Hivi karibuni Tanzania itaanza kufaidika na ushirikiano wa kimichezo na utalii na Klabu ya Sunderland, inayoshiriki Ligi Kuu ya England. Hatua hii inafuata baada ya uongozi wa timu hiyo kutua nchini hivi karibuni na kukutana na uongozi wa Serikali kupitia Bodi ya Utalii nchini.

Moja ya mambo yatakayoanza kutekelezwa na uongozi wa Sunderland ni ujenzi wa uwanja wa michezo katika eneo la Kidongo Chekundu, jijini Dar es Salaam.

 

Mkurugenzi wa Biashara wa Sunderland, Gary Hutchinson, alinukuliwa na vyombo vya habari hapa nchini hivi karibuni akisema kuwa ujenzi wa uwanja huo utaanza siku chache zijazo na kuwa watashirikiana na Kampuni ya Kufua Umeme ya Symbion Power.

 

Hizi ni jitihada za ushirikiano uliopo kati ya Sunderland na Tanzania kupitia Bodi ya Utalii nchini. Hatua hii itaipeleka Tanzania katika mafanikio makubwa kimichezo na kiutalii pia. Hizi ni jitihada zinazoonekana na ni dhahiri kuwa mambo yanasonga mbele.

 

Wakati haya yakiendelea, kuna baadhi ya wapenzi na mashabiki wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, ambao walitaka kujua mipango ya timu yao na Sunderland imefikia wapi.

 

“Huyu jamaa wa Sunderland kaja juzi hapa Dar es Salaam, lakini hatujasikia hata kukutana na viongozi wetu Simba, hata sisi viongozi wetu walishatwambia kuwa wamekubali kutusaidia, tuna mkataba nao,” alisema mmoja wa mashabiki wa Simba, ambaye hakutaka kutaja jina lake.

 

Juzi, kuna gazeti lilimkariri kiongozi wa Sunderland, Hutchinson, akisema kuwa klabu yake haijapata kuingia mkataba wowote na Klabu ya Simba. Alisema kuwa uongozi wa klabu yake hauna ubia wa ushirikiano na Simba.

 

Hii ni kinyume cha tambo ambazo zimekuwa zikitolewa na uongozi wa Klabu ya Simba kwamba una makubaliano ya ushirikiano wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

 

Hiki ni kipimo kingine kwa uongozi wa Simba, kwani kila mara umekuwa ukilalamikiwa na wanachama wake kwa kuwa na ahadi feki ambazo matunda yake hayaonekani.

 

Kwa wafuatiliaji wa masuala ya soka la Tanzania wanajua kuwa moja ya mambo yaliyokuwa yanalalamikiwa na baadhi ya wanachama katika mkutano mkuu wa Simba uliofanyika miezi kadhaa iliyopita, ni pamoja na ahadi hewa.

 

Kuna haja ya uongozi wa Simba kutoa kauli itakayowaridhisha wanachama juu ya uhusiano ambao uongozi huo umekuwa ukiusema kati ya Sunderland na Klabu ya Simba. Na hata kama haujafikia mwafaka, ni bora ikafahamika kuwa uongozi umefikia hatua gani juu ya hilo badala ya kukaa kimya.

 

Kauli zaidi za kiongozi wa Sunderland katika vyombo vya habari zilizema kuwa kwa sasa katika Bara la Afrika Klabu ya Sunderland ina ubia na klabu mbili nchini Ghana na Afrika Kusini, ambazo huzisaidia kwa kuzitafutia wafadhili na mawakala wa wachezaji. Klabu hizo ni Asante Kotoko ya Ghana na Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

 

Kuna wakati baadhi ya viongozi wa Simba walikaririwa wakisema kuwa wamemshawishi mmiliki wa Sunderland, Ellis Short, kukubali kuisaidia Klabu ya Simba.

 

Walidai kuwa uongozi wa Sunderland umekubali wachezaji kupata nafasi ya kufanya majaribio Sunderland, makocha wao kupewa mafunzo na kujengewa kituo cha soka na uwanja wa mazoezi kwa timu za Simba za vijana.

1239 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!