Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema upimaji wa Kifua Kikuu (TB) na UKIMWI kwenye baa hautakuwa wa lazima.

Waziri wa Afya ameyasema hayo baada ya kuzuka hofu miongoni mwa wananchi ambapo baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakipotosha kuwa, upaji huo utafanywa kwa lazima.

Ameyasema hay wakati akizungumza katika maadhimisho wa miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), na kusema watatumia ushawishi kuhakikisha wananchi wanapimwa na kujua afya zao.

“Tutatekeleza mpango wa kusogeza huduma za upimaji TB na ukimwi kwenye baa, ila hautakuwa wa lazima, tutachofanya ni kuwashawishi wananchi kutumia fursa ya kusogezewa huduma hiyo,” alisema.

Alisema, wizara ipo katika mkakati wa kufanyia marekebisho ya Sheria ya UKIMWI kwa lengo la kuruhusu watu kujipima mwenyewe, kutoa fursa kwa vijana kuanzia miaka 15 kwenda kupima UKIMWI bila kupata ridhaa ya wazazi au walezi.

“Haya ni maeneo ambayo kama tutayafanyia marekebisho tutaweza kusaidia kuongeza kasi ya kudhibiti maambukizi ya UKIMWI,” alisema.

Katika hatua nyingine, kufuatia ombi lililotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, Justin Mwinuka, Waziri Ummy Mwalimu aliagiza kuanzia Julai mosi mwaka huu, watu wanaoishi wa virusi vya UKIMWI kupewa dawa za miezi mitatu badala ya sasa ya kupewa kwa miezi mwili.

Katika ombi lake mwenyekiti huyo alisema kuwa, utaratibu wa kupewa dawa za miezi miwili umekuwa ukiongezea gharama, kwani wamekuwa wakitakiwa kupima afya zao kila baada ya miezi mitatu.

Waziri huyo alisema utaratibu huo wa kuwapa dawa kwa miezi mitatu mitatu uanze haraka isipokuwa kwa wale ambao wanaonekana hawataweza kutunza dawa hizo au ambao ndio kwanza wanaanza kutumia dawa hizo.

By Jamhuri