Ndoa inapokuwa imefungwa kisheria, kuna haki za msingi ambazo huandamana na mkataba huo. Moja ya haki maarufu ni ile ya mume kumtunza mkewe. Tutaangalia kinyume cha haki hii kuona kama mke naye ana wajibu wa kumtunza mumewe. Lakini kabla ya hilo tutazame haya:

1. Baadhi ya haki zinazoibuliwa na ndoa

(a) Haki ya tendo la ndoa. Hii ni haki ya lazima kwa wanandoa na kutokuwapo kwake kunaweza kubatilisha ndoa iwapo mmoja wa wanandoa ataamua kushitaki kudai haki hiyo. Ni haki ambayo huchukuliwa kama ndiyo ndoa yenyewe, hivyo kuifanya kuwa na umuhimu wa pekee.

(b) Haki ya kutumia jina la mume. Hii ni haki aliyonayo mwanamke ambapo anaruhusiwa kutumia jina la mume wake badala ya lile la baba yake. Hata hivyo, sheria haikueleza iwapo mwanamume naye anaweza kutumia jina la mke wake, au la baba wa mke wake, au la ukoo wa mke wake.  

Pia, si tu mwanamke ameruhusiwa kutumia jina la mume wake, isipokuwa hata lile la ukoo wa mume wake.

(c) Haki ya kutumia mali za familia kwa pamoja. Haijalishi mali hizo ni za nani kati ya wenza hao. Ikiwa ni za mwanamke, basi mwanamume atakuwa na haki ya kuzitumia, halikadhalika zikiwa ni za mwanamume, mwanamke naye atakuwa na haki nazo.
Lakini matumizi ya mali hizo ni lazima yasikiuke sheria.

(d) Haki ya kutunza watoto/mtoto. Ikiwa familia imebarikiwa kuwa na mtoto/watoto basi wanandoa kwa pamoja wanawajibika kuwatunza watoto hao kila mtu kwa nafasi yake. Hii ina maana mwanamke anawajibika zaidi kuwa mwangalizi mkuu wa kila siku wa watoto, huku mwanamume akilazimika kutoa matumizi hasa yale ya kifedha ili kukidhi mahitaji ya mtoto/watoto.

(e) Haki ya kugawana mali pindi ndoa inapovunjika. Hii uhusisha mali zote ambazo wanandoa watakuwa wamezichuma pamoja wakati wakiishi kama mume na mke.
(f) Pia ipo haki ya kurithi na kurithiana mali iwapo mmoja wa wanandoa atafariki dunia. Mwanamke aweza kurithi mali za mume wake, halikadhalika mwanamume naye anaweza kurithi mali za mke wake. Hii huenda mpaka kwa watoto waliopatikana katika ndoa ambapo nao wana haki ya kurithi mali za wazazi wao.
(g) Haki ya matunzo baina ya wanandoa.  Hii ndiyo itakayojadiliwa japo kwa ufupi.

2. Mwanamume kumtunza mwanamke

Sura ya 29 ya Sheria ya Ndoa, Kifungu cha 63(a) kinasema kuwa ni wajibu wa kila mwanamume kumtumza mke/wake zake kutokana na njia za kipato chake. Neno njia za kipato chake maana yake ni namna anavyopata kipato ndivyo atavyotakiwa kutoa matunzo kwa mwanamke.  

Haiwi kwamba mwanamume anapata kipato kidogo halafu alazimishwe kutoa matunzo makubwa. Ushahidi wa namna anavyopata kipato chake ndio utakaoainisha kiasi cha matunzo kwa mke wake.

Aidha, kwa mujibu wa kifungu hicho, matunzo yanayoongelewa hapa yanahusisha makazi, mavazi, chakula na huduma nyingine kama za afya n.k. Kitu cha msingi hapa ni kuwa, ni lazima kwa mwanamume kutoa vitu hivi kwa mke wake.

3. Mwanamke kumtunza mwanamume

Kifungu hicho hicho cha 63(b) kinasema kuwa utakuwa ni wajibu wa kila mwanamke, lakini mwenye uwezo, kutoa matunzo kwa  mume wake iwapo mume huyo ana ulemavu/hajiwezi jumla au sehemu ya mwili wake, kiakili au kimwili, hivyo kutokuwa na uwezo wa kuingiza kipato kutokana na hali hiyo.

Kwa kifungu hiki tunaona kuwa mwanamke anao wajibu wa kumtunza mume wake lakini iwapo tu kwanza ana uwezo, pili mwanamume awe na tatizo ambalo kwalo hawezi kuingiza kipato na tatizo hilo liwe la kimwili au kiakili.
Kumbe basi, tunaona kuwa mwanamume kumhudumia mwanamke ni lazima hata mwanamke awe mzima wa afya, huku hafanyi kazi, wakati mwanamke kumhudumia mwanamume ni pale tu atapokuwa ana tatizo ambalo linamfanya asiweze kufanya kazi. Lakini pia sheria imesema mwanamke atatoa huduma iwapo ana uwezo wakati neno iwapo ana uwezo haikuliweka kwa mwanamume. Kwa mwanamume kutoa ni kutoa tu.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.  

By Jamhuri