Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeshangazwa na kuwepo kwa mvutano wa chini kwa chini kati ya Mamlaka ya Bandari (TPA), Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na wadau wengine.

Kamati hiyo imekutana na wadau wa bandari nchini mwishoni mwa wiki ili kuweza kuwasikiliza na kupata maoni yao kuhusiana na sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kufahamu changamoto zao.

Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Dk. Dalali Kafumu imeshangazwa na kuwepo kwa mvutano wa wadau wa sekta hiyo ambao wameilalamikia TRA na TPA huku wakiwatuhumu kwa kutokuwa na ushirikiano wa kutosha katika kuboresha huduma za bandari nchini.

Mkurugenzi wa operesheni wa Tanzania Road Haulage (1980) Ltd Group of Company, Ali Lilani anasema matumizi ya sheria mpya ya Sumatra inayozitaka bandari kavu (ICD) kujengwa  kilometa zaidi ya 30 toka bandarini ni jambo ambalo linakiuka  haliwezekani katika kipindi kifupi kutokana na kutumia gharama kubwa katika uwekezeaji wa awali uliokuwa hauna sharti hilo.

“Wafanyabiashara wamefanya uwekezaji mkubwa, dola za kimarekani milion 9-10 na sasa unamtaka atafute eneo jingine la uwekezaji wakati keshaweka pesa yake hapo, walichukua mikopo ili wawekeze,”anasema Lilani.

Anasema kuwa wapo wawekezaji na wamiliki wa ICD’s ambao hawajapata mzigo kutoka bandarini kwa kipindi cha miezi 3 mpaka minne jambo lililowasababishia hasara kubwa huku wakishindwa kulipa mikopo ya benki pamoja na kulazimika kusimamisha ajira kwa wafanyakazi wa kampuni hizo.

Seleman Mnyayo anasema kuwa Mkurugenzi Mkuu wa bandari ni tatizo maana wamekuwa wakiomba kukutana naye ili kuweza kufanya majadiliano naye lakini amekuwa akiwakwepa jambo ambalo wanaamini ya kuwepo kwa agizo la siri.

“Nafikiri kuna agizo la bandari  kuongeza makusanyo kutoka billion 600 mpka trillion 1 sasa  wameamua kuzigeukia ICD, maana bandari wapo kimya, hawaleti kazi kwa zaidi ya miezi mitatu na ajira zimekufa”anasema Mnyayo.

Akizungumzia mapendekezo ya wadau, Dk.Kafumu amesema kutokana na maoni ya wadau ameweza kubaini kuwa serikali haipendi kukutana na wadau jambo ambalo limekuwa tatizo katika sekta mbalimbali.

Dk. Kafumu anasema wadau wote wanalalamikia VAT iliyowekwa  ambayo inaonekana kuwa tatizo kubwa hivyo ipo haja ya kuangaliwa upya ili kuweza kuondoa kero hiyo inayopingana na taratibu za kimataifa.

“Pamoja na utawala mpya, viongozi wengi hawashirikishi wadau, hawataki kukutana hata wanapowaongezea kodi, haiwezekani unamtengenezea mtu bila kumshirikisha. Hapa pana tatizo linalohitaji kufanyiwa kazi haraka” anasema Dk. Kafumu.

Dk. Kafumu anasema atahakikisha anafanya mchakato wa kuwakutanisha wadau wa bandari na serikali ili kuweza kuubaini ukweli mapema iwezekanavyo katika kipindi hiki cha bunge kabla ya Januari mwakani.

Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni anasema wadau wa bandari wanao uelewa mpana wa masuala yanayopaswa kutekelezwa kuliko waliokabidhiwa dhamana ya bandari.

Chegeni anasema kuwa kila Mtanzania anahitaji maisha bora hivyo ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake ipasavyo.

“Ni lazima kuondoa upotoshaji unaofanywa kwa makusudi, hapa wadau wametulisha afya njema ya neema ya nchi yetu.  Kuna upotoshaji mkubwa unaofanywa kwa makusudi kabisa hasa na watendaji ndani ya serikali jambo ambalo lazima likemewe na kuchukuliwa hatua za makusudi”anasema Chegeni.

Anatropia Theonest anasema kuwa kumekuwa na tabia ya kuwaangalia wafanyabiashara kama wezi na watu wasiofaa nchini kutokana na upotoshwaji unaoendelea jambo ambalo si sahihi.

“Mizigo haipitishwi tena bandarini, nchi inapoteza zaidi ya asilimia 42, kwa sasa kutokana na kupungua kwa mizigo, ufike wakati ukweli ujulikane na rais wa Jamhuri ya Muungano John Magufuli aambiwe ukweli  kuwa anadanganywa na watendaji wake” anasema Anatropia.

Wakati mbunge huyo akisema shehana ya mizigo imeshuka kwa asilimia 42, ripoti ya TRA na TPA zinaonyesha kuwa mzigo umeshuka kwa wastani wa asilimia 9-30.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamalaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko ameieleza kamati ya bunge kuwa sababu za kushuka kwa mizigo bandarini ni kuzibwa kwa mianya ya ukwepaji kodi.

Hata hivyo anasema kuwa kutokana na kuzibwa kwa mianya hiyo ya ukwepaji kodi, mapato yamezidi kupanda  kutokana na kila mzigo kulipiwa tozo yake kama inavyotakiwa ikiwa ni pamoja na iliyokuwa ikitunzwa katika bandari kavu ambayo ilikuwa hailipiwi kama ilivyotakiwa.

Pia ameeleza kuwa kupungua kwa mizigo bandarini kunatokana na mtikisiko wa uchumi ambao umeikumba nchi ya China ikiwa ni  pamoja na nchi jirani za Zambia na Congo kusafirisha mizigo yake kwa kutumia njia ya reli.

Katika maelezo yake, Mhandisi Kakoko ameonesha kushangazwa na mikataba ya ICD’s kuwa mibovu huku akimshangaa aliyetia saini mikataba hiyo.

Pia ameeleza kuwa bandari imeanza kuweka vitega uchumi vyake ili iweze kujiendesha kwa faida lakini katika miradi yake hiyo haipo tayari kupokea mikopo yenye masharti yasiyo na tija kwa taifa kama ambavyo baadhi ya nchi zimefanya.

Mkurugenzi Mkuu huyo anasema, wapo baadhi ya vigogo ambao pia wamekuwa mstari wa mbele kuiangamiza bandari kwa kutumia nyadhifa zao kujinufaisha jambo ambalo hayuko tayari kuliona katika uongozi wake.

 “Wapo vigogo na baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakitaka upendeleo kwa viongozi wa bandari jambo ambalo limechangia limeiua bandari hii, yuko mbunge mmoja alikuja nikamfukuza siwezi kutoa upendeleo wowote” anasema Kakoko.

Hata hivyo ameongeza kwa kusema kuwa ni lazima mamala ya mapato (TRA) ibadilishe mfumo wa utendaji ili kuenenda na sayansi na teknolojia katika kitengo cha kutoza ushuru kwani wamekuwa wakitumia utaratibu wa kizamani katika kutoza ushuru.

Baadhi ya wachumi waliozungumza na JAMHURI wanasema, Ni ukweli uliowazi kuwa kwa kiasi fulani mizigo imepungua kwa wastani wa asilimia 9-30 kutegemea na nchi.

“Mizigo mingi iliyokuwa inapita bandari ya Dar kwa kisingizio inaenda Kongo siyo kweli ilikuwa inaenda Kongo badala yake ilikuwa wana-dump humu nchini, kudorora kwa bei ya shaba Zambia, Uchaguzi Malawi, amani na utulivu wa Msumbuji kiasi kwamba bandari ya Beira imeanza kufanyakazi vizuri,” anasema mmoja wa wachumi ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.

Anataja sababu nyingine kwamba ni kuanza kutumika kwa utaratibu wa ushuru wa pamoja wa forodha ambapo mizigo inalipiwa katika bandari ya Dar es Salaam, kabla ya kusafirishwa kwenda Kongo DRC ambapo inawanyima wafanyabiashara kule Kongo kukwepa kodi.

Mchumi huyo anasema, wakati meli zikiwa zimepungua katika bandari ya Dar es Salaam, mapato yatokanayo na forodha mwaka 2015 yalikuwa wastani wa Shilingi Bilioni 200-300 kwa mwezi. Tangu Disemba 2015 – August 2016 wastani wa mapato ya Forodha kwa mwezi ni kati ya shilingi bilioni 400-550.

By Jamhuri