Kwa miezi miwili sasa kumekuwa na msuguano kati ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala na mamlaka za Wizara ya Afya, Maendedeo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Wizara ya Afya imetoa matamko mawili ambayo yote yalipingwa na Matabibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala. Katika matamko hayo mawili, tamko la pili ndilo lilikuwa na uzito mkubwa na kuibua hisia miongoni mwa matabibu na hata wananchi.

Lakini tunaweza kujiuliza; je, mvutano huu unaozungumzwa una tija? Ukilisoma tamko la mwisho lina maelezo mengi, lakini kuna ambayo matabibu wamekubaliana nayo na kuna baadhi hawakukubaliana nayo. Moja kubwa ni Wizara kukataza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu afya ya mwanadamu na jinsi tiba asili inavyoweza kusaidia afya ya mwanadamu kuimarika.

Tayari Wizara imetoa vibali vya matangazo tu na si vibali vya kutoa elimu kwa umma. Ukilisoma tamko linasisitiza kuwa kumekuwa na taarifa zinazoweza kupotosha umma. Wizara haijatoa mifano ya namna umma unavyopotoshwa.

Hata hivyo, ukiangalia kwa undani utagundua kuwa wahusika wote wa tamko la waziri ni waumini wakubwa wa tiba za kisasa au za kimagharibi na wengi ndio washauri wa karibu wa waziri. Ni dhahiri kuwa matabibu wa tiba za kisasa hawataki kusikia matabibu wa tiba asili wakizungumzia magonjwa mbalimbali na sababu kubwa ni kwamba matabibu wa tiba asili hawana weledi wa kuzungumzia magonjwa hayo.

Inawezekana ni kweli japo taarifa za magonjwa mbalimbali si lazima uzipate kwa kuingia darasani Muhimbili au chuo chochote. Katika dunia ya utandawazi unaweza kupata elimu ya jambo fulani kwa kadri unavyotaka kujifunza. Lakini tunaweza jiuliza kwa sababu kumekuwa na madai ya upotoshaji katika kutoa elimu; je, suluhisho ni kuzuia au kuweka mifumo mizuri ya udhibiti wa hizo taarifa?

Je, wananchi hawana haki ya kupewa taarifa ya namna mimea tiba inavyoweza kubadilisha maisha yao kiafya? Na je, huko si kupoka haki ya kupata taarifa ambayo ni haki ya kikatiba?

Ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya matabibu wamekuwa wakitoa elimu kwa umma baada ya taarifa zao kuhakikiwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kutoa kibali ili vyombo vya habari viweze kurusha matangazo au elimu husika. Na kama kuna ambao walikuwa wakitoa elimu bila kuomba kibali kwenye Baraza hao walikuwa wanakiuka sheria na kanuni zilizopo. Na hilo ni kosa ambalo lina adhabu zake. Hapa swali litakuwa watu hao wamewahi kuadhibiwa? Kama hawakuwahi Baraza lilikuwa linafanya kazi gani?

Kwa maoni yangu kabla hata ya kutoa matamko, Wizara ilitakiwa kujichunguza na kuangalia utendaji wa vyombo vyake likiwamo Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala. Baraza limepewa majukumu mengi mno kisheria na hivyo basi linapasika kufanya kazi yake. Na katika mvutano huu Baraza linatakiwa kusimama na kuipigania Tiba Asili kwa kusimamia sheria kuhusu matangazo na elimu kwa umma ya tiba asili na tiba mbadala.

Sasa matamko yametolewa; je, huu mvutano unaweza kumalizwa vipi? Je, una tija kwa maslahi ya pande zote? Jibu la haraka ni kwamba mvutano huu hauna maslahi. Na ili kuuondoa mambo kadhaa yanaweza kufanyika:

1.    Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuendelea kusimamia majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye sheria.

2.    Kuweka utaratibu kuwa kama tabibu wa tiba asili anataka kuzungumzia magonjwa na tiba anayoweza kutatua shida hiyo, basi mtu au watu wenye utaalamu huo wa kufundishwa darasani watoe elimu ya ugonjwa au magonjwa yanayojadiliwa siku hiyo na mtaalamu wa tiba asili au tiba mbadala aje kuzungumzia mimea tiba inavyoweza kutibu au kutoa nafuu kwa ugonjwa unaozungumziwa.

 Na hili sio jipya, kwani tumeona kwenye vipindi kadhaa vya televisheni baadhi ya matabibu wakifanya hivyo. Kwa maana rahisi hapa ni kuangalia namna mpya ya kuboresha. Na ukweli ni kuwa kuzuia utoaji wa elimu kwa umma ni sawa na kuizika tiba asili. Na ikumbukwe vituo vya tiba asili si kama hospitali za kisasa ambazo zinajulikana na kutapakaa kila kona.

Watu hasa wale ambao wamepewa tiba kwenye hospitali za kisasa wanaposhindwa kupata ahueni ni lazima wajue wapi wanaweza kukimbilia. Na hilo linawezekana pale anaposikia na kupewa elimu juu ya ugonjwa unaomsumbua na namna tiba asili inavyoweza kutenda miujiza na kumrudishia mtu afya yake na kurudi kufurahia maisha kama watu wengine.

3.    Kwa mfumo wa Wizara ulivyo, kunahitajika kuwapo cheo cha Mganga Mkuu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala. Mtu atakayeteuliwa kwenye eneo hilo awe na weledi wa kutosha wa tiba asili na tiba mbadala. Na moja ya majukumu yake iwe kusimamia utendaji kazi wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na lingine kumshauri Waziri mambo yote yanayohusu tiba asili na tiba mbadala. Si jambo lenye afya kwa waziri kupewa ushauri na watu wa tiba za kisasa ambao hawaipendi tiba hii na wanaihofia wakidhani itafika wakati watu watakimbia hospitali wanazomiliki na kukosa wateja wa kununua dawa kwenye maduka wanayoyamiliki.

     Hii ni hofu isiyokuwa na mashiko yoyote wala utafiti wa kutosha. Utafiti uliofanywa na mwandishi kwenye kituo kimoja cha tiba asili na tiba mbadala umegundua kuwa wagonjwa wengi sana wanaofika kwenye vituo vya tiba asili ni wale ambao wamekwishapatiwa tiba katika zahanati na hospitali mbalimbali na kushindwa kupona au ugonjwa kujirudiarudia.

4.    Kuna haja ya kuwapo mijadala ya magonjwa na tiba na kubadilishana mawazo kati ya matabibu wa tiba za asili na wale wa kisasa na kupeana mawazo badala ya kupingana bila sababu. Ni vyema wananchi wakagundua kuwa nchi nyingi duniani tiba hizi mbili zimeunganishwa na zimetoa matokeo makubwa.

Ni vema ikaeleweka kuwa hizi tiba kwa maana ya tiba asili na tiba mbadala hazipaswi kuchukuliwa kama tiba kinzani. La hasha! Hizi ni tiba zinazosaidiana kuhakikisha afya ya mwanadamu inaimarika kwa namna Mungu alivyopanga. Na hapa nitahadharishe kuwa siku ikitokea (Mungu apishe hilo mbali) mgonjwa afariki akiwa anapatiwa huduma kwenye kituo cha tiba asili nashawishika kuamini kuwa kituo hicho na vingine vitaingia kwenye matatizo makubwa mno ikiwa ni pamoja na kufungiwa. Hili linaweza kufanyika kana kwamba hospitali za kisasa kila anayetibiwa lazima apone. Dhana hii si sahihi, na ndiyo maana mochwari zipo karibu kila hospitali kubwa kama kielelezo kuwa kuna wakati uwezo wa mwanadamu wa kutoa tiba unafikia ukomo; na Mungu anafanya kazi yake.

5.    Kuna haja ya kuanza kujiuliza na kutafakari juu ya hii tiba asili na kwa kuanzia kwa kujiuliza neno “asili” lina maana gani? Maneno tiba asili yana maana gani? Tiba mbadala ina maana gani? Nina hakika kuna watu wasomi waliobobea ambao hawawezi kutofautisha kati ya tiba asili na tiba mbadala. Si lengo la makala hii kutoa tofauti za maneno hayo. Hili ni muhimu kwa vile huko tunapoelekea kwa namna tiba hii inavyodhibitiwa na kuwekewa masharti u-maana wa neno “asili” katika tiba hiyo utaondoka.

Ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya tiba hii ni ya kurithi na wakati mwingine maelezo yakinifu ya kisayansi ya namna kwa mfano mti fulani unavyoweza, mfano kutibu ugonjwa sugu unaosumbua kina mama UTI hayawezi tolewa na tabibu wa tiba asili ila yeye anachojua na alichoambiwa ni kuwa mti huo ni tiba. Na huo ndiyo uasili wa tiba hiyo.

Nimalizie kwa kusisitiza mijadala kati ya matabiu wa kisasa na wale wa asili ni jambo muhimu sana.

6.    Mwisho, kama wadau wote wa afya watakuwa na nia njema bila kuangalia upande mwingine wa tiba kwa jicho hasi kama inavyojionesha kipindi hiki, basi kwa pamoja tunaweza kuimarisha afya za binadamu.

Ikumbukwe kuwa zaidi ya asilimia 80 ya dawa hospitalini zinatokana na miti shamba. Huko vijijini asilimia kama hiyo ya wananchi wanapona kwa miti shamba. Wakoloni walipokuja walivuruga maisha ya Waafrika kwa kuwafanya waamini miti shamba ni kama ‘uchawi’ au kitu kisicho na maana. Sasa Afrika ni huru. Tuache kasumba hiyo. Lakini Serikali inachopaswa kufanya ni kuhakikisha Tiba Mbadala haiingiliwi na matapeli.

 

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kama mdau wa tiba asili na tiba mbadala na kitaaluma ni mwanasheria. Anapatikana kupitia [email protected]

By Jamhuri