Msatahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, amesema anamshukuru Mungu, Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), kwa kumchagua kwa kishindo kuingia katika Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.

Silaa akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita, alisema kuingia kwake kwenye CC kumepanua wigo na kunawafanya vijana kuona nao wamewakilishwa katika kikao hicho cha juu cha uamuzi ndani ya chama.


“Nimekuwa nikitambua uongozi ni utumishi. Unapopata nafasi ya uongozi umebeba mzigo. Maana yake kuna mzigo umetwishwa. La kwanza ni kuwaza nini expectations (matarajio) ya wale unaowaongoza. Huduma zako lazima ziwe juu ya kile walichokitegemea.


“Kupata ujumbe wa Kamati Kuu… ile peke yake kuwa kati ya wateule 21 wa Mwenyekiti wa Taifa, ambaye ni Rais wa nchi ni heshima kubwa mno. Kwamba Bara wanateuliwa 21 na Zanzibar 21, kisha anawaambia naomba mnichagulie 14, saba Bara na saba Zanzibar, na kati ya hao saba lazima angalau wawili wawe wanawake, peke yake hiyo ni heshima kubwa mno,” ameiambia JAMHURI.


Silaa kijana mwenye umri wa miaka 31, anakuwa kijana wa kwanza kuingia Kamati Kuu kwa njia ya ushindani, bila kupitia makundi kama Umoja wa Vijana hii ikiwa ni rekodi ya pili kwake hapa nchini, kwani alikuwa kijana wa kwanza kupata umeya wa Manispaa ya Ilala akiwa na umri wa miaka 28 mwaka 2010. Kabla ya hapo alikuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo.


Anasema heshima aliyopewa ya kushika nafasi ya pili kwa wajumbe wa Kamati Kuu kutoka Tanzania Bara baada ya Stephen Wasira, inamfanya awashukuru wajumbe wa NEC kwa matumaini makubwa waliyowekeza kwake.


“Inatoa sura ya demokrasia sahihi. Mimi sina historia kwenye siasa, wala sina unasaba na familia yoyote ya kisiasa, lakini nimechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu. Hii inadhihirisha demokrasia ndani ya CCM,” anasema.


Baada ya kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa CC anasema hakufanya sherehe, bali alijua wazi kuwa sasa amepewa jukumu la kuwa jicho la vijana ndani ya CC. “Imetoa image (sura) nzuri kwenye chama kwamba vijana wanaweza kuingia,” anasema.


“Nimetoka mtaani nimeingia kwenye Kamati Kuu, sisemi kwa nia mbaya, maana unapokaa kwenye chama miaka 20 na zaidi [waliomtangulia], unaweza ukawa hujui baadhi ya mambo nje, ukasema mkate ni Sh 20,” anasema.


Anasema uwakilishi wa sasa wa wajumbe wa NEC kutoka ngazi ya wilaya na idadi ya vijana walioingia kwenye vikao vya uamuzi, unampa imani kuwa CCM itaendelea kuwa katika mioyo ya Watanzania na inawafikia wananchi wengi huko vijijini waliko kuliko hali ilivyokuwa awali.


Kuhusu wapinzani, anasema wapo wapinzani ambao wameamua kupinga kila kitu bila kutoa majibu kwa Watanzania. Yapo ambayo wapinzani wanasema, kwa mfano mfumko wa bei, si Tanzania peke yake. Mfumko ulianzia Ulaya, ukaenda Marekani sasa umerejea Ulaya. Na hapa kwetu lazima tuathirike. Mambo kama ya mafuta, yakipanda bei, usafirishaji gharama zitapanda, lazima kutakuwa na mfumko wa bei na italeta ugumu wa maisha, anasema.


Hata hivyo, anasema ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili Watanzania ni kuwaondoa watu kwenye matumizi ya vitu ghali, kwa mfano, matumizi ya mbolea aina ya ammonia na kutumia mbolea ya asilia yenye gharama ndogo.


Tayari Serikali imetangaza kujenga kiwanda cha mbolea pale Mtwara kitakachozalisha mbolea na kupunguza bei ya mbolea nchini na kuwezesha kilimo, ili wananchi wawe na chakula cha kutosha.


Moja kwa moja anawashambulia wapinzani: “Chama kina wabunge, hakisemei bungeni kinasemea barabarani. Huko bungeni ni kutukana tu kisha kusemea kwenye mikutano ya hadhara. Hawaendi majimboni kwao kamwe… ni chama cha ajabu sana hiki. CCM tusifanye siasa ya ushabiki, tuendelee na siasa za ustaarabu. Wananchi wanatuelewa na kujivunia tulipowafikisha.”


Anasema kuna baadhi ya mikoa kama Kilimanjaro ina bahati ya asili. “Mkoa wa Kilimanjaro, haujawahi kuwa na shida ya maji. Kuna watu wanasema pale wana maji, lakini uhalisia hakuna pampu hata moja pale. Chanzo cha maji ni cha asili na kipo mlimani [Mlima Kilimanjaro] maji yanasafirishwa kwa gravity (mvutano wa mteremko).


“Gongo la Mboto tunayatoa maji Pugu Kimani. Unayapeleka Pungu Mwakanga na kuyapeleka kwenye kilima Pugu Kajiungeni. Hapa tunatumia umeme. Kunahitajika ulinzi, dizeli, matumizi ya fedha za kigeni yataongezeka. Lazima tufike mahala tuwaeleze wananchi wanayopaswa kuyasikia. Kwamba maji Moshi hayana gharama kama Dar es Salaam, hivyo tuungwe mkono badala ya kukatishwa tamaa,” anasema.


Ameiambia JAMHURI kuwa inakatisha tamaa kuona viongozi wanazungumza uongo mchana kweupe, lakini nao CCM sasa wamejipanga kuhakikisha kila taarifa inayopotoshwa inawekwa sawa mbele ya wananchi kwa takwimu sahihi.


Je, unafahamu Meya Silaa anazungumziaje Mradi wa Mji Mpya Kigamboni? Unafahamu ana maoni gani kuhusu hali ya Jiji la Dar es Salaam na huduma za usafiri, mapato ya Jiji je? Usikose toleo la wiki ijayo kwa makala murua juu ya maoni ya Meya Silaa aliyezungumza na JAMHURI pekee.

1082 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!