ziwa Victoria.

TAMISEMI inapaswa kuhakikisha kwamba:

1. Serikali za Mitaa (Halmashauri) zenye shughuli za uvuvi zinadhibiti uingiaji katika shughuli za uvuvi kwa kuimarisha na kuzingatia usajili na kutoa leseni kwa vyombo vya uvuvi na wavuvi.


2. Serikali za Mitaa (Halmashauri) zinatunga sheria ndogo ndogo kuwezesha kutekeleza muundo imara wa kisheria katika kudhibiti uvuvi haramu katika maeneo yao.

Uratibu/ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi inapaswa kuhakikisha kwamba:

1. Utendaji wa Sekta ya Uvuvi unaratibiwa na kutathminiwa ipasavyo

 

2. Utendaji wa shughuli za Usimamizi, Udhibiti na Doria

Uvuvi (MCS), unaratibiwa na kutathminiwa ipasavyo

 

3. Njia za udhibiti zilizowekwa vinaratibiwa na kutathminiwa mara kwa mara

4. Kuna mfumo ambao utavisaidia vikundi vya usimamizi wa mialo (BMUs) kuwa na fedha za kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

 

5. Inajenga uhusiano wa kazi wa karibu na Halmashauri zenye shughuli za uvuvi.

TAMISEMI inapaswa kuhakikisha kwamba:

1. Halmashauri zenye shughuli za uvuvi Kanda ya Ziwa zinaratibu na kufadhili shughuli za uvuvi za BMUs ipasavyo; na

2. Halmashauri zenye shughuli za uvuvi Kanda ya Ziwa zinaratibu na kutathmini njia za udhibiti wa shughuli za uvuvi mara kwa mara.

Kupambana na uvuvi haramu

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi inapaswa kuhakikisha kwamba:

1. Inatekeleza mpango kazi wa kanda wa nchi wanachama wa kutokomeza uvuvi haramu, usioripotiwa na kudhibitiwa kwa kuboresha shughuli za uratibu wa shughuli za uvuvi, udhibiti na doria;


2. Inaanzisha hifadhidata “database” na kufanya mapitio ya taarifa hizo mara kwa mara kwa ajili ya kubadilishana habari na Taasisi ya Uvuvi Ziwa Victoria (LVFO), Vituo vya Usimamizi, Udhibiti na Doria Uvuvi, Halmashauri zenye shughuli za uvuvi Kanda ya Ziwa na wadau wengine.


3. Kampeni za uelimishaji kwa wadau wote wa Ziwa Victoria zinafanyika ipasavyo

 

4. Hatua muhimu za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wahalifu wote.

TAMISEMI inapaswa kuhakikisha pia kwamba halmashauri zinachukua hatua za kisheria dhidi ya wahalifu wote.


1877 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!