Wakati wowote kuanzia sasa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) aliyesimamishwa kazi mwaka mmoja uliopita, Charles Ekelege atapandishwa kizimbani kujibu tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.

Taarifa za uhakika zilizolifikia JAMHURI kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zinasema uchunguzi dhidi ya Ekelege unaelekea ukingoni .

 

“Tuhuma za msingi ni za ukaguzi wa magari. Wabunge walikwenda Hong Kong waliyoyashuhudia ni aibu tupu, lakini mbaya zaidi amejipatia mamlaka ya kusamehe madeni wadeni wa TBS jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” kilisema chanzo chetu kutoka TAKUKURU.

 

Taarifa zinaonesha kuwa Ekelege alitumia kampuni hewa tatu, ambazo ni Jaffer Ali Mohamed ya Dubai, Quality Motors Limited ya Hong Kong na Planet Automotive Pty iliyodaiwa kuwapo Singapore.

 

“Mambo mengine ni aibu,” kiliongeza chanzo chetu. “Kampuni hizi zilikuwa hazina hata mtambo mmoja wa kukagua ubora wa magari, lakini Ekelege akawa anasisitiza kuwa zinafanya kazi kwa ufanisi, hadi wabunge walipobaini ujanja huo.”

 

Mbaya zaidi, uchunguzi ulionesha kuwa kampuni hizo tatu zinazomtia matatani Ekelege nyaraka za usajili zinaonesha kuwa zinamilikiwa na mtu mmoja, ajulikanaye kwa jina la Said Abood.

 

Chini ya mkataba unaodaiwa kuingiwa kati ya kampuni hizi na TBS, kampuni zilipaswa kuwasilisha asilimia 25 ya mapato yatokanayo na ukaguzi wa kila gari, lakini hadi Ekelege anasimamishwa kazi wakubwa hawa walikuwa hawajalipa.

 

Ukiacha kutokagua magari na kutotoa hiyo asilimia 25 iliyokubaliwa, kuna nyaraka zilizokusanywa na maafisa uchunguzi zinazoonesha kuwa Ekelege alikuwa anazisamehe kampuni hizo  asilimia 25 baada ya kuandika barua kwake na kusema hazina uwezo wa kulipa kiasi hicho.

 

“Mamlaka ya kusamehe deni kwa TBS ni ya Bodi na si ya Mkurugenzi Mkuu. Ekelege alijipa madaraka makubwa ajabu. Ukiacha hiyo, barua zenyewe ukizisoma za kuomba kusamehewa deni lugha iliyotumika inafanana kwa kiasi kikubwa kwa kiwango cha kutia mashaka kuwa mwandishi wa barua hizo ni mtu mmoja,” chanzo kingine kililifahamisha JAMHURI.

 

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa Ekelege alisamehe hadi dola 45,000 karibu Sh milioni 70 na hadi sasa kampuni hizo zinadaiwa karibu dola 50,000 karibu Sh milioni 80.

 

Uchunguzi wa JAMHURI umeonesha kuwa Ekelege aliyesimamishwa kazi Mei 20, 2012 ikiwa umetimia mwaka mmoja, bado anaendelea kupata mshahara na mafao mengine ambayo ni wastani wa Sh milioni tano kwa mwezi.

 

Juhudi za kumpata Ekelege kueleza alivyojipaga kukabiliana na tuhuma hizo hazikuzaa matunda kwani mwandishi alipokwenda hata nyumbani kwake Dar es Salaam aliambiwa amesafiri nje ya nchi, ukiacha simu yake ya mkononi kutopatikana.

 

By Jamhuri