“Mwezi Julai 1959 wakati wa kushangilia siku ya Saba Saba, Rais wa Chama, Julius Nyerere, aliweza kutamka; “Silaha ya amani tuliyotumia; njia ya Katiba ya juhudi zetu; uwazi wa nia zetu na jinsi tulivyotoa madai yetu bila uoga, umeleta sura mpya katika historia ya Tanganyika” (Kitabu: Tanzania Kabla na Baada ya Uhuru).

Nimenukuu tamko hili kwa sababu kuu tatu. Mosi, kuonesha thamani na umuhimu wa maneno umoja, amani na Katiba yalivyoenziwa tangu dahari ya kudai uhuru ya chama TANU (1954-1961 ) hadi Tanganyika kuwa huru.

Pili, chama cha siasa kinapokuwa katika harakati za kupigania haki na kutokomeza dhuluma kinavyojali amani (utulivu na usalama); na kinavyofuata na kuzingatia Katiba waliyoiunda wanachama wenyewe kuwaongoza katika mambo yao.

Tatu, kumbe juhudi, uwazi na kutokuwa na uoga, chama cha siasa kinaweza kuleta sura mpya katika historia ya nchi, bila kutoleana kauli za vitisho na ubabe; dharau na kejeli; na hata kutojenga chuki na kisasi baina ya viongozi na wanaoongozwa.

Kuundwa kwa TANU, tarehe 7 Julai, 1954 hadi tarehe 7Julai, 1959, kipindi cha miaka mitano tu, chama hicho kiliweza kujenga umoja, ari na ujasiri wa kutambulika kitaifa na kimataifa katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Ndani ya miaka mitano TANU walitumia silaha UMOJA na AMANI kujenga mshikamano wa makabila 125 nchini; Kiswahili kilifanywa lugha kuu ya mawasiliano; madai ya uhuru yalielezwa na kufafanuliwa kwa wananchi; ilitangaza misingi ya demokrasia  na ilishinda katika chaguzi kuu mbili za serikali (Septemba, 1958 na Februari, 1959 ) na kupata mawaziri wananchi.

Hayo ni baadhi tu ya mafanikio ya chama. Leo nchi iko huru na amani tele; na kuweka historia mpya ya kuwa na kizazi kipya chenye wasomi wa hali ya juu. Kinachoshangaza; sehemu ya kizazi hicho kinakwepa kujenga nguvu ya hoja ndani na nje ya chama cha siasa, kustawisha uchumi na kufanya maisha bora kwa wananchi.

Wananchi wanahitaji hoja zinazojenga uchumi na maendeleo; hoja ya kupanua elimu ya sayansi na teknolojia; kilimo na viwanda; maarifa ya utunzaji na matumizi ya rasilimali gesi, mafuta, madini, maji, viumbehai vya majini na ardhini, kwa malengo ya kuachana na umaskini.

Wala hawahitaji hoja za nguvu na kutengeneza misuto, zohali na mikingamo ili wasipate utajiri wala kuendeleza umaskini. Wanatambua umaskini umeachana hatua moja tu na utajiri. Juhudi na umoja wao ndiyo vitakavyowapeleka katika nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali.

Aidha, kuna kasoro kwa baadhi ya kizazi kipya kushindwa kutumia lugha fasaha kuimarisha silaha yetu ya umoja na amani. Ni dhahiri shahiri silaha hii inapoelekezwa mbele itashambulia adui. Ikielekezwa kwako itakudhuru na kukuua. Si jambo la kujaribu. Kufanya hivyo ni kupoteza taaluma na usomi.

Wananchi wanahitaji uchumi na maendeleo, siyo kuvuruga vikao vya chama, taratibu za vyombo vya amani, kubeza mihimili ya nchi na kutia jakamoyo watu kuhusu maisha na mali zao. Laiti hayo yangefanyika huko nyuma, leo tusingekuwapo hapa.

Uongozi wa nchi na wa vyama hauna budi kupeana chambi ili raia na wanachama waweze kuishi kwa amani. Wazee na vijana wamudu kupeana historia na maarifa mapya yanayotokea duniani wakiwa na lengo la kuimarisha amani.

Katiba ya chama (siasa au michezo ) inashabihiana na Katiba ya nchi kwa kauli na kitendo wala si kwa maandishi yaliyojaa utamu na mvuto wa lugha; uchache wa ukweli na ufinyu wa huba. Hazitakuwa katiba za wananchi bali za wavunja nchi.

Wenzetu (TANU na Serikali) waliona hitilafu kama hizo na walijitahidi kuzikwepa kwa kusoma mistari ya maneno katika Katiba na nchi (ukoloni) na katiba ya chama, hatimaye chama kilifaulu na kudumisha silaha umoja na amani na kurudisha nchi mikononi mwao salama salimini.

Vipi sasa, viongozi eti mshindwe kulinda silaha umoja na amani na kutoa nchi mikononi salama salimini na kuweka kwenye mikono ya chuma iliyoimarishwa na moto mkali huku mkishabikia umwagaji wa damu. Kilio tutalia iwapo mtafanya hivyo. Moyo wa nani hautazizima?

1073 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!