Nani anataka matokeo mabovu? Kuna uwekezaji mkubwa, huku wachezaji wakipewa kila kitu, halafu unakuja kutoa sare na timu ambayo unaamini ni mbovu? Swali kubwa. Nyumba inajengwa kwa siku moja?

Matokeo ya mechi ya Ligi Kuu ya mwishoni mwa wiki kati ya Simba na Yanga ni funzo kutoka katika uwekezaji mkubwa katika sekta ya michezo ndani ya nchi hii. Unaweza usione, lakini ni funzo.

Tujiulize! Yanga iliyoonekana ya kuungaunga inayopambana na kikosi kipana chenye uwekezaji mkubwa, inatoka kuchapwa mabao mawili na kuyarudisha yote. Unadhani mshindi ni nani hapa?

Hivi unadhani Simba hawatakasirika? Unaamini Yanga ya Dk. Mshindo Msolla itaacha kufurahi kwa matokeo haya? Hata wenyewe hawaamini.

Kuna habari sasa, Simba mwishoni mwa msimu inapangua kikosi na wale wanaojitambua na kujua umuhimu wa jezi ya Simba ndio watakaobaki, lakini wanaosubiri ‘pilau’ siku zao zinahesabika.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameamua moja tu, kukisuka upya kikosi cha timu hiyo kwa gharama zozote zile.

Chanzo chetu cha uhakika kilitupasha kuwa, Mo anachohitaji yeye ni Simba kutawala kila kitu katika anga ya Tanzania na si kusumbuliwa na watu wanaoungaunga.

Msikie Manara

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, amewataka wachezaji wa timu hiyo kutambua thamani ya jezi yao na kujituma zaidi wawapo uwanjani kama wafanyavyo wapinzani wao wa jadi Yanga.

“Wenzenu hawapati mnachokipata, wanapanda daladala hadi Mbeya, hawakai kambi nzuri, hawalipwi kwa wakati, hawapati bonus mzipatazo lakini wanawazidi katika upambanaji. Kifupi, baadhi yenu mmeboa mno,” anasema Manara.

Anadai katika mchezo huo, Simba haikustahili matokeo ya sare, huku akiwabebesha lawama wachezaji kwamba wamewaangusha mashabiki, uongozi na Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mwenyekiti wake, Mohamed Dewji ‘Mo’.

Kocha wa Simba

Kocha wa Simba, Sven Van Der Broeck, anasema licha ya vijana wake kucheza vizuri kiufundi lakini wameshindwa kucheza jihadi.

Anasema katika mchezo huo uliopigwa na timu mbili; moja ilicheza kiufundi huku nyingine ikicheza kwa kujitolea.

“Yanga walitumia makosa yetu kutuadhibu, hivyo vijana wangu wamejituma kwa kucheza kiufundi, sasa tunakwenda kujipanga kwa mechi zijazo,” anasema.

Sven anasema waamuzi wa mchezo huo wametumia vema sheria za soka na matokeo yao yameamuliwa na sheria za mpira wa miguu.

Wakongwe wanasemaje?

Wakongwe na wachezaji wa zamani wa Simba na Yanga wametoa neno kuhusu mchezo kati ya timu hizo.

Ally Mayai ‘Tembele’ anasema ‘derby’ hiyo imeendelea kuthibitisha kuwa matokeo yake hayaendani na ya mechi zilizopita, na ndiyo maana inafananishwa na fainali.

Anasema hakuna ambaye alitegemea kama Simba ingetoa sare katika mchezo huo, kwa sababu walikuwa na kikosi bora na kipana, tena kilichokaa muda mrefu tofauti na Yanga ambao walikuwa wanajenga kikosi.

Boniface Pawasa anasema Simba ilipoteza umakini, kwani iliingia uwanjani vizuri lakini kadiri muda ulivyokwenda umakini ulipotea, kwakuwa walimiliki mpira muda mrefu na Yanga walianza kujilinda sana.

Anasema baada ya kuona wamewakamata wakaanza kujisahau na kupoteza nidhamu ya kiuchezaji na walifanya makosa mepesi sana.

“Simba ninadhani wamepata somo zuri, wanatakiwa wafanyie kazi mapungufu yao,” anasema.

Wachezaji wanena

Tunajua mashabiki wetu wanavyobezwa sana, mpira ni mchezo wa makosa, tulaumiwe sisi wachezaji wote,” anasema Meddie Kagere, mfungaji wa bao la kwanza la Simba.

“Nadhani matokeo tu yamegoma, tulicheza vizuri sana, tukafanya makosa mawili tukaadhibiwa, bado tunaongoza ligi hata wakishinda viporo vyao,” anasema John Bocco, nahodha wa Simba.

“Imekuwa bahati mbaya sana kwetu, lakini hatuchezi ligi kwa mchezo mmoja pekee, ligi ina mechi 38,” anasema Pascal Wawa, beki wa kati wa Simba.

“Wana haki ya kuzungumzia wanachokiamini na wameona, niwaahidi furaha yao itarejea hivi karibuni,” anasema golikipa wa Simba, Aishi Manula.

“Yanga ni timu kubwa, tulijua tutabezwa na tutachekwa, tukaja na nia moja tu, kuitetea na kuilinda klabu yetu,” anasema Ditram Nchimbi wa Yanga.

Mkwasa anasemaje?

Kocha wa Yanga, Boniphace Mkwasa, anadai kwake ilikuwa mechi ya kawaida isiyo na presha, lakini kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu kwake na akawapunguza presha wachezaji wake.

“Waliingia na matokeo, tukaingia na kudharauliwa kwetu, lakini bado ninaendelea kukijenga kikosi na nina imani tutafika ninakotaka,” anasema.

Wataka Manula asaidiwe

Baada ya kuonekana anarudia makosa yale yale kila siku, mashabiki wameibuka na kutaka uongozi umsaidie kipa Aishi Manula kurudi upya.

Kauli hiyo imekuja baada ya juzi kufungwa mabao mawili na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa.

Shabiki na mwanachama wa Simba, Juma Ndambile, anasema lawama anazielekeza kwa benchi la ufundi na wachezaji Mzamiru Yassin na Aishi Manula.

Anasema ni aibu, kwa sababu kipa huyo ndiye anategemewa hata katika timu ya taifa halafu anafungwa mabao rahisi.

Mohammed Kipukuswa anawataka viongozi wamsaidie Manula, kwa sababu inawezekana kocha aliyenaye si mzuri, kwani amekuwa akifungwa mabao yanayojirudia kila siku.

Ushauri

Kama misingi sita sahihi ya soka mpaka michezo yote isipofuatwa, bado lawama zitakuwa palepale, ila hizi timu mbili zinaweza kuwa funzo kwa michezo ya Tanzania.

Kuna umuhimu wa kuanzia chini na kuwatengeneza vijana ambao watakuwa wanajua nini cha kufanya, kwani michezo ni elimu na elimu ni michezo.

By Jamhuri