Mwaka juzi mwanasiasa wa siku nyingi wa nchini Malaysia, Dk. Mahathir Mohamad, alishinda uchaguzi kwa kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Najib Razak.

Kilichotokea kinashangaza. Inakuwaje babu wa miaka 92 afanye kampeni kwa mafanikio na kuweza kumuengua waziri mkuu aliyekuwa madarakani? Na afanye hivyo baada ya kustaafu siasa kwa miaka 15, akijipatia sifa ya kuwa kiongozi wa nchi mzee kuliko wote duniani?

Sababu mbili zinafafanua maajabu haya ya kisiasa. Kwanza, ni historia yake Mohamad, na pili ni tatizo la mpinzani wake kuwapuuza wapiga kura.

Mchambuzi wa siasa alimtaja Dk. Mohamad kuwa “babu wa taifa” la Malaysia. Ni mwanachama wa awali kabisa wa chama cha siasa kilichoundwa mwaka 1947 kilichoongoza nchi yake tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 1963 mpaka alipokiangusha kwenye uchaguzi wa mwaka juzi baada ya kujiuzulu uanachama na kuanzisha chama kipya cha siasa. Kabla ya kuchaguliwa upya mwaka 2018 aliwahi kushika wadhifa wa waziri mkuu kati ya mwaka 1981 hadi 2003.

Katika kipindi chake cha mwanzo kama waziri mkuu, pamoja na kwamba wapo wanaomkosoa kwa kuingilia uhuru wa mahakama na kuwaandama wapinzani wake wa kisiasa, Mohamad anakumbukwa kama kiongozi mwenye visheni imara kwa nchi yake, mzalendo wa kweli, na ambaye amefanikisha kuwapo mikakati iliyoletea maendeleo makubwa ya viwanda na uchumi.

Pili, mpinzani wake hakuwa na majibu thabiti juu ya matatizo yaliyowakabili wapiga kura, kama vile kupanda kwa gharama za maisha, na kodi. Lakini, baya zaidi na ambalo naliona kama dharau kubwa kwa wapiga kura na sababu mojawapo iliyowafanya wapiga kura wa Malaysia kumchagua Dk. Mohamad ni tuhuma za ufisadi dhidi ya waziri mkuu.

Najib Razak alituhumiwa kuiba dola milioni 700 za Marekani kutoka kwenye shirika la umma na kuziweka kwenye akaunti yake binafsi. Ni kashfa hii iliyomrudisha Dk. Mohamad kwenye siasa, akianza kwa kumshutumu waziri mkuu na kumtaka ajiuzulu, na baadaye kuamua kupambana naye kwenye uchaguzi.

Kama Mohamad anaweza kulaumiwa kwa kuminya uhuru wa mahakama, basi Razak anaweza kushukiwa kuwa swahibu wa mahakama. Madai ya wizi dhidi yake yaliyofikishwa mahakamani hayakuweza kuthibitishwa pamoja na watu kushangazwa na utajiri mkubwa wa baadhi ya wanafamilia wake. Wakati huo huo mke wake alichunguzwa kwa kununua vito vya thamani ya dola milioni 30 za Marekani.

Nchini Marekani nako kumejitokeza sauti ambayo inafanana kidogo na ile iliyomrudisha Mohamad madarakani. Kuna msemo kwamba kuna mambo mengi ambayo hayatokei kwingine duniani ila hutokea nchini Marekani tu. Si yote mabaya, lakini mengine yanawashangaza wengi.

Lakini hata hao walioizoea Marekani ambayo ni mashuhuri kwa kama nchi inayoibua kila aina ya matukio walishangaa kidogo Donald Trump alipochaguliwa kuwa rais wake wa 45. Inasemekana hata Trump mwenyewe alipigwa butwaa kwa ushindi wake, ushindi ambao hakuutarajia.

Na bado upo uwezekano wa kushangaa zaidi. Kuna kundi dogo la watu sasa linajenga hoja kuwa inafaa kwa rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, arudi kugombea tena nafasi ya urais. Ana umri  wa miaka 93, rika la Dk. Mohamad, kwa hiyo siyo ajabu sana kuwa anafikiriwa kurudi tena kwenye ulingo wa siasa. Labda kitakachoshangaza ni yeye kukubali hilo wazo.

Mashabiki wake wa leo wanamsikiliza anapozungumza na wanaona kama anatoa mawaidha mazuri ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zinaiandama dunia, siyo tu Marekani. Wanaona, tofauti na ofisi aliyotumikia kama rais wa 39 wa Marekani, ofisi ambayo kwa hulka yake tu inakulazimu kubaki wakati wote kwenye hali ya ukinzani siyo tu na maadui zako, lakini hata na marafiki wa nchi yako, kuwa sasa ni mtu ambaye anahubiri umuhimu kwa binadamu wote kuishi pamoja kwa amani licha ya kuwapo tofauti miongoni mwetu.

Kwa Marekani sidhani kama ni wazo ambalo litapewa uzito mkubwa, lakini uwepo tu wa wazo miongoni mwa watu – hata hao wachache – kwamba rais mstaafu wa miaka 93 anafikiriwa kama mgombea muafaka – ni dalili ya kuwapo ombwe kwenye uongozi.

Kuzungumzia babu wa Malaysia kuchaguliwa kuwa waziri mkuu, na babu wa Plains, Marekani, kufikiriwa kuongoza tena Marekani ni matokeo ya uborongaji uliotukuka wa viongozi ambao wamepewa dhamana na wapiga kura wao.

Si ajabu kwamba uborongaji ukiwa mkubwa sana kiongozi yeyote – hata yule kama Jimmy Carter ambaye alionekana mdhaifu wakati wa uongozi wake – anaanza kuonekana ni bora kuliko aliyeko madarakani.

Labda somo ni kuwa mpigakura ana kumbukumbu nzuri sana ya ahadi zinazotolewa wakati wa kampeni. Ana kumbukumbu nzuri pia ya makosa ya uongozi yanayojitokeza baada ya uchaguzi. Ana kumbukumbu nzuri sana ya ugumu wa maisha magumu anayoishi na bila shaka anachukizwa sana na ubadhirifu, ufisadi, na ufujaji ambao unaendelezwa na baadhi ya viongozi anaowachagua.

Unapowadia uchaguzi kuna uwezekano mkubwa wa kukumbuka changamoto zinazomkabili sasa hivi na kuzifanyia uamuzi kuliko kukumbuka changamoto zilizomkabili mpigakura mwenzake miaka 20 au 30 iliyopita. Na ndiyo ikawa sababu kwa wale viongozi wa zamani kuonekana bora kuliko hawa wa sasa.

Hatujui lakini kwa vyovyote vile, bado inashangaza kiongozi anayekaribia miaka 100 kufanikiwa au kufikiriwa kuongoza nchi.

By Jamhuri