Tunapozungumzia siasa hatuwezi kudai kwa haki kwamba siasa ni kitu kibaya. Ungeweza kusema kwamba siasa ni maneno mazuri yanayomtoa nyoka pangoni. Kwa kifupi siasa inasaidia kutatua matatizo.

Chukua kwa mfano, tulijaribu kumfukuza mkoloni kwa kutumia mapambano ya silaha. Tukashindwa. Lakini mkoloni aliondoka pale tulipoamua kutumia mapambano ya siasa.

 

Ukweli ni kwamba nchi nyingi za Afrika zilipata Uhuru kwa kutumia vyama vya siasa ukiweka kando nchi 12 zilizoupata kwa mapambano ya silaha zikitanguliwa na Algeria, iliyokuwa nchi ya kwanza barani Afrika kupata Uhuru kwa mapambano ya silaha mwaka 1962.

 

Kwa hivyo, siasa si kitu kibaya. Lakini leo Watanzania tunaitumia vibaya siasa kiasi kwamba imevuruga masuala muhimu katika Taifa letu. Siasa inachangia kwa kiasi kikubwa kuzamisha nchi yetu. Tumeweka mbele ubinafsi na siasa badala ya kuweka mbele maslahi ya Taifa letu.

 

Leo, kwa mfano, siasa imevuruga kwa kiasi kikubwa umoja wa Taifa letu. Limebaki vipande vipande! Na matunda ya kuvurugika kwa umoja wetu yamesababisha kuvurugika kwa sekta nyingine za maisha.

 

Katika chama tawala si siri tena, hakuna umoja. Tamaa ya kupata urais imevuruga umoja ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wanaotafuta urais kwa udi na uvumba wamejiundia vikundi vinavyohasimiana. Hili ni jambo la hatari kwa Taifa pale chama tawala kinapoishi kwa vikundi. Maana kusambaratika kwa chama tawala kunaweza kusababisha kusambaratika kwa Taifa.

 

Kwa mfano, sakata la kuteswa na kuumizwa kwa Absalom Kibanda, Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Limited. Tukio la kuumizwa kwa Kibanda tayari amehusishwa Benard Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

 

Imedaiwa kuwa Julai 16, 2012 katika kipindi kilichorushwa na kituo cha Televisheni cha ITV, Membe alisema, “Kuna watu 11 wakiwamo waandishi wawili wa habari, nitawatwanga kweupe.” Hakuna anayetaka kumtetea Membe, lakini lazima tujiulize maswali na tuyatafutie majibu kama watu wazima.

 

Je, kuanzia Julai 16 mwaka jana hadi alipoteswa Kibanda, hakuna Watanzania wengine walioumizwa wakiwamo waandishi wa habari? Kwa vyovyote wapo. Kwanini matukio hayo hakuhusishwa Membe?

 

Membe amehusishwa na tukio la kutekwa Kibanda wakati vyombo vya usalama vikipeleleza tukio hilo. Na upelelezi hufanyika kwa siri ili ushahidi usivurugwe. Kwanini watu wanaomtuhumu Membe kwa tukio hilo hawakutaka kushirikiana na vyombo vya usalama, badala yake wameamua kuropoka katika suala nyeti kama hilo?

 

Benard Membe alisema atawatwanga mahasimu wake kweupe, je, Kibanda alitwangwa kweupe?

 

Halafu ni kosa kumtuhumu Membe kwa sababu alisema atawachukulia hatua mahasimu wake. Kwanza asingeweza kukaa kimya, pili, hakumtaja Absalom Kibanda kwamba ni mmoja wa mahasimu wake hao. Juu ya yote, kusema si kutenda.

Miaka 2000 iliyopita Yesu Kristo aliletwa kwenye baraza la viongozi wa dini ya Kiyahudi lililoitwa Sanhedrin. Akatokea shahidi aliyesema, “Huyu Yesu alisema tulivunje hekelu na yeye angelijenga kwa siku tatu.”

 

Katika baraza lile lililokuwa na wajumbe 70 wakiongozwa na Kuhani Mkuu, watu wawili – Nikodemo na Yusuf Arimathaya – walikuwa upande wa Yesu. Wakauliza, “Je, mlilivunja hekalu akashindwa kulijenga kwa siku tatu?” Huo ukawa mwisho wa ushahidi wa uongo.

 

Ushahidi wa kumhusisha Membe na mateso aliyopata Kibanda ni wazi kwamba ni ushahidi wa uongo uliotolewa kwa sababu za kisiasa. Hakuna mtu mwenye ubinadamu anayefurahia mateso yaliyompata Kibanda. Watanzania inatupasa kuwa waangalifu.

 

Tusimwingize mwenzetu kwenye matatizo yasiyomhusu. La kwanza, kama tuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba Membe anahusika na kuumizwa kwa Kibanda, basi tushirikiane na vyombo vya usalama. La pili, ni jambo baya sana kumhusisha na matukio ya kigaidi mtu asiye na hatia.

 

Mwenye hatia hufurahi anapoona ukweli unapotoshwa. La tatu, kitendo kama hicho kinahatarisha maisha ya Membe. Ndugu na jamaa wa Kibanda hapana shaka wanamwangalia vibaya Membe.


Tumeruhusu siasa kuvuruga umoja wetu na amani yetu.

Mapema katika makala haya nimedokeza kwamba siasa imevuruga umoja ndani ya CCM. Lakini pia siasa imevuga umoja ndani ya Bunge. Ushabiki wa kisiasa umegeuza Bunge kuwa kikao cha vyama vya siasa, ambapo kila chama kinapigania maslahi yake kuliko maslahi ya Taifa.


Leo hoja nyeti na muhimu kwa Taifa hili zinatupwa nje kwa sababu tu zinaletwa na wabunge wa vyama vya upinzani. Angalia, kwa mfano, hoja ya Mbunge James Mbatia iliyotaka iundwe tume ya kuchunguza udhaifu wa elimu katika nchi yetu.

 

Hata mwananchi wa kawaida anajua kuwa kuna udhaifu mkubwa kwenye elimu. Lakini, kwa sababu tu waziri wa serikali ya CCM, Dk. Shukuru Kawambwa, hakutaka wizara kutambua kwamba ina madudu yasiyo na idadi, wabunge wengi wa CCM walimlinda badala ya kulinda elimu.

 

Hapana shaka Taifa hili litaendelea kuzama katika kila kitu kama tutaendelea kutanguliza siasa kwa sababu tu za kibinafsi.


1220 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!