Baba mzazi wa mwanafunzi aliyeruhusiwa na Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi iliyoko Kibaha, Pwani kufanya mtihani wa taifa kwa mwaka jana akiwa mjamzito amedhamiria kuishtaki shule hiyo kwa kuharibu ndoto za mwanaye.

Egbert Bayi, baba mzazi wa mwanafunzi (jina linahifadhiwa) anataka kuishtaki shule hiyo ili imlipe gharama zote alizozitumia kumsomesha mwanafunzi huyo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne alipopata ujauzito.

Mbali na gharama hizo anataka kuishtaki shule hiyo ili imlipe fidia ya kusababisha mwanaye kupata ujauzito akiwa shuleni hapo na shule kuficha taarifa hizo.

“Ni dhahiri shule ilishindwa kumlinda mwanangu, mimi nilimkabidhi shuleni ili apate elimu lakini cha kushangaza uongozi wa shule akiwemo Mkurugenzi wa Shule (Anna Bayi) walipogundua mwanangu amepata mimba wao walinificha.

“Wakati alipobainika kuwa na mimba sikuambiwa ilhali muda mwingi nilikuwa nashinda shuleni pale, nilikuwa na kazi ya kusambaza nyama shuleni, lakini walimu na mkurugenzi hawakuniambia hadi kilipokaribia kipindi cha kufanya mtihani wa taifa,” amesema Egbert.

Kinachomsukuma kufikia uamuzi huo ni kitendo cha Mkurugenzi wa shule hiyo, Anna Bayi, ambaye ni mama yake mzazi kumuandama kwa tuhuma kwamba ndiye anayevujisha taarifa hizo hadi kusababisha mgogoro wa kifamilia.

“Kitendo cha JAMHURI kuandika kwamba Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi imeruhusu mwanafunzi mjamzito kufanya mtihani wa taifa wa kumaliza kidato cha nne kimeibua mgogoro mkubwa katika familia yetu. Mimi na mama kwa sasa hatuelewani. Ananichukia na hataki kuniona,” amesema Egbert.

Amesema shule hiyo ndiyo iliyosababisha ashindwe kumhoji mwanaye ili amtaje aliyempa mimba badala yake walimweleza akae kimya ili kulinda heshima ya shule.

Kutokana na hali ilivyo kwa sasa anadai ili mtoto wake aweze kutendewa haki anataka kuifungulia mashtaka shule hiyo kwa kuwa ndiyo iliyoshauri kuachana na harakati za kumtafuta aliyempa ujauzito mwanafunzi huyo.

“Mkuu wa shule alisema tukianza kumchokonoa mtoto wetu aeleze nani aliyempa mimba, cha kwanza taarifa zitasambaa, hivyo hatafanya mtihani wa taifa, vilevile atazalishwa ovyo na watu wengine,” amesema.

Amesema mwaka jana wakati wa kufanya sherehe za kuhitimu kidato cha nne katika shule hiyo, ambazo zilifanyika wiki moja kabla ya kuanza mtihani wa taifa ndipo alipoelezwa kuwa mwanaye amepata mimba.

“Nilisikitika, mke wangu akaanza kulia lakini hatukuwa na jinsi kwani tulichagua kufuata ushauri tuliopewa na uongozi wa shule wa kukaa kimya ili mtoto wetu aweze kufanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne,” amesema.

Kutokana na shule kuhusika moja kwa moja katika kudhibiti taarifa za ujauzito huo kutojulikana kwa watu, amesema haiwezi kujiondoa kwenye kashfa ya kumharibu mwanaye.

Mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) alifanya mtihani huo kwa namba S 1437/0002 katika matokeo ya mtihani yaliyotangazwa Januari mwaka huu, alifaulu kwa kupata daraja la pili lenye alama 20 (Division II, 20).

JAMHURI limeelezwa wakati anabainika kwamba ni mjamzito, tayari ujauzito huo ulikuwa umetimiza miezi saba na kwa kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 16.

Mmoja wa wafanyakazi wa shule hiyo ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini ameliambia JAMHURI kuwa kubainika kwa mwanafunzi huyo kulitokana na utaratibu wa kupima afya za wanafunzi shuleni, hasa upimaji wa mimba kwa wanafunzi wa kike.

Inadaiwa kuwa kutokana na mwanafunzi huyo kuwa mwanafamilia ya mmiliki wa shule hiyo, ilipobainika kuwa mjauzito suala hilo lilifanywa siri.

“Familia ilifanya hivyo kulinda heshima ya shule na jina la shule lisichafuke,” kimesema chanzo chetu.

Kumekuwa na madai kutoka vyanzo vya habari vya gazeti hili kwamba, mbinu za kuficha suala hilo ziliratibiwa na mmoja wa viongozi waandamizi wa shule hiyo kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Shule, Anna Bayi, ambaye ni bibi wa mwanafunzi huyo.

“Shule ilipobaini kuwa (mwanafunzi) ana ujauzito wa miezi saba, bibi yake, kwa kushirikiana na mkuu wa shule walimruhusu afanye mtihani, wakakubaliana suala hilo kulifanya siri hadi kwa wazazi wa (jina linahifadhiwa) wasijue mpaka hapo mtihani wa taifa utakapokwisha,” amesema mfanyakazi huyo.

Hata hivyo, baada ya kumaliza mtihani na kuhitimu elimu ya sekondari, Januari mwaka huu, mwanafunzi huyo alijifungua mtoto wa kiume na kumpa jina (linahifadhiwa). Huduma ya kujifungua alipatiwa katika Hospitali ya Aga Khan iliyopo jijini Dar es Salaam.

Ester Minja, ni mama mzazi wa mwanafunzi huyo, amefuatwa na Gazeti la JAMHURI ofisini kwake na kueleza kuwa anafahamu kila kitu kuhusu mwanaye kubebeshwa mimba, lakini hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo kwa undani.

Amesema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu mtoto huyo haishi naye na kwamba, kimepita kipindi kirefu bila kuwa karibu na mwanaye huyo na anayeweza kuzungumzia hilo zaidi ni bibi yake ambaye ndiye mlezi wake kwa sasa.

“Siwezi kuongea chochote kuhusu (mwanafunzi huyo) kwa sababu hapa niko kazini na suala hili mnalotaka kujua ni la kifamilia, kwani mpaka mnanifuata ofisini kwangu hampajui nyumbani kwangu? Kwa nini hamjanipigia simu, kwanza, nani kawaeleza?

“Kama mnataka kujua suala hili mngenifuata nyumbani na si hapa kazini, nakwambieni siwezi kuongea chochote, hata mkinifuata nyumbani msitegemee kuambiwa lolote, siwezi kulizungumzia suala hilo, mtafuteni bibi yake,” amesema Minja.

Baada ya mazungumzo hayo, Minja akiwa katika hali ya hasira akaanza kuondoka huku akiomba kufahamu jina la mtu ambaye ametoa taarifa hizo kwa Gazeti la JAMHURI.

JAMHURI lilimtafuta mwalimu mkuu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Yasintha, ambaye alieleza kuwa hafahamu lolote kuhusu tukio hilo kwa sababu hakuwepo shuleni hapo kwa mwaka jana.

“Mimi nimeletwa shuleni hapa mwaka huu, mwalimu mkuu aliyekuwepo kwa mwaka jana unaweza kumuuliza akakupa ufafanuzi,” amesema Yasintha.

Ameongeza kuwa mwalimu mkuu aliyekuwepo mwaka jana kwa sasa yupo masomoni na kwamba mkuu huyo pamoja na mkurugenzi wa shule hiyo ndio wenye kuweza kuzungumzia suala hilo kwa undani.

JAMHURI limezungumza na mkurugenzi wa shule hiyo, Anna Bayi na kukana kutokuwa na taarifa za mwanafunzi mjamzito kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne kwa mwaka jana katika shule yake.

“Hilo haliwezekani, yaani mwanafunzi awe na ujauzito wa miezi saba halafu ashindwe kubainika? Kwenye chumba cha mtihani chenye wasimamizi kama wanane wakiwamo watu wa Ofisi ya Rais, hicho kitu hakiwezi kutokea, sijui atavaa nguo gani ambazo zinatamficha mimba hiyo isionekane?” alihoji Sangoma.

Hata hivyo, anakiri kwamba suala hilo linaweza kutokea na asifahamu kwa sababu amekuwa na majukumu mengi ya kikazi shuleni hapo.

“Hapa tunapambana na mengi, watoto tunawafundisha malezi kila siku lakini hawasikii, hilo linaweza kutokea ikawa bahati ya mwanafunzi huyo kufanikiwa kufanya mtihani bila kubainika kwa sababu baadhi ya wanawake wana maumbile ambayo huwaficha na kushindwa kujulikana hadi siku ya kujifungua,” amesema Sangoma.

Alipoelezwa kuhusika katika kuficha taarifa za ujauzito wa mwanafunzi kwa kushirikiana na mkuu wa shule hiyo, alisema suala hilo halifahamu.

Hata hivyo baada ya kuelezwa kwamba mwanafunzi anayetajwa ni mjukuu wake, alisema hilo halimaanishi kwamba anaweza kumsaidia kumvusha kwenye tuhuma kama hizo na jambo hilo lisihusishwe na shule yake.

“Shule haihusiki kumpa mimba mwanafunzi, kama wazazi wake walishindwa kumpa malezi ya kutosha wasitake kuchafua jina la shule yetu kwa hoja kama hiyo.

“Hata hivyo, mtihani umekwishafanyika nyinyi gazeti, sijui la JAMHURI mnafuatilia suala hili ili mfaidike na nini?

“Kama mtoa taarifa kwenu alikuwa na mapenzi mema na shule yetu, kwa nini hakuja hapa shuleni kutueleza kabla ya kulifikisha kwenu?

“Kwa hiyo nyinyi mmefuatilia jambo hili ili iweje? Haya, mwanafunzi huyo ameshajifungua, Mungu kampitisha bila sisi kumgundua, nyinyi mnataka sisi (shule) tufanye nini kwa mwanafunzi ambaye ameshamaliza shule?” amehoji Anna.

Alipoelezwa kwamba yeye ndiye mlezi wa mwanafunzi huyo na mpaka sasa anaishi naye nyumbani kwa mujibu wa mama mzazi wa mtoto huyo (Ester Minja), alisema taarifa hizo zinaonekana kulenga kuchafua jina la familia ya Bayi kwani mtoto huyo hakai kwake.

“Mume wangu hana mpango na kugombea aina yoyote ya uongozi, hana mpango wa kuwa diwani, mbunge wala kugombea nafasi yoyote katika siasa, sasa sijajua mnaleta taarifa kama hizo ili nini kitokee?” alihoji.

Majibu ya wizara

Akizungumzia suala hilo wiki kadhaa zilizopita, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Dk. Ave-Maria Semakafu, alimweleza mwandishi wetu kuwa wizara haisimamii uendeshaji wa shule hiyo moja kwa moja.

“Wizara haifanyi usimamizi wa moja kwa moja wa shule hiyo pamoja na shule nyingine, masuala ya uendeshaji wa shule yamo mikononi mwa uongozi wa shule. Kuna mambo yanayosimamiwa na wizara katika shule hizi, mambo ya jumla ya kitaifa na si uendeshaji wa kila siku,” alisema kiongozi huyo wa wizara, akielezea nafasi ya wizara katika masuala ya elimu.

Sera ya elimu

Sera ya elimu pamoja na mambo mengine, inaeleza kuwa msingi wa elimu na mafunzo utajikita katika kumjengea Mtanzania misingi bora ya malezi, maadili, ujuzi, umahiri na kumwezesha kujitegemea.

“Elimu ya kujitegemea itaendelea kuongoza utoaji wa elimu na mafunzo kwa kuzingatia mabadiliko yanayotokea katika jamii, kisiasa, kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia,” inaeleza sera hiyo.

Kuhusu dira, sera inaeleza malengo ya kuwa na Mtanzania  aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo  chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya taifa, wakati dhima ikilenga kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo pamoja na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

By Jamhuri