Picha ya Waziri MagembeSerikali imetenga Sh milioni 362 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi 973 Agosti mwaka huu ambao ni miongoni mwa waliopunjwa fidia zao wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya baada ya kuhamishwa katika vijiji  vyao kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amelileza JAMHURI, kwamba kutokana na agizo la Waziri Mkuu,  Julai 12 mwaka huu walikutana na wananchi hao wanaolalamika kupunjwa fidia zao katika mkutano uliowahusisha Wakuu wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe, Mkuu Wilaya ya Mbarali, Mbunge wa Mbarali, Wenyeviti wa Vijiji na Serikali za Mitaa kuendeleza kazi za kikosi kazi kilichoundwa na Waziri Mkuu aliyepita.

Makalla anasema kiasi hicho cha fedha kimetengwa kuwalipa waliobainika kupunjwa fidia zao baada ya uchunguzi na wale waliolipwa bila kufanyiwa tathmini watafanyiwa upya.

“Tuligundua kuwa mgogoro upo na kilichojitokeza ni kuuingiza katika siasa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita ili utumiwe kama kete ya kukubalika hasa kwa baadhi makada waliokuwa wanawania nafasi ya urais kupitia CCM akiwemo Lazaro Nyalandu,” anasema Makalla.

Nayalandu wakati huo alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii huku ikielezwa kwamba aliwapa matumaini ya kulipwa fidia zao wananchi hao bila ya kusikiliza madai yao na kufanya tathmini kwa kina.

Makalla anasema upanuzi wa Hifadhi hiyo ulitangazwa na Serikali kwa GN 28, lakini walichobaini ni kutoeleweka kwa wananchi walengwa ukihusisha vijiji  vipatavyo 7 vya awali hadi kufikia 34 vilivyomegwa na hifadhi.

Katika utekelezaji na mapendekezo waliyofikia, anasema waliopunjwa walipwe pia. Baadhi yao walilipwa fidia wakati hawamiliki chochote katika maeneo hayo jambo linaonesha wazi kwamba kulikuwa na ufisadi uliowahusisha baadhi ya viongozi walioshiriki mchakato huo.

“GN inafutwa kwa GN, hivyo TANAPA walipaswa kuwashirikisha wananchi katika kuwalipa na zaidi sana uangaliwe umuhimu wa hifadhi na mchakato unapaswa kufanyika upya huko huko waliko wananchi baada ya kujiridhisha kwamba kuna watu walilipwa bila kufanyiwa tathmini,” anasema Mkuu huyo wa Mkoa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Wahanga hao, Patrick Mnyota anasema awali waliopaswa kulipwa fidia walikuwa 4,749 zikiwemo taasisi mbalimbali, lakini idadi ilipunguzwa na kufikia 2,307 ambao wanatajwa kwamba wana haki ya kulipwa mapunjo ya fidia.

Mnyota anasema kwenye taarifa ya uchunguzi idadi ya watakaonufaika na malipo ya fidia ilipungua na kufikia 1,680 na kuwataka wengine wanaosalia warejee katika maeneo yao kwa ajili ya kuhakikiwa upya.

Mwenyekiti huyo amelieleza JAMHURI, kwamba wamesikitishwa na ubabaishaji unaoendelea kujitokeza kwenye suala hilo lililodumu kwa kipindi kirefu na kutishia kupotea kwa haki zao. Anasema idadi hiyo imeendelea kupungua hadi kufikia watu 973 wanaostahili kulipwa fida kwa viwango kati ya Sh Laki 3, 5 na Sh milioni 1.5.

“Mthamini Mkuu wa Serikali aliiomba Serikali kuchukua maoni ya upande wa pili kwa lengo la kumaliza mgogoro huo na kwamba kuwalipa watu wachache kutaibua mgogoro mkubwa zaidi huku wananchi wakiendelea kuteseka bila sababu za msingi.

“Katika kumaliza mgogoro huo tuliiomba Serikali kumlipa kila mhanga fidia ya Sh milioni 10 bila kujali ukubwa wa eneo la mtu, nyumba, ardhi na mali zingine zisizohamishika, lakini wamekataa na kutaka kuwalipa watu wachache na kiasi kidogo cha fidia,” anasema.

Hata hivyo, anasema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya iliwaleta wakaguzi kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kukagua maeneo yote ya mgogoro tangu mwezi Februari hadi Aprili mwaka huu, lakini matokeo ya ukaguzi huo hayajulikani licha ya kuwaahidi wananchi kwamba wangeyatoa mwishoni mwa Aprili.

Anasema wakaguzi hao walifanya ukaguzi TANAPA, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Wizara ya Maliasili na Utalii. Hata hivyo, kitendo cha kukalia ripoti hiyo kinaibua hofu ya kuendelea kwa mgogoro huo.

Pamoja na hayo ameiomba Serikali kuwapa maeneo mbadala kwa ajili ya shughuli zao za kilimo ili wajikwamue na hali ngumu ya maisha inayowakabili baada ya kuchukuliwa kwa maeneo yao.

Mgogoro huo tangu ulipoanza mwaka 2007 na baadaye 2008 walipohamishwa katika makazi yao kupisha upanuzi wa hifadhi ya Ruaha na baadhi yao walilipwa fidia ya kati ya Sh 4,000 na Sh 10,000 kwa ardhi yenye ukubwa wa ekari moja yenye mazao, majengo na gharama za usafiri.

Kiasi hicho cha fidia kilijumuisha gharama za usafiri na posho ya usumbufu wa pango la nyumba kwa miezi 36, kitendo kinachoelezwa na wakazi hao kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Serikali, Wilaya na TANAPA walijihusisha na ufisadi wa fedha hizo.

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alipofikishiwa malalamiko ya wananchi hao kabla ya kuondoka ofisini, aliamuru iundwe kamati iliyowashirikisha Wakuu wa Mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa na kuagiza wananchi hao wakutane na Mthamini Mkuu wa Serikali.

Machi 12, mwaka jana, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abas Kandoro, akiwa ameambatana na wakuu wa mikoa hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, walikutana na wananchi wilayani Mbarali na kusikiliza malalamiko yao.

Baada ya kusikiliza hoja zao, walitoa ahadi kwamba fidia ingelipwa, lakini hadi sasa hakuna ufumbuzi uliopatikana zaidi ya wahusika kutupiana mpira wakidai suala hilo liko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wakipofika huko wanaelezwa liko TANAPA, mara Kwa Waziri Mkuu na kwingineko lengo likiwa ni kuwahadaa wananchi hao.

Pascal Shelutete, Msemaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), anasema zimetengwa Sh milioni 362 kwa ajili ya kuwalipa fidia wote waliopunjwa awamu ya kwanza na kwamba fedha hizo zitalipwa kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mwezi huu.

2377 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!