Sheria ni kama silaha, itumike kwa uangalifu

Katika sifa nyingi zinazohitajika kuwa polisi, sifa moja ambayo haitajwi ni imani ya polisi kuwa kila binadamu ana uwezo wa kuvunja sheria na iwapo bado hajavunja sheria kuna siku atafanya hivyo. Ni sifa inayofanya polisi kuamini kuwa kila raia anayekutana naye anaficha uhalifu ambao polisi anapaswa kuufichua.

Ni sifa ambayo inasaidia kudhibiti uhalifu na uvunjifu wa sheria, lakini ni sifa ambayo inawasumbua wengi ambao hawajavunja sheria.

Kuna dalili kuwa utendaji kazi wa aina hii ambao kwa kiasi fulani unaleta mafanikio katika kudhibiti uhalifu unaanza kuonekana wa kawaida kwenye mamlaka nyingine za serikali.

Malalamiko dhidi ya mamlaka hizi yangetoka nje ya serikali pekee yasingebeba uzito sana. Lakini imefika hatua sasa kwamba baadhi ya malalamiko ya kinachoonekana kama uhusiano usio na tija kati ya baadhi ya idara hizi na wadau mbalimbali zinatoka pia kwenye taasisi za serikali.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe, amelalamikia utaratibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kufunga biashara ambazo zinadaiwa kodi badala ya kutafuta suluhisho muafaka ambalo litairuhusu hiyo biashara kuendeleza shughuli zake pamoja na kulipa kodi.

Aliyoyalalamikia mkurugenzi huyu ni mfano tu wa malalamiko ya aina hii dhidi ya maafisa ambao wana haraka ya kukimbilia uamuzi ambao unaleta hasara zaidi ya manufaa.

Kufunga biashara ni moja ya hatua tu ambazo zinaweza kuchukuliwa dhidi ya mkwepa kodi. Lakini bila shaka sheria inaruhusu mkwepa kodi kupewa muda wa kulipa deni la kodi inayodaiwa na akaendelea na biashara yake na wakati huo huo akitunisha makusanyo ya kodi kwa serikali.

Tunakumbushwa kuwa sheria ni msumeno na anayeivunja anapaswa kutumikia adhabu. Lakini ipo sababu ya msingi kabisa ya kutumika busara kwa makosa madogo ambayo yanaweza kuepukika iwapo aliyefanya kosa ataelimishwa au ataelemishwa pamoja na kutakiwa achukue hatua za kurekebisha kosa alilofanya.

Katika suala hili la TRA busara inafungua fursa ya kuelimishana na matokeo yake ni kulinda ajira na kuongeza mapato ya serikali. Kwamba athari hii ya kutoa adhabu haiko dhahiri sana ni tatizo la kukosekana kwa uratibu wa karibu kati ya idara za serikali kukumbushana, kila mara, kuwa ufanisi wa kutimiza malengo ya serikali kwenye eneo moja unahitaji kuwepo kwa mazingira yasiyokinzana kwenye eneo lingine.

Hii mifano ya idara au taasisi moja ya serikali kulalamikia taasisi nyingine ni ishara kuwa kila idara au taasisi inajifungia ofisini na kujipangia malengo yake bila kufanya tathmini ya athari ya uamuzi wake juu ya ufanisi wa taasisi nyingine.

Ofisa wa Idara ya Uhamiaji ambaye kila anapoona mgeni atamsimamisha na kudai vibali vya uhalali wake wa kuishi nchini anaweza kuwa anatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, lakini kitendo kama hiki kikianza kuonekana kuwa ni usumbufu kwa wageni ambao vibali vyao havina hitilafu, na hasa kama ni watalii, basi upo uwezekano mkubwa kuwa watalii wataamua kuwa Tanzania si nchi inayopenda watalii na watatafuta nchi nyingine za kutembelea.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, amenukuliwa akisema kuwa sekta ya utalii imechangia Sh trilioni 4.7 kwenye pato la taifa mwaka 2016. Ni sekta ambayo inaleta manufaa makubwa kwa uchumi ikiwa ni pamoja na kuchangia mapato, kodi ya serikali, na ajira. Watalii wanaongeza mahitaji ya vyakula, vinywaji, uvuvi, uwindaji, na kukuza biashara ya jumla na ya rejareja.

Labda si rahisi kupata ushahidi wa kitafiti kufahamu athari za kusumbua watalii 1,000 na 100 tu kati yao ndiyo wakutwe na makosa ya kuwa nchini bila vibali. Tunaweza kubaki kukisia kama wale 900 waliobaki watavumilia usumbufu walioupata na kama wataamua kurudi tena kutembelea Tanzania.

Na hatutarajii kuwa haya ni maswali anayojiuliza ofisa uhamiaji ambaye kwake la msingi ni kutekeleza sheria ambayo kuna ofisa mwenzake alishaitekeleza alipomruhusu mgeni kuingia nchini kwa mara ya kwanza. Lakini ni maswali ambayo yatamsumbua mdau wa sekta ya utalii ambaye shughuli zake zinalindwa na kuwapo kwa mazingira rafiki kwa watalii, badala ya mazingira yanayomgeuza kila mgeni kuwa mshukiwa wa uhalifu.

Kusudio siyo kupinga kutekelezwa kwa sheria zilizopo, iwe za kodi, za uhamiaji au sheria nyingine ambazo zimekiukwa. Badala yake ni jitihada ya kushauri iwepo subira na busara, sheria inaporuhusu, kuelimisha na kutoa fursa ya kurekebisha makosa, badala ya kukimbilia kuadhibu. Serikali inategemea sana wadau kutekeleza majukumu yake. Mafanikio yanahitaji ushirikiano wa karibu na uimarishwaji wa uhusiano kati ya pande zote.

Turudi tena kujifunza kutoka kwa polisi. Sheria ni kama silaha, lakini silaha haitumiwi kila mara.

Maoni: [email protected]