Hivi karibuni Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA) iliwekwa ‘kitimoto’ na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyo chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na makamu wake, Deo Filikunjombe wa Ludewa.
Ulikuwa ni mkutano uliokutanisha Wakurugenzi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali, SSRA na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kikubwa kilichogunduliwa huko ni madeni makubwa ya Serikali kwa mifuko hiyo hali inayofanya ihatarishe uhai wake wa kuhudumia wanachama wao.
Uongozi wa Gazeti la JAMHURI hauna budi kujisifu kwa kuwa chombo cha kwanza kutangaza kuhusu hatari ya kifo kinachonyemelea mifuko ya hifadhi ya jamii. Habari hiyo ilichapwa kwa mara ya kwanza Agosti 12, mwaka huu.
Ilikuwa ni habari iliyochapishwa katika ukurasa wake wa kwanza ikiripoti kwamba kuna madeni sugu ya Serikali yanatishia uhai wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Kutokana na taarifa hiyo, SSRA ikatoa angalizo kwa Serikali na kuitaka ilipe madeni yote ambayo kwa ujumla yanafikia Sh 8.43 trilioni.
Nasi tunaungana na mamlaka hiyo ya SSRA ambayo imetoa kilio kuwa madeni hayo yametokana na Serikali na taasisi zake kukopa kwenye mifuko hiyo huku wadau hao wakichelewa kulipa.
Baadhi ya mikopo hiyo ni kwa asasi mbalimbali kutopeleka michango ya wanachama hali inayotishia uhai wa mifuko hiyo.
Kwa mujibu wa SSRA madeni hayo ni,  Sh 7.9 trilioni ni deni la PSPF, PPF Sh 192 bilioni, NHIF (Sh 107 bilioni), NSSF (Sh 467 bilioni), PSPF (Sh 4.29 bilioni), LAPF (Sh 170 bilioni) na GEPF inadai Sh 6.86 bilioni.
Hakuna ubishi kwamba hatma ya mifuko ni mbaya kwani mwenendo huu wa Serikali na taasisi zake kuendelea kukopa na kutopeleka michango ya wanachama wake, ni wazi kwamba mifuko hiyo itaathirika kwa kiasi kikubwa.
Mifuko hii ni muhimu kwa taifa na ikiendeshwa vema itasaidia jitihada za kupambana na umaskini kupitia malipo ya pensheni inayoendelea kuyatoa kwa wanachama wake wakiwamo wale waliostaafu au waliopatwa na majanga wakiwa kazini na kupoteza nguvu za kufanya kazi.
Kwa kuwa tunatambua umuhimu wa mifuko hiyo bila shaka hatuna budi sasa kuilinda kwa kuiimarisha na siyo kupunguzwa uwezo wake, lakini kitendo cha ‘kuitafuna’ kiasi hiki hakuna tafsiri nyingine zaidi ya kuona kuwa inauawa.
Kutokana na hali hiyo sisi wa JAMHURI tunaona kwamba Serikali haina budi kulipa madeni hayo kama ilivyoshauriwa SSRA.

1864 Total Views 11 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!