Singeli kuifunika Bongo Fleva? (2)

Katika makala iliyopita tulianza kuangalia kwa ufupi historia ya mwanamuziki Man Fongo, ambaye ni mmoja wa watu ambao wameufanya muziki wa Singeli ukasisimua nchini. 

Ingawa Man Fongo na wenzake wamefanya kazi kubwa kuutambulisha muziki huo ambao sasa unashindana na Bongo Fleva, lakini bado baadhi ya watu wanauona muziki huo kama wa kihuni kutokana na asili yake. 

Singeli kuonekana uhuni

Man Fongo anasema muziki huo umekuwa ukiitwa wa kihuni kutokana na mazingira ambayo umekuwa ukichezwa kuwa ya Uswahilini sana, ambapo vijana wa huko wanaonekana kuwa wahuni.

“Naona hii ni hali ya kawaida kwa sababu Singeli ni muziki wa vijana na vijana ni damu changa. Kwa hiyo wao muda wote wanataka kucheza, labda katika kufanya vile watu wengine wakauona ni wa kihuni.

“Muziki huu jamani si wa kihuni, labda watu wanaoupenda ndio wanaonekana wahuni… Uswahilini hawaishi mabrazamen, huku wanaishi watu wa kawaida, ndiyo maana labda unachukuliwa kihivyo, lakini ni muziki mzuri, mtamu na unachezeka,” anasema.

Changamoto

Hata hivyo, licha ya mafanikio makubwa ambayo muziki wa Singeli umefikia, bado kuna changamoto na vikwazo vingi kwa muziki wenyewe na kwa wale wanaoimba muziki huo. 

Man Fongo anabainisha kuwa msanii anapokuwa staa, lazima kuwe na changamoto mbalimbali anazokutana nazo. Anasema amekuwa akipata usumbufu mkubwa kutoka kwa wasichana katika mitandao mbalimbali ya kijamii wanaomtaka kimapenzi.

“Siishiwi kupigiwa simu na baadhi ya wadada wakinisumbua, Instagram huko ndiyo shida zaidi… lakini ninajua ni mashabiki wangu, siwezi kuwachukia ila ukweli ni kwamba mimi nina mchumba wangu ambaye nipo naye kwa muda mrefu sana, baada ya kipindi kifupi kijacho tutafunga ndoa.

“Kupendwa kupo, lakini wajue tayari miye ni mali ya mtu. Napenda sapoti yao, waendelee kupenda muziki wa Man Fongo lakini si mambo ya mapenzi,” anasema Man Fongo.

Pia anaeleza kinachomchukiza zaidi katika muziki, ambapo anasema yeye hapendi kupigana, kwa sababu wakipigana ndiyo wanaonekana wahuni wakati lengo lao ni kuufanya muziki huo kukubalika kimataifa.

Anasema muziki huo ulikuwa umekwisha kuaminika kwamba ni wa kihuni, kwani hata mitindo yake ya uchezaji imekuwa si ya kufaa kwa jamii, pia umekuwa ni wa hatari kwa kuwa watu wengine hucheza na silaha.

“Muziki wa Singeli ulikuwa bado mchanga na walikuwa hawajaupokea, ulikuwa unaonekana wa kihuni, zamani ilikuwa wanacheza wahuni tu kati, ukicheza uwe na roho ngumu hasa, lakini sasa hivi kina mama, watoto, masela na kila mtu anacheza, mpaka tunaingia studio kubwa,” anabainisha Man Fongo.

Anaendelea kusema kuwa sababu zilizoufanya muziki huo uonekane wa kihuni ni kutokana na kipindi hicho hawakuwa na uwezo wa kuingia studio kubwa na kuurekodi na kuupa hadhi nzuri kwa jamii.

Man Fongo anasema kuwa amepata mafanikio makubwa kupitia muziki wa Singeli kwa muda mfupi kuliko matarajio yake ya hapo awali.

Man Fongo anasema anayashangaa mafanikio makubwa ambayo ameyapata ndani ya muda mfupi kupitia muziki wa Singeli, hususan kupitia kazi yake ya ‘Hainaga Ushemeji’, ambayo imemtambulisha vema kwa jamii.

Staa huyo wa Singeli anasema kuwa muziki huo umebadilisha maisha yake ndani ya muda mfupi, na sasa anaona maisha kwake ni kama mepesi akilinganisha na kipindi cha nyuma.

Man Fongo anasema amekwishaanza kumwandaa mtoto wake wa kiume kuwa msanii mkubwa zaidi yake.

“Nataka mtoto wangu aje kuwa msanii mkubwa kunizidi mimi na nimejipanga kumwandalia njia ambazo zitakuwa rahisi yeye kufanikiwa kwa urahisi kuliko njia ngumu nilizopitia, nitampatia elimu bora na kumfunza heshima na nidhamu ya hali ya juu,” anasema Man Fongo.

Man Fongo anasema muziki wa Singeli umesababisha mpaka amepanga nyumba nzima maeneo ya Tabata, huku akimiliki gari aina ya Toyota Altezza, akisisitiza kuwa hayo ni mafanikio makubwa kwake.

Anaongeza kusema kwamba hayo ni mafanikio makubwa kwake yaliyokuja kwa muda mfupi sana kutoka kuishi maisha ya ghetto – chumba kimoja mpaka sasa anaishi nyumba nzima huku familia ikimtegemea yeye.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa magazeti na mitandao ya kijamii.

Mwandaaji anapatikana kwa simu namba: 0784331200, 0713331200, 0735331200 na 0767331200.