Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwenye kilele cha Sherehe za Mei Mosi, 1995 mjini Mbeya. Kwenye sehemu iliyopita, Mwalimu alisema mtu yeyote mwenye akili akikupa mawazo ya kipumbavu na wewe una akili na unajua ni ya kipumbavu na ukayakubali, atakudharau. Alielezea hisia zake juu ya uuzwaji holela wa viwanda na mashirika yaliyokuwa yakijiendesha kwa faida. Endelea…

 

…alimu Benki ya Dunia”. Benki ya Dunia hawa nani? Mungu gani mpya huyu anaitwa Benki ya Dunia? Vile vile wanasema, “Mwalimu, tumebanwa na Shirika la Fedha la Kimataifa”. Hawa ndiyo nani? Hawa nimeanza kuwasema mwaka 1980 nikasema “tangu lini Shirika la Fedha la Kimataifa limegeuzwa kuwa Wizara ya Fedha ya Kimataifa?”

 

Swali hili nililiuliza mwaka 1980 wakati nilikuwa nadhani nitaacha uongozi wa nchi yetu. Kwa nini, kama kweli sisi watu wazima na akili zetu, tunakubali mambo ya kipumbavu tunasema, ‘tuuze mashirika yetu’. Tulianza na mashirika ambayo hayana faida tukasema; “uzeni hili halina maana”.

 

Lakini, taratibu tukasema, ‘mashirika yenye faida sasa uzeni’ na tunaanza kuyauza. Hata hivyo, tunauliza “haya tunayauza kwa misingi gani maana hata chama chetu kinasema tusiyauze” wanajibu, “ah! Mwalimu, tumebanwa na Shirika la Fedha la Kimataifa”. Mungu mpya nani huyu? Hivi ni kweli hatuwezi kukataa sasa? Kwa nini nasema hivi ni kwa sababu tayari tunayo matatizo mengi katika uchumi, afya na huduma za umma zote. Mambo yanakwenda ovyo. Ukiuliza kwa nini, wanajibu “Shirika la Fedha la Kimataifa mzee”. Ni kitu gani hicho?

 

Serikali haihimizi ulipaji kodi

Wamewahi kunijia vijana wetu wamiliki wa viwanda hapa nchini wakati bado ningali Mwenyekiti wa CCM wakaniambia: “Mwalimu, wafanya biashara hawa si wafanyabiashara ni walanguzi”. Vile vile, wafanyabiashara wenye viwanda vyao walinifuata pale Msasani, wakati ningali Mwenyekiti wa CCM, wakaniambia: Mwalimu, tunaomba Serikali ikusanye kodi, hilo tu.

 

Hatuombi Serikali itulinde. Isilinde viwanda vyetu kwa namna nyingine yoyote isipokuwa ikusanye kodi, basi. Kama ikikusanya kodi, basi nguo zinazoingia kutoka nchi jirani, zisiingie bila kulipa kodi. Zilipe kodi, hatuombi zaidi ya hapo. Zikilipa kodi, basi tutashindana. Zisipolipa kodi, bidhaa tunazoziona zote hizi hazilipi kodi. Hatuwezi kushindana hata kidogo. Tutakufa.

 

Wakubwa hawa hatuwawezi. Wataleta vitu hapa, kwanza ni rahisi zaidi kuliko vyetu. Pili, visilipe kodi forodhani, viingie nchini hivi hivi! Viwanda vyetu vitakufa! Sasa nasema, angalao Serikali ichukue kodi na kodi ipo, na wala sisemi waongeze kodi kwani vipimo vile vya kodi vipo. Tunachoomba Serikali itoze tu.

 

Serikali, wananiambia, “Zaidi ya miaka mitatu tokea mwaka 1995 imepoteza shilingi sitini bilioni taslimu”. Nimeambiwa hilo zaidi ya mara tatu na wafanyabiashara. “Serikali inapoteza shilingi sitini bilioni kwa kutokusaya kodi”. Mara tatu! Kwa hiyo, safari hii niliposikia wakubwa wanasema mmepoteza sabini bilioni miaka mitatu au minne iliyopita, sikushangaa.

 

Hamkusanyi kodi kwa nini? Kwa kutokusanya kodi, mnaviua viwanda vyetu vya nyumbani hapa. Lakini, mnafanya madhambi mengine makubwa zaidi kuliko kuviua viwanda vyetu. Mnasemaje, maana kisingizio hiki cha kusema ni Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia hakipo tena kwani baadhi yao ndiyo wanaosema “kusanyeni kodi”.

 

Hivi kisingizio hiki cha kwamba kila jambo ni Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia ni cha kweli mpaka leo? Mbona wao tena ndiyo wanaowaambieni “Kusanyeni kodi, msipokusanya tunaweza tukafikiria kuchukua hatua kama mnadhani ni mambo ya utani hivi. Sasa kusanyeni kodi!”

 

Tunakwenda wapi? Viongozi tunaowataka

Naeleza baadhi ya matatizo ambayo viongozi tutakaowachagua tuwe na hakika iwapo wanayaona hivi kama sisi tunavyoyaona. Yanawauma kama sisi yanavyotuuma na kwamba, watakapofika hapo wanapopataka watusaidie kuyatatua. Wanayaona, yanawakera na hata watakapofika hapo, hicho ndicho kitakachowasukuma kutaka kuwa marais wetu na wabunge wetu.

 

Marekani walikuwa na rais wao kijana mmoja mdogo anaitwa John Kennedy. Walimpiga risasi. Marekani nao ni watu wa ajabu sana! Vijana walilaani tukio hilo kwa kuwa walikuwa wanadhani wamemchagua rais wa umri wa kama miaka arobaini na mitatu au minne hivi. Sasa huyo ni kijana, hata kwa hapa Tanzania leo ni kijana.

 

Alipochaguliwa na Marekani akawa Rais wao. Katika hotuba yake ya kwanza kabisa aliwaambia wananchi wenzake, hasa vijana “Usiulize Marekani itakufanyia nini, jiulize wewe utaifanyia nini Marekani?” Kila anayetaka kuwa mgombea wa urais/ubunge ajiulize ataifanyia nini nchi yake.

 

Tunataka mtu anayetaka kuwa rais wetu ajiulize anataka kuifanyia nini nchi yetu na siyo nchi yetu itamfanyia nini. Na tunataka swali hilo ajiulize kila mtu anayetaka kuwa mgombea wa chama chochote kuwa mbunge/rais: “Kwa nini, kwa dhati kabisa, anaumwa na umasikini wetu na umasikini huo ndiyo unaomsukuma ashughulike na mambo haya ya siasa katika ngazi hiyo ama ya ubunge ama ya urais”. Kama sivyo, hatufai!

 

Mtu hapakimbilii Ikulu: Hakuna Biashara Ikulu

Mtu anayetaka kwenda Ikulu kutaka faida yoyote Ikulu pale hatufai hata kidogo. Wananchi, mimi nimekaa pale Ikulu kwa muda mrefu zaidi kuliko mwingine yeyote, wala sidhani kuna mtu mwingine anaweza kuzidi muda huo. Tayari hapa tumeweka sheria. Kwa mujibu wa sheria, mtu hawezi tena kukaa Ikulu zaidi ya miaka kumi, kipindi ambacho hata hakijafikia nusu ya kipindi nilichokaa. Mimi nimekaa miaka ishirini na tatu!

 

Najua, kwa mtu halisi kabisa, Ikulu ni mzigo! Hupakimbiliwi! Si mahali pa kupakimbilia hata kidogo; huwezi kupakimbilia Ikulu. Unapakimbilia kwenda kutafuta nini? Ni mgogoro; ni mzigo mkubwa kabisa! Ukipita barabarani, unakuta watu wana njaa, unaona ni mzigo wako huo. Pazito pale! Huwezi kupakimbilia na watu safi hawapakimbilii. Ukiona mtu anapakimbilia, na hasa anapotumia tumia vipesa kwenda Ikulu, huyo ni mtu wa kuogopa kama ukoma!

 

Mtu yeyote anayeonekana anapenda sana kwenda Ikulu na hata yupo tayari kununua kura ili kumwezesha kufika Ikulu ni wa kumkwepa kama ukoma. Kwanza, hizo fedha kapata wapi. Mtanzania wa leo hawezi kununua watu bila kwanza yeye kununuliwa. Na kama kanunuliwa, atataka kuzilipaje? Kazipata wapi? Watanzania wote ni masikini tu. Mtanzania anaomba urais wetu kwa hela! Amezipata wapi?

 

Pili, kama hajanunuliwa, kazipata wapi? Kama kakopa, atarudishaje? Ikulu pana biashara gani mtu akope mamilioni halafu aende ayalipe kwa biashara ya Ikulu? Ikulu mimi nimekaa kwa muda wa miaka ishrini na mitatu. Ikulu ni mahali pazito. Kuna biashara gani Ikulu?

 

Rushwa na matumizi ya fedha bila utaratibu wakati wa uchaguzi

Sisi Waafrika ni watu wa ajabu sana. Unajua ni wadogo, lakini nasema, ni udogo wa mawazo. Umaskini wa mawazo ni umasikini mbaya kupita wote. Unaweza ukawa na almasi mfukoni, akaja tapeli na kijiwe kimetengenezwa kama almasi akakuambia “ebu tuone almasi yako. Bwana aa! Hii ya kwako siyo almasi ni chupa tu, almasi ni hii. Kwanza nipe bwana.” Mkabadilishana. Yeye akachukua almasi yako na akakuachia kichupa na ukatoka hapo unashangilia kama zuzu!

 

Sisi hapa Tanzania tulikuwa tumeanza utaratibu ambao ukitumia fedha nje ya fedha za chama na Serikali na ukatumia fedha zako mwenywe katika uchaguzi, tunakutoa. Hufai! Huo ndiyo ulikuwa utaratibu wetu. Tulikuwa tunakuuliza: “Hii nchi ya masikini, wewe mwenzetu una mali umeipata wapi?”

 

Mali, kwa wakati huo, kwetu sisi ilikuwa ni sifa ya kukunyang’anya uwezo wa kugombea uongozi Tanzania. Tulijua kwamba, kama una mali, utaficha. Leo watu wanasema waziwazi: “Mwalimu uchaguzi wa mwaka huu utapitishwaje?”

 

Marekani wanatumia fedha nyingi sana katika uchaguzi. Nyingi sana! Kama Marekani sasa hivi wanazungumza watunge sheria inayofanana na ile mliyoitupa ninyi mnadhani kwa sababu ni mawazo ya masikini, haina maana.

 

Wakubwa wanayafikiria mawazo hayo sasa hivi. Marekani wanafikiria uwezekano sasa wa kutunga sheria itakayoweka utaratibu wa fedha za ugombeaji kutokana na mfuko mmoja baada ya kugundua kwamba inapokuwa holela na kila mtu akiachiwa lwake, inavuruga. Inaleta rushwa kubwa kabisa. Unanunuliwa urais na unaweza kununuliwa na fedha za wauza bangi na wauza baa. Wauza bangi wanaiona hatari hiyo, ninyi haa!

 

Hapa tulikuwa na utaratibu mzuri kabisa tuliouanzisha mlioutupa, mnafikiri, sisi mwaka huu fedha tu! Uchaguzi wa fedha, mtazipata wapi? Mimi nimetoka juzi tu, mara mmetajirika kiasi hiki! Waswahili hee! Kumbe mnaweza kutajirika zaidi kwa haraka hivyo? Sasa kama mnao uwezo wa kutajirika, nawambieni ‘Fanya wote tutajirike. Hivi mtajirike peke yenu, tutajirike wote”. Wapi! Ni rahisi sana watu wachache kutajirika.

 

Tunataka Serikali inayotoza kodi

Kwa hiyo, naserna sasa hivi mimi sijali kabisa na wala msifikiri tena napinga watu wanaotaka uhuru wa kujipatia mali. Tunataka Serikali itakayotoza kodi. Tulikuwa na viserikali vya rafiki zetu za Skandinavia vinavyoongozwa na watu wanaojali maslahi ya umma. Vinatoza kodi matajiri, halafu mapato hayo yanasambazwa kwa faida ya wote. Hata hapa fanyeni hivyo. Lakini isiwe ni kukusanya kodi na halafu, kilicho chetu mnataka kukiuza. Hata hicho muuziane, halafu mpate pesa na hizo pesa zenu wala msilipe kodi! Hii ndiyo kazi tuliyowapeleka Ikulu?

 

Sifa za ziada za viongozi

Nilipokuwa Dar es Salaam, nilieleza mahala fulani kwamba watu wanaotaka kutuongoza wawe angalau na sifa hizi na hizi. Sasa nasema hata wakiwa nazo bado tutawauliza: “Sifa mnazo, lakini mnakwenda kufanya nini?”  Hata nikiwa na watano wenye sifa nzuri bado nitasema: “Ninyi watano mna sifa nzuri kabisa, mimi sioni kama mna kasoro lakini bado nitawauliza hasa mnakwenda kutafuta nini Ikulu. Uniambie kwa dhati ya moyo wako kinakuuma nini kwamba unaweza kweli ukaumwa kabisa”. Halafu ukasema: “Mwalimu, Ikulu sipapendi. Ikulu siyo tatizo. Kama mambo yanakwenda ovyo ovyo utaacha tu?

 

Zile sifa nilizozitamka hazitoshi: kwamba lazima uwe Mtanzania na unaheshimu Tanzania. Maana tunatafuta rais wa Tanzania na wala hatutafuti wasifu wa Rais wa Tanzania. Tuna miezi saba uwe umezipata zile tano na kuendelea. Hata hivyo, bado tutawauliza mambo ya uchumi, viwanda na shule unavyoyaelewa. Mambo ya afya, ninyi mnayajua yote. Hospitali zetu, hali yake ya sasa hivi mnaielewa inaendaje endaje na kama mnaelewa ninyi unaionaje? Unaona raha tu? Maana sisi ni watu wa sera ya kuchangia. Sawa. Lakini wewe umechangia mara ngapi? Hebu nenda katika hospitali moja uone watu wanavyochangia.

 

Tunataka kufikiria kwa msingi kwamba kitu kimoja tunachotaka kuelewa ni hali ya matatizo yetu yalivyo sasa. Hii ni kwa sababu Awamu ya Kwanza, awamu yangu mimi, imefanya mema na imefanya ya kijinga. Yale ya kijinga, mnayaacha. Lazima yanaachwa. Ubaya wenu ni kwamba mnayaacha mema na mnachukua ya kijinga.

 

Miaka ishirini na tatu, bwana, lazima tumefanya makosa. Pale, bwana, hatukuwa na wasomi wengi, ujuzi wala chochote. Tulikuwa tunahangaika tu. Kama watu hamjui kuogelea, mnatupwa kwenye maji, mnahangaika kuogelea, lazima mtafanya makosa. Tusifanye makosa kwani sisi ni malaika? Awamu ya Kwanza ina mambo fulani fulani na hasa ya msingi na mengine ya utekelezaji mazuri, mnaendelea nayo. Mengine ya utekelezaji ya ovyo ovyo, mnayaachilia mbali mnaanzia hapo tena.

 

Ila la ajabu ni kwamba hata ya msingi mnayawekea alama ya kuuliza. Mimi sikudhani kama ya msingi yalikuwa na matatizo, nilidhani mambo yetu ya utekelezaji yana matatizo mengi hivi ya kusikilizana, hata ya msingi. Sasa watu wataanza kugombana katika misingi ya ukabila, udini na mambo mengine ya kijinga kabisa.

 

Kwa hiyo, nasema, Awamu ya Pili mnaanza na mengine mnaongeza hapo. Awamu ya Pili nayo inafanya makosa yake, itafanya mema yake. Yale mema, ndiyo mnayoendelea nayo; mnaendelea na yale mema yake. Yale mabaya mnayaacha kama yalikuwapo ya msingi yamesahauliwa mnayarudia. Kutoyarudia yale ya msingi, mtapotea tu. Mnafanya hivyo halafu mnaendelea.

 

nataka kujua kama viongozi wetu wa sasa hivi wanaotaka kuingia katika Awamu ya Tatu ya uongozi wanayaelewa hivyo na tutaelewana hivyo au wanafikiri uongozi ni biashara tu! Je wanaotaka kutuongoza wanaweza, kwanza, kuelezea tulikuwa wapi, tuko wapi, tunataka kwenda wapi? Pili, je wanao uwezo wa kutupeleka kule tunakotaka kwenda? Tatu, watatushirikishaje kule ili na sisi tusaidiane kwenda huko? Hiyo ndiyo kazi iliyobaki. Pimeni Sana!

 

1302 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!