Maendeleo ya binadamu yamebaki kuwa mtihani mgumu unaosumbua vichwa vya wengi wanaoendesha Serikali, taasisi binafsi au kuajiriwa. Kila binadamu anafanya kazi kwa nia ya kujiletea maendeleo binafsi ili hatimaye maendeleo ya mtu mmoja mmoja yazae maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Wiki iliyopita niliandika juu ya ‘Amri 10 za kujihakikishia umaskini wa kudumu’. Nisema nimefarijika kwa kiwango kikubwa kutokana na mrejesho nilioupata kutoka kwa wasomaji wangu. Nimefarijika pia kuona kuwa mengi kati ya niliyoandika ndiyo matatizo yanayoikabili jamii yetu na ndiyo chimbuko la umaskini unaotukabili bila ukomo.

Si nia yangu kuzirudia zile amri 10 ila nieleze mbili ambazo karibu kila aliyenipigia simu alizizungumzia. Hizi ni amri ya kwanza ya mtu kama unataka kukaribisha umaskini uwe wa kwanza kulala usiku na wa mwisho kuamka asubuhi. Lakini nyingine iliyozungumziwa mno ni kutumia kiasi chote cha fedha unayopata bila bajeti na baada ya kuishiwa unaanza kuhesabu vidole na kukuna kichwa na kujiuliza eti fedha hizo umezitumiaje!


Haya ndiyo yaliyokuwa matatizo yetu ya msingi na chimbuko kubwa la umaskini. Tunaposema mtu mmoja mmoja kutimiza wajibu wake, matokeo yake yanakwenda mbali zaidi. Kwa mfano, mtumishi wa umma anayefika ofisini amechelewa na kuwa wa kwanza kutoka kazini, anaathiri uchumi wa nchi. Kazi anazokuwa amepangiwa kuzifanya hazifanyi kwa wakati na hivyo kuathiri wananchi wengine wanaotegemea huduma yake.


Kinachotokea baada ya hapo ni kwa mtumishi huyu wa umma kutafuta kila mbinu kuficha uzembe wake. Hasara iliyopatikana kutokana na kuchelewa kwake kufika kazini na kuondoka mapema inahamia kwa wananchi. Vivyo hivyo, kama ni mtumishi wa benki  kama alipaswa kuingia ofisini saa 1:30 asubuhi na anasimamia kitengo cha kuidhinisha mikopo, kuchelewa kwake kunachangia mteja kuchelewa kupata mkopo.

 

Unapochelewa kupata mkopo ina maana biashara uliyokusudia kufanya inachelewa pia na hatimaye unakuta unapata hasara. Hasara hiyo haiishii kwa mkopaji pekee bali inakwenda mbali zaidi na kugusa wote ambao wangeshiriki katika mradi husika na kupata malipo kwa njia ya mishahara na posho kutokana na kazi waliyofanya.


Mifano hii ukiihamishia kwenye ngazi ya Serikali ndipo utakapoona ukubwa wa tatizo. Wapo watu wanaodhani nafasi wanazozishikilia serikalini ni zao. Wanafanya watakalo –  iwe ni kuchelewesha haki za watu au kutumia vibaya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi maalumu. Kuweka wazi mapato na matumizi hawaoni kama ni jukumu lao kwa njia yoyote ile.


Umaskini tulionao au tabu tunazopata kama wananchi vinatokana na kutokuwa na taarifa za uhakika. Kwa mfano, ukijua kuwa hospitali ya mtu binafsi inatoa dawa feki, hutahangaika kwenda kupima malaria katika hospitali hiyo maana una uhakika kuwa hata wakikupa dawa zao feki hazitakuponya.


Ukiwa na taarifa kuwa mradi fulani ukiufanya utapata hasara, hakika huwezi kujiingiza katika mradi huo. Ukiwa na taarifa kuwa Serikali inazo nafasi za kupeleka Watanzania masomoni na nafasi hizo zitatolewa kwa uwazo na kwa vigezo vinavyofahamika, hakika kama huna sifa hutajisumbua kupoteza fedha kidogo ulizonazo kuomba nafasi hizo. Kama unazo sifa utaomba mara moja.


Sitanii, ukijua kwa uhakika kabisa kuwa kodi unayolipa inatumika vyema kujenga barabara, kusambaza maji, kulipia elimu na afya yako bila sehemu ya fedha hizo kupelekwa kwenye akaunti za nje kama Uswisi, kamwe hutokataa kulipa kodi. Utalipa kodi kwa furaha na kushiriki kazi za maendeleo bila kinyongo.

 

Kwa bahati mbaya, uwazi limekuwa tatizo katika dunia tuishiyo. Wasomi na wataalamu wameweka mikakati mbalimbali inayolenga kukuza uchumi wa taifa na hatimaye mtu mmoja mmoja, ila mikakati hii imeshindwa kufanikiwa kutokana na kitu kinachoitwa usiri.


Leo wewe msomaji unayesoma makala haya, hivi nikikuuliza na sitanii, nini maana ya MKU, MKUZA, MKURABITA, MKUKUTA na misamiati mingine inayofanana na hiyo, nataraji si wengi watakaojibu swali langu kwa usahihi. Kwa sasa tunayo santuri ya Kilimo Kwanza lakini uliza wangapi wanajua Kilimo Kwanza ni nini? Bajeti iliyotengwa ni kiasi gani na inaishia wapi? Utastaajabu!


Kwa mfano, Mkoa wa Kagera katika eneo la Kilimo Kwanza mwaka juzi ulitengewa Sh bilioni 10, lakini waliishia kupata Sh bilioni 3.5 tu. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amelalamika wazi kuwa bajeti aliyotengewa katika wizara yake kwa mwaka wa fedha uliopita alipata asilimia 44 tu.


Mkoa wa Kagera na Membe ni tone la mifano katika bahari. Bajeti ya Serikali tunaambiwa ni Sh trilioni 15, lakini uhalisia fedha zinazokusanywa na kutumika Mungu tu ndiye anayezifahamu. Tunatangaziwa bajeti hewa na unakuwapo utekelezaji hewa. Ndiyo maana kila mwaka tunatangaziwa bajeti ya kukarabati barabara, mifumo ya maji, afya na elimu lakini hakuna kinachotekelezwa.


Sitanii nduu zanguni, kwa kuliona hili wataalamu waliokutana katika jijini  Sofia, Bulgaria, Septemba 28, 2002 walifikia uamuzi wa kuanzisha Siku ya Haki ya Kujua (Right to Know Day). Siku hii inalenga kuwapa wananchi fursa ya kudai taarifa sahihi kutoka serikalini.  Ni taarifa sahihi peke yake ndizo zitakazoweza kuwapa wananchi fursa ya kujiletea maendeleo.


Kati ya mambo yaliyoainishwa katika miaka 10 iliyopita kuwa ni nguzo ya maendeleo kwa taifa na mtu mmoja mmoja, ni kila mwananchi kupata taarifa sahihi kutoka serikalini na mamlaka mbalimbali kwa wakati, utawala wa sheria, kuzuia usiri serikalini na katika vyombo vyote vya umma. Kwamba taarifa zikiombwa na yeyote zitolewe kirahisi, haraka na bure.


Mambo mengine yaliyopendekezwa na wakubwa hawa ni maafisa wenye dhamana kuwajibika kusaidia watu wanaoomba taarifa kuzipata bila vikwazo. Wanasema kukatalia habari iwe mwiko na ikitokea basi ziwepo sababu za msingi zinazokubalika kwa kila upande. Kanuni ya maslahi ya jamii kwanza inapaswa kutawala katika utoaji wa taarifa.

 

Mashirika ya umma na taasisi kwa ujumla vinapaswa kuwajibika kuchapisha taarifa za mapato na matumizi yake mara kwa mara na kwamba kiwepo chombo cha kusimamia haki hii. Pendekezo hili linaungwa mkono na Rais Barack Obama wa Marekani linasema yeyote anapokataliwa habari awe na fursa ya kukata rufaa. Ni kwa msimamo huo mwaka 2010 Rais Obama alianzisha mpango wa Serikali ya Uwazi wakati nchi zaidi ya 48 ikiwamo Tanzania sasa zimekwishautia saini.


Kwa wanaokumbuka Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Mathias Chikawe, wakati akiwasilisha  bajeti ya wizara yake bungeni mwaka huu, alisema watatunga sheria ya Uhuru wa Habari na akasema sheria hii haitakuwa kwa ajili ya magazeti pekee, bali kwa ajili ya wananchi wote.


Sitanii, hili ndilo lililokuwa likipiganiwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) tangu mwaka 2002. Wakati wataalamu hawa wakikaa na kuona umuhimu wa Serikali yenye uwazi kwa maana ya kutoa taarifa sahihi kwa wananchi mara nyingi kadri inavyowezekana, kwa hapa nchini MCT nao walianzisha mchakato wa sheria ya Haki ya Kupata Habari.


Mwaka 2006 Serikali ilitaka kutunga iliyoiita Sheria ya Uhuru wa Habari, lakini uhalisia ulikuwa muswada wa kunyonga habari. Wanahabari waliukataa muswada huu na kupendekeza sheria hii itengwe katika sheria mbili; Haki ya Kupata Habari na Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari.


Septemba 28 mwaka huu Tanzania inaadhimisha siku hii ya Haki ya Kupata Habari katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. Siku hii inalenga kumpa mwananchi fursa ya kujua mambo yanavyoendeshwa serikalini na katika sekta binafsi.


Ni fursa kwa Mamlaka kama ya Vitambulisho, Vizazi na Vifo, benki mbalimbali, Hospitali, taasisi za utafiti, shule na vyuo, kampuni za ujenzi na nyinginezo kushiriki maadhimisho haya na kuwafahamisha Watanzania wenzao wako wapi na wafanya nini.

 

Siku hii pia itumiwe kama changamoto kwa Serikali kukubali kufikisha bungeni Sheria ya Haki ya Kupata Habari na Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari itakayosimamia waandishi wa habari pekee. Kama nchi kadri tutakavyotoa habari kwa wingi ndivyo kasi ya maendeleo ya nchi yetu na mtu mmoja mmoja vitakavyoongezeka. Usiri utatumaliza. Tuukatae.

 

 

 


 

 

 

 

 

 

By Jamhuri