Takribani wiki mbili baada ya Marekani kuiingiza Tanzania katika orodha ya nchi ambazo wahamiaji wake hawaruhusiwi kuingia nchini humo, Serikali imesema bado haijapata taarifa rasmi kuhusiana na suala hilo.

Aidha, Serikali imesema pia haijapata taarifa zozote kuhusiana na katazo la kwenda nchini humo alilopewa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Akizungumza na JAMHURI Jumamosi iliyopita,  Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Emmanuel Buhohela, amesema bado serikali iko gizani kuhusiana na masuala hayo.

JAMHURI ilitaka kujua msimamo wa serikali kwa hatua za Marekani kuiweka Tanzania katika nchi zilizowekewa vikwazo kwa wahamiaji wake kuibgia Marekani.

Aidha, gazeti hili pia lilitaka kujua msimamo wa Serikali kuhusiana na marufuku iliyowekwa na marekani kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, na mke wake kuingia nchini humo.

“Kwa kawaida Serikali inafanya kazi kupitia taarifa rasmi. Kuhusiana na masuala uliyouliza, hadi sasa ninapozungumza na wewe bado serikali haijapata taarifa zozote kuhusiana na mambo hayo,” anasema Buhohela.

Anaeleza kuwa hiyo ndio sababu iliyoifanya serikali kutotoa kauli yoyote kuhusiana na masuala hayo hadi sasa.

“Hata sisi tunayasoma mambo haya kwenye mitandao lakini Serikali haifanyi kazi kupitia ‘rumours’ (tetesi). Kunakuwa na taarifa rasmi za kidiplomasia ambazo huletwa Serikalini ndio ambazo zinafanyiwa kazi,” alifafanua.

Buhohela alisema labda Ubalozi wa Marekani nchini una majibu kuhusiana na masuala hayo kwani nchi hiyo ndiyo inatajwa kutoa matamko hayo.

Januari 31, mwaka huu Marekani iliitangaza Tanzania miongoni mwa nchi sita duniani ambazo zimeongezwa katika orodha ya nchi ambazo nchi hiyo haitapokea wahamiaji wake.

Nchi nyingine katika orodha hiyo ya nyongeza ni Nigeria, Myanmar, Eritrea, Kyrgyzstan na Sudani.

Kuongezwa kwa Tanzania katika orodha hiyo kuliwashangaza watu wengi.

Akiandika katika mtandao wa twitter,  Nako Mbelle, alieleza kuwa Tanzania inatambulika kama moja ya mataifa yenye utulivu na amani barani Afrika. Akabainisha kuwa kwa kuwa si Watanzania wengi wana hati za kusafiria, hivyo katazo hilo linaweza kuwaathiri watu wachache tu.

Lakini akahoji; “Kwa nini Tanznaia imewekwa kwenye orodha hiyo?”

Wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wanasema hatua ya Tanzania kuwekwa kwenye orodha hiyo, ukichanganya na katazo la Makonda kuingia nchini humo, ni ishara kuwa uhusiano baina ya Marekani na Tanzania, ambao ulionekana kuwa imara sana kwa miaka mingi, sasa umeyumba.

Tanzania ni kati ya nchi chache sana barani Africa ambazo zimewahi kutembelewa na viongozi wengi wa juu wa Marekani, ikiwa ni ishara ya nchi hiyo tajiri zaidi duniani kuzikubali sera za Tanzania.

Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Tanzania imetembelewa na marais wawili wa Marekani na viongozi wengine kadhaa wa ngazi za juu wan chi hiyo.

Kati ya Agosti 28 na 29, 2000, Rais Bill Clinton aliitembelea Tanzania. Alitua jijini Arusha ambako pamoja na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, pia alikutana na aliyekuwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, Rais wa zamani wa Afrika kusini, nelson Mandela.

Baadaye akafuatia Rais mstaafu wa nchi hiyo, George W. Bush, ambaye aliitembelea Tanzania Februari 2008 na kukytana na rais Mstaafu, Jakaya Kikwete. Ni katika ziara hiyo Bush alisaini mktaba wa Millenium Challenge.

Pamoja na Dar es Salaam, katika ziara hiyo Bush alitembelea pia Arusha ambako alitangaza mpango kabambe wa Marekani kulisaidia bara la Afrika kukabiliana na Ukimwi na malaria.

Ni kupitia ziara hiyo Rais Bush aliahidi msaada wa mamilioni ya vyandarua kwa nchi za Afrika.

Julai 2013, Barack Obama, Rais ambaye amerithiwa na Trump, aliweka historia kwa kuitembelea Tanzania. Pamoja na kukutana na Rais Kikwete na kufanya mazungumzo, Obama pia aliweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu ya watu waliouawa katika shambulio la kigaidi katika ubalozi wa nchi hiyo mwaka 1988.

Obama pia alitumia ziara yake hiyo nchini kutangaza mpango wa serikali yake kulisaidia bara la Afrika katika masuala ya kuimarisha upatikanaji wa nishati chini ya mpango unaojulikana kama Power Africa.

Aprili 2016, Tanzania pia ikawa mwenyeji wa Hillary Clinton, mke wa Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton. Baadaye, Hillary aliteuliwa na Obama kuwa waziri wa Mambo ya Nje. Wakati Obama alipomaliza ngwe yake ya Urais, Hillary aliteuliwa na chama chake cha Democrat kuania Urais mwaka 2016 lakini alipigwa mwereka na Rais wa sasa, Donald Trump.

Rais Clinton mwenyewe ameshawahi kuitembelea Tanzania mara kadhaa baada ya kutoka madarakani. Shirika analoliendesha la Clinto Foundation linatekeleza programu kadhaa nchini hasa katika sekta ya afya.

By Jamhuri