Serikali ikiwa mbaya, CCM itakuwaje nzuri?

Vinara wawili, kati ya wale wanaotuhumiwa kuifanya Loliondo isitawalike, wamewatumia wanasheria wao kuniandikia barua wakitaka ‘nisiwaguse’ kwa chochote kinachoendelea Loliondo.
Edward Porokwa na Maanda Ngoitiko, wanaamini kwa kuninyamazisha mimi na Gazeti la JAMHURI, ‘sifa na utukufu’ wao katika Loliondo, vitaendelea kudumu! Maandishi ya wanasheria wao yameandikwa kwa lugha ya mbwembwe nyingi, lakini sikuona mahali walipokanusha yaliyoandikwa juu ya Loliondo na ushiriki wao kwenye migogoro.
Loliondo na Ngorongoro kwa ujumla wake ni mali ya Watanzania wote. Haiwezekani sehemu moja ya nchi ikawa na vinara wa kuchochea migogoro halafu tukazuiwa. Kupitia maandishi yetu, wananchi wengi wametambua nini kilichojificha ndani ya NGOs zaidi ya 30 ndani ya wilaya moja. Wananchi wametambua namna watu hawa (NGOs) wanavyopokea mabilioni ya shilingi kwa kisingizio cha kuwatetea wananchi, ilhali wakiwa hawasaidii chochote.
Watoto wa wafugaji wameendelea kuwa mbumbumbu ili wawe vitegauchumi vya hawa wanaojiita watetezi wa haki za binadamu. Utateteaje haki za binadamu kama huzuii utumikishwaji wa watoto malishoni, au kuwapatia elimu yenye kulenga kuwakomboa?

Porokwa, ambaye ni kiongozi wa NGO ya Pingos Forum, ni msomi. Kama msomi, anajua hoja hujibiwa kwa hoja. Hoja hazijibiwi kwa vitisho na mazuio. Ajitokeze ajibu yale anayoamini ni uongo.
Kwamba Porokwa ana ushirika wa karibu mno na maadui wa nchi wa ndani na nje, hilo halina mjadala. Kwamba Porokwa amekuwa sehemu ya wanaoyumbisha mambo Loliondo, hilo ni la kweli. Kwamba Porokwa amekuwa akipinga mipango mingi na halali ya Serikali, hilo halipingiki.

Kwamba Porokwa, Maanda na washirika wenzao wamekuwa na ubia wa kimaslahi na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na Mkuu wa Mkoa wa Arusha; pamoja na magenge ya Wazungu wanaowafadhili, hilo lina ushahidi. Kwamba wawili hawa wamekuwa na ushirika na raia wa kigeni ambao kila uchao wanaibua mbinu za kuivuruga Loliondo, hilo nitakufa nikiliamini maana ni la kweli.
Mara kadhaa nimesema watu wanaoleta chokochoko nchini mwetu wamekuwa wakitiliwa shaka uraia wao. Maanda yumo kwenye kundi hilo. Hili si langu, bali ni la mamlaka za nchi.
Idara ya Uhamiaji imeanza uchunguzi kuwapata watumishi wake walioshiriki kumpa hati ya kusafiria, Maanda ambaye ni Mkurugenzi wa shirika lisilo la serikali (NGO) la Pastoral Women Council (PWC).

Anadaiwa kuwa ni raia wa Kenya
Awali, Maanda alikuwa na hati ya kusafiria yenye jina la Maanda Sinyati Ngoitiko, yenye Na. AB 113266 iliyotolewa Dar es Salaam, Januari 21, 2006. Hati hiyo iliisha muda wake Januari 20, mwaka jana.
Alipokwenda Uhamiaji wilayani Ngorongoro ili kupata hati nyingine, Uhamiaji waligoma, wakimtaka atoe vielelezo vya kuthibitisha uraia wake wa Tanzania.
Tangu wakati huo hakuweza kuthibitisha uraia wake, kwa hiyo suala lake likawa bado linashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Wakati hayo yakiendelea, Maanda akawa amepata hati nyingine ya kusafiria jijini Dar es Salaam, ilhali fomu zake za maombi zikiwa bado zipo Ngorongoro.
Msemaji wa Uhamiaji, AllyMtanda, anasema Maanda amezuiwa kusafiri hadi hapo suala lake litakapokuwa limemalizwa. Vituo vyote vya Uhamiaji nchini vimejulishwa kuhusu hatua hiyo.
Haya siyafanyi mimi. Yanafanywa na Uhamiaji ambacho ndicho chombo chenye dhima hiyo. Maanda ananizuia nisiyaandike haya. Nikikubaliana naye nitakuwa siitendei haki nchi yangu. Wajibu wa mimi kushiriki kuilinda nchi yetu ni wajibu wa kikatiba. Huu si utashi wa mtu.

Lakini mwenye sakata la Lolindo, kwa namna ya kipekee, mtu unaweza kubaini mambo mengi.
Unapoona Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wanakuwa washirika wa NGOs, na hata kujipanga kukoleza migogoro, basi ujue kuna tatizo kubwa la kimaadili. Viongozi walioapa kulinda maslahi ya nchi na wananchi wanapogeuka kuwa mawakala wa NGOs na hata kushiriki kuzipatia mbinu za kuibana Serikali, hao ni wasaliti.
Kwa nyakati tofauti wameshiriki kuhakikisha kuwa Maanda anapata hati ya kusafiria licha ya utata wa uraia wake. Siyo siri kwamba wamekuwa wakishinikiza apate hati hiyo.

Wiki moja iliyopita tumeambiwa Maanda amejitoa Chadema na kujiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM)! Eti anasema anarejea CCM baada ya kuridhishwa na kasi ya utendaji kazi ya Rais John Magufuli! Ajabu kweli kweli.
Hii si habari ya kushangaza hata kidogo. Mwaka jana niliandika juu ya habari hii ya Maanda kurejea CCM. Mpango ulikuwa umeandaliwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Michael Laizer. Mwenyekiti huyu alipanga ziara katika wilaya za Ngorongoro  kwa kile alichosema ni kuimarisha uhai wa chama, ingawa nyuma ya pazia ilikuwa kumpokea Maanda.
Mwenyekiti huyu ndiye Mwenyekiti wa Hifadhi za Jamii (WMAs). Huyu ni muumini mkuu wa uanzishwaji wa WMA Loliondo kama ilivyo kwa kina Maanda, Porokwa, DC wa Ngorongoro na RC wa Arusha. Kwa taarifa tu ni kuwa tayari kuna maeneo ambayo wakubwa fulani fulani wilayani Ngorongoro na katika Mkoa wa Arusha wameanza kujiandalia kuyamiliki wakiamini kuwa Waziri Mkuu au Rais atatangaza uanzishwaji wa WMA ambazo ni chaguo la viongozi, lakini wananchi wenyewe katika vijiji hawataki kabisa kusikia hicho kitu. Majina na sehemu hizo tunavyo.

Laizer amekuwa akipigana kuhakikisha Maanda anapata hati ya kusafiria, kwani mara kadhaa amewahusisha watu wa Uhamiaji. Baada ya kuona mbinu mbalimbali zimeshindikana, kilichofanyika ni kumshauri Maanda aachane na Chadema. Aingie CCM. Awe anaketi karibu na wakubwa wa chama tawala na Serikali. Imani yao ni kuwa mbinu hiyo itamsaidia kupata hati ya kusafiria na kuachwa ‘kufuatwafuatwa’ na vyombo vya dola kama ilivyo sasa!
Chama Cha Mapinduzi kina misingi yake. Sidhani kama ni kweli chama hiki kina ukame wa wanachama kiasi cha kukifanya kiwapokee na kuwatumia watu wanaoihujumu Serikali ya chama hicho hicho. Sidhani kama CCM ni chama chepesi kinachoweza kumpokea kila anayetaka kujiunga nacho bila vigezo wala masharti.

Huyu huyu anayerejea CCM, akishirikiana na Porokwa, wiki kadhaa zilizopita NGOs zao ziliwaingiza nchini kinyemela raia wawili wa kigeni – Mfaransa, Profesa Jeremie Gilbert, na Mwingereza, Luke Tchalenko – ambao walifika Loliondo na kuchukua maelezo na picha ambavyo vitatumika kuichafua Tanzania kwa kuonesha kuwa inakiuka haki za binadamu. Wageni hawa walipiga picha na kuchukua maelezo yenye kuonesha kuwa Serikali ya CCM ni ya watu waonevu na wasiowatendekea haki wanaLoliondo.
Gilbert anatoka shirika la kimataifa la Minority Rights Groups (MRG), ilhali Tchalenko ni mpiga picha za filamu na majarida maarufu Uingereza, Kanada na Marekani ya The Times, The Globe and Mail na World of Interiors.
Raia mwingine wa Sweden, Suzan Nordlund, ameshafukuzwa nchini mara kadhaa kwa PI, lakini akawa anasaidiwa na NGOs za hawa watu kupenya Loliondo kufanya uchochezi.

Huyu mtu aliyeuaminisha ulimwengu kuwa Loliondo kuna uonevu, anapata wapi ujasiri, si tu wa kuisifu CCM, bali kuamua kujiunga nayo! Je, anajiunga CCM kuendeleza maovu ambayo kwa miaka yote amesema inawatendea wanaLoliondo? Kwa undumilakuwili  huu, tunaposema Loliondo hakuna migogoro isipokuwa kuna kelele tu za NGOs zinazofaidi fedha za wafadhili, tunakosea?
Je, ni kweli nafsi ya Maanda inamtuma kwa dhati ya moyo wake ampende Mwenyekiti John Magufuli, anayeongoza chama chenye Serikali inayowatesa wananchi wa Loliondo? Kama migogoro ya Loliondo haijamalizwa na Serikali ya CCM, kitu gani kimemvuta Maanda hata aone sasa CCM ndiyo mahali sahihi kwake?

Lakini kwa wanaojua staili za kuishi za watu wenye utata hawashangazwi na kilichofanywa na mwanamama huyu. Mara zote CCM imetumiwa kama kichaka cha watu wasio waungwana kwa kuamini kuwa hawataguswa. Sidhani kama fomula hiyo inaweza kuwafaa kwa uongozi huu wa sasa ambao hauna soni kwa waovu.
Niseme tu kuwa Loliondo kama yalivyo maeneo mengine nchini, rasilimali zilizoko huko ni rasilimali za Watanzania wote. Kusijitokeze genge la watu kujiona wana haki zaidi kwa eneo hilo kuliko Watanzania wengine. Tunapotetea kumalizwa kwa migogoro Loliondo maana yake tunatetea uhifadhi. Bila Loliondo hakuna Serengeti. Huo ndiyo ukweli.

Tunaposikia watu fulani wakipinga kupunguzwa au kuondolewa kwa mifugo ya raia wa kigeni wilayani Ngorongoro, tunapata hisia kwamba huo ni uchochezi kwa sababu tunaona wananchi wa maeneo yenye rasilimali kama Mtwara, Geita, Mara, Msitu wa Hifadhi wa Amani (Muheza) na kwingineko wakiheshimu uamuzi wa Serikali wa matumizi ya rasilimali kwa wananchi wote.
Mgogoro wa Loliondo umedumu kutokana na viongozi wakuu wa Serikali wilaya na mkoa kuwa upande wa NGOs, hasa kwenye suala la kutengwa kwa eneo la kilometa 1,500 kwa ajili ya uhifadhi. Eneo hilo la Loliondo ndilo lenye asilimia 50 ya vyanzo vyote vya maji yanayoingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Kwa maana hiyo hatuna wajibu wa kuheshimu tafiti mbalimbali za wataalamu wa ndani na nje ya nchi kuhusu umuhimu wa kuilinda Loliondo.
Nihitimishe kwa kuwakaribisha Maanda na Porokwa kujibu hoja kwa hoja badala ya kutumia wanasheria kutuzima kuyasema haya mambo ambayo tunaamini yana maslahi mapana kwa wananchi wa Loliondo na Watanzania kwa jumla.

Namwuliza Maanda, Serikali (anayosema inawakandamiza wananchi wa Loliondo) inawezaje kuwa mbaya, lakini CCM inayoongozwa na huyo huyo anayeongoza kukandamiza ikawa nzuri? Werevu hawatopata shida kutambua kuwa kilichomsukuma kujiunga CCM ni kujaribu kupata mwanya wa kunyoosha mambo yake yaliyokwama. Alichokosea ni kupuuza ukweli kwamba mkuu wa Serikali ndiye huyo huyo mkuu wa CCM.