Serikali yamkomoa msaidizi wa Mkapa

Kanali mstaafu Nsa Kaisi, ambaye amekuwa Msaidizi wa Rais Benjamin Mkapa kwa miaka mingi, amepokwa shamba lenye ukubwa wa ekari 14 katika eneo la Pugu Mwakanga mkoani Dar es Salaam.

Uvamizi huo umefanywa na kundi la watu mnamo Oktoba 19, 2011. Pamoja na kuwa na hati zote za umiliki halali wa eneo hilo, Serikali pamoja na vyombo vyake, hasa Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam, imegoma kumsaidia.


Kaisi ambaye amewahi kuwa mkuu wa wilaya na mikoa mbalimbali, amehangaika kwa muda wote huo katika ngazi nyingi, lakini ameshindwa kabisa kupata msaada wa kumwezesha kupata haki yake.


Kwa mujibu wa Mipango Miji, eneo hilo limeteuliwa na kutengwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya huduma za viwanda, na yeye amekuwa akilipia hati zote tangu alipomilikishwa eneo hilo .

Kova amtosa, ataka aende mahakamani

Hata Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Saalam, Suleiman Kova, amekataa kumsaidia kuwaondoa wavamizi hao.


Kaisi analithibitisha hilo kwa kusema, “Nilipoona sipati jibu kwa barua yangu ya Januari 10, 2012 nilikwenda kuonana na DCP Kova. Alinielekeza kwamba siyo kazi ya polisi kuondoa wavamizi na akanitaka nionane na DC (Mkuu wa Wilaya ya Ilala) ili nipewe barua kwenda mahakamani kupata ‘Court Order’.


“Nilipokwenda kwa wanasheria kutaka ufafanuzi zaidi, walishangaa kwa wasimamizi wa sheria na kanuni wamenieleza hivyo; kutokana na kwamba wavamizi wa eneo langu wameachiwa kuharibu mali yangu halali kisheria, pamoja na kwamba wametenda kosa jingine kufuatana na Penal Code: Under Section 299, Sub-section (a) and (b) ambayo inazungumzia ‘Criminal Trespass’.”

Mwanzo wa matatizo yote

Uchunguzi unaonyesha kuwa Novemba 24, 2011 alimwandikia barua aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni , Jordan Rugimbana; Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile; (kwa wakati huo)  na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime; akiwaeleza juu ya uvamizi huo, lakini kote huko hakusaidiwa.


Katika barua hiyo, Kaisi alisema, “Kwa heshima nakuja mbele yenu kuomba msaada wa kuwaondoa, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria kundi la wavamizi ambao Oktoba 19, 2011, majira ya saa tatu usiku walivamia na kuingia eneo langu ninalomiliki kisheria, ambalo lipo Pugu Mwakanga, Mtaa wa Kigogo Fresh, Kata ya Pugu.


“Baada ya kutokea uvamizi, msimamizi wa eneo hilo , Omari Nyangala, alitoa taarifa kwenye uongozi wa Serikali ya Mtaa, Kigogo Fresh. Viongozi hao walichukua jukumu la kuwaita wawakilishi wa wavamizi na kuwaeleza kuwa eneo linamilikiwa na mimi kisheria, pamoja na kuwaonya kwamba Serikali ya Mtaa haiwatambui na inawataka waondoke katika eneo hilo; wao waliwajibu viongozi wa Serikali ya Mtaa kwamba, ‘sisi siyo wavamizi ila tumekuja kuishi baada ya kukuta kuna shamba pori, mwenyewe ameshindwa kuliendeleza kwa muda mrefu kwa mujibu wa wenyeji walivyosema. Tulikuwa hatuna mahali pa kukaa, tumeamua tuishi hapo…Tupo watu 240 na tutaendelea kuwepo, iwapo kuna mtu amejitokeza anasema pake atupeleke mahakamani ili tukasikilizwe maelezo yetu’.”


Imeelezwa kuwa baada ya mahojiano na wavamizi, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa aliyetajwa kwa jina moja la Maguno alipeleka taarifa kwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Sitakishari, akiomba msaada wa kuwaondoa wavamizi.


Kituo cha Polisi Sitakishari kilifungua jalada STU/RB/16093/2011/KUINGIA/JINAI. Novemba 19, 2011 Mkuu wa Kituo (OCD) hicho, Jumanne Muliro alifika eneo la tukio na kuwakuta baadhi ya wavamizi wakiendelea na ujenzi.


“OCD aliwafahamisha kwamba eneo walilovamia lilikuwa na mmiliki halali kisheria na kuwaelekeza kwamba iwapo walihitaji eneo la kujenga na kuishi inabidi wapeleke maombi yao kwa viongozi wa Serikali ya Mtaa.


“Pamoja na ushauri wa OCD, wavamizi bado wapo wanakalia eneo langu na kuendelea kuleta uharibifu mkubwa…tayari wameshateketeza mali zangu nyingi na kupora vitu mbalimbali pamoja na kuvuruga mazingira,” amesema Kaisi katika barua yake kwenda kwa Rugimbana.


Kaisi, anawaomba viongozi wanaohusika katika utatuzi wa mgogoro huo kwa kusema, “Ninawasihi viongozi wangu mchukue hatua zipasazo za haraka za kushughulikia wavamizi hawa na kulikomboa eneo langu.


Kitendo chao ni cha jinai, kinavunja sheria na Katiba ya Tanzania …binafsi nilionalo baya zaidi, ni kule kuwepo katika jamii yetu makundi ya wahalifu ambao wamejiandaa kufanya na kuendeleza vitendo vya kijinai with utter impunity na wakati huo huo wakitishia amani miongoni mwa jamii.

Kwa upande mwingine, inaashiria kuwa kikundi cha watu 240 kilichovamia eneo langu ni mojawapo tu ya vikundi vingine ‘crime active and operating’ katika Wilaya ya Ilala na Jiji kwa jumla.”


Hata hivyo, ana maswali mengine anayojiuliza: Je, hivi viko vingapi? Pamoja na uvamizi wa ardhi, vinaendeleza uhalifu gani mwingine? Viongozi wa vikundi hivi ni nani? Je, upo uwezekano kwamba vikundi hivi vya wahalifu vinashirikiana na baadhi ya viongozi wa Serikali za Mitaa, watendaji wa Kata, na makatibu tarafa? Kwanini wanavikundi wajigambe na kujieleza kuwa wao ni Wakurya? Ni kweli kwamba makao makuu ya vikundi hivi ni maeneo ya Kitunda na Mombasa-Ukonga?


Kaisi anahitimisha kwa kutoa ombi, “Viongozi wangu, nikiwa raia mwema, nina imani na mfumo wetu wa kulinda watu na mali zao, pamoja na kudumisha amani katika nchi yetu kwa kuzingatia na kuheshimu sheria; yaani kuwepo kwa utawala wa sheria. Kwa hiyo, ninaendelea kuwasihi kunipa msaada wa kushughulikia ipasavyo wavamizi wa eneo langu, pamoja na kuwaondoa, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria.”

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam azungumza

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck, amezungumza na JAMHURI na kusema hana taarifa za uvamizi wa shamba la Kanali Kaisi.


“Kwa kweli sina habari, bahati mbaya kwa sasa nipo Mwanza, wasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala inawezekana yeye akawa na uelewa wa suala hilo.


“Kila kitu kinakwenda kwa utaratibu na sheria, tutaangalia namna alivyovamiwa na tutafikia mwafaka.


“Nakumbuka tuliagiza operesheni ifanyike katika wilaya zote za Dar es Salaam kuondoa waliovamia ardhi ili irejeshwe kwa wamiliki halali, Nadhani suala la Mheshimiwa Kaisi litakuwa kati ya hayo, wiki ijayo (wiki hii) nitakuwa ofisini, nakuhakikishia kuwa haki itatendeka,” amesema Meck.

Kauli ya DC wa Ilala

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, ameiambia JAMHURI kuwa ana taarifa zote zinazohusu uvamizi wa mashamba na viwanja vya wananchi katika maeneo mengi ya Wilaya ya Ilala, yakiwamo ya Pugu, Chanika na Msongola.


“Juhudi zinaendelea kufanywa kukabiliana na hali hii, najua kabisa uvamizi upo, lakini kusema ukweli sikujua kama Mzee Kaisi naye yupo kwenye matatizo haya.


“Inawezekana kweli akawa na tatizo hilo kwa sababu kuna wakati alimtumia mtu mmoja kuweka miadi ya kuonana na mimi. Nikawapa siku na muda wa kuonana naye, lakini sikumwona,” amesema.


Amesema kama mtu anamiliki ardhi, na akatokea mtu akaingia kwa jinai, ni wajibu wa polisi kumwondoa mvamizi au wavamizi.


“ Kama ni civil matter inabidi iingie mahakamani, Mahakama itoe order. Sisi Serikali, polisi ni wajibu wetu kusimamia kumtoa huyo mvamizi.


Kama ni sura ya criminal, yule aliyeingia kwa jinai akamatwa, anafunguliwa kesi mahakamani. Kwa wasio na hati kuna mlolongo mrefu kwa sababu inabidi Mahakama isikilize na kutoa uamuzi; kama Mzee Kaisi ana hati hilo ni suala la kuwaondoa wavamizi tu,” amesema.


Hata hivyo, Mushi ametoa rai kwa vyombo vya habari kuhakikisha vinawaelimisha wananchi ili wasiwe kikwazo wakati wa kuwaondoa wavamizi.


“Watu wanavamia maeneo ya watu wengine kwa makusudi, tukitumia nguvu kuwaondoa utasikia mara ooh haki za binadamu zinavunjwa, polisi wanatumia nguvu…Haiwezekani kukawa na watu ambao kazi yao ni kuvamia tu, na pale wanapoondolewa ndipo ionekane haki za binadamu zinavunjwa.


“Vyombo vya habari vitusaidie kukabiliana na wahalifu hawa, amesema Mushi.”