Simba, Yanga hazishangazi

Ukiona Simba wanachukua wachezaji wengi kutoka Afrika Magharibi, Yanga nao watakwenda huko. Ukiona pia Yanga wanachukua kocha kutoka Ulaya Mashariki, Simba nao watakimbilia huko.

Bahati mbaya zaidi Azam FC nao wameingia katika mkumbo wa kufuata siasa za Simba na Yanga. 

Simba labda walionekana kufurahishwa na soka la Patrick Aussems, wakaamua kumtwaa Sven Van Der Broeck kutoka hukohuko Ubelgiji ili aendeleze falsafa yake ya soka.

Sikushangaa pia kusikia Yanga wamemtwaa Luc Eyameel kutoka Ubelgiji Kikubwa ni kwamba hata makocha wa timu zote za Ligi Kuu wangetoka Ubelgiji, chakujiuliza ni je, tumepangaje kutoka hapa? Je, tukiendelea kutegemea mtu mmoja kuendesha timu soka letu litapanda?

Sitaki kuzungumzia soka la vijana wala mfumo wa michezo nchini, ila tujadili tu leo utegemezi wa kocha akuletee miujiza ambayo haipo.

Jezi za timu nyingi Ulaya zimejaa nembo za biashara za wadhamini wa kila aina. 

Kuna wadhamini wengine ambao hutangaza biashara zao kupitia uwepo wa mabango yanayowekwa pembeni ya viwanja. 

Timu moja ya ligi kuu Ulaya inatumia jezi iliyopambwa na nembo zaidi ya tatu za kampuni kubwa kibiashara na wakati huo huo yupo mdhamini wa ligi kuu.

Uwezo wa timu kumudu gharama za maisha zinazopanda kila kukicha huchangiwa kwa kiasi kikubwa na fedha za wadhamini ambao biashara zao ndizo zinazotangazwa kupitia jezi za timu.

Hakuna ukiritimba katika suala zima la udhamini wa timu au ule wa ligi kuu. Aliye tayari kuingia mkataba na uongozi wa klabu au ule wa bodi zinazoongoza ligi kuu ndiye atakayetangaziwa biashara yake. Arsenal ni mfano wa klabu zenye kujua namna ya kuwavutia wenye fedha zao, timu imeweza kuishi ndani ya bajeti zinazopangwa. Inasikitisha kuona hapa Tanzania tunao ukiritimba wa udhamini wa timu za ligi kuu.

Miaka michache iliyopita Klabu ya African Lyon ilipata udhamini wa Kampuni ya Zantel, lakini wakaambiwa na viongozi wa ligi kuu kwamba huyo ni mshindani na mdhamini mkuu wa ligi, Vodacom, hivyo hapaswi kuidhamini klabu hiyo. Matokeo yake mipango mingi ya African Lyon ikaishindwa kutimizwa na timu ikateremka daraja. 

Mtanzania gani leo hii angeijua Kampuni ya AON kama isingeingia mkataba na Manchester United? Lakini African Lyon ikakumbana na ukiritimba ambao uliikwamisha na ikashindwa kukabiliana na gharama za uendeshaji wa ligi kuu. Kila mdhamini mwenye kuingiza fedha zake kwenye soka ni mlipa kodi na udhamini wake huongeza pato la taifa.

Hivyo udhamini wa kampuni moja pekee kwa ligi kuu yetu, si jambo zuri hata kwenye suala la ongezeko ya kodi ambayo ni pato lenye kumgusa kwa njia moja au nyingine kila Mtanzania.

Si jambo zuri kutengeneza mazingira ambayo yanawakatisha tamaa wadhamini wapya. Jezi za timu za ligi kuu yetu zinapaswa kujaza nembo za wadhamini wengi kadiri iwezekanavyo. Wamarekani wengi hivi sasa wanaifuatilia Ligi Kuu ya England kiasi cha matajiri wengi kujiingiza kwenye uwekezaji kwa maana ya umiliki wa baadhi ya timu, sababu hasa ni udhamini wa kampuni za Kimarekani.

Hata timu kubwa za Ulaya zinazokwenda kwenye nchi za Asia na Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu, ni kwa sababu ya uhusiano uliopo kati ya nchi hizo na zile kampuni zinazodhamini hizo timu.

Soka la Tanzania linawahitaji wadhamini wengi zaidi ya hawa waliopo hivi sasa. Timu zetu nyingi hazina hata viwanja vya kufanyia mazoezi. Muonekano wa timu zetu nje ya uwanja bado unahitaji mchango mkubwa wa fedha, hivyo tusipende kuishi kama matajiri wakati yale mambo mengi ya msingi hayajaweza kuboreshwa.

Patrick Aussems

“Zibadili mfumo wa uendeshaji, hata kama kuna tajiri amejitokeza lazima zisake masoko ili kuinua pia soka la vijana, bila kuwekeza chini itakuwa shida na ni gharama kubwa.” 

Luc Eyameel

“Nalijua soka la Afrika, lakini kuna uwekezaji mkubwa unaotakiwa kufanyika. Yanga ina nafasi kubwa ya kufanya hivyo, ninaamini itafanikiwa.” 

Sven Van Der Broeck

“Afrikakuna vipaji vingi, tena vikubwa hasa, ila uwekezaji ni lazima uwe mpana.”

Mtazamo

KwaSimba na Yanga ambazo ndizo zinachukuliwa kama kioo, wala haishangazi kwao kutofikiria juu ya uwekezaji mpana zaidi ya kuishinda nyingine.

Haishangazi pia kuiona Yanga ikitolewa katika Kombe la Mapinduzi, Simba wanasikitika kwa sababu walitaka kulipa kisasi cha sare.