Wiki iliyopita nilieleza namna changamoto za kiuchumi zinavyowahenyesha wafanyakazi. Pia nilianza kueleza mchapo unaonihusu wa namna nilivyopambana kujikwamua kiuchumi nikiwa nimeajiriwa kwa kazi ya ualimu. Leo nitahitimisha kwa kubainisha mbinu kadhaa ili kumudu mchakamchaka wa maisha ya kiuchumi. Endelea…

Nimepokea makumi ya simu na meseji kutoka pande zote za nchi. Pamoja na mambo mengi, wasomaji wengi wamekuwa na kiu ya kutaka kufahamu, je, ningali nikiendelea na ualimu? Je, biashara niliyoianzisha inaendeleaje?  Naomba nijibu swali la kwanza na hili la pili nitalijibu kiuchambuzi katika makala zijazo.

Kama nilivyosema wiki iliyopita ni kuwa mwaka 2007 niliajiriwa kuwa mwalimu wa muda nikitokea kidato cha sita. Nilifundisha kwa mwaka mmoja na baadaye mwaka 2008 hadi 2011 nikajiunga na masomo ya biashara, chuo kikuu kwa ngazi ya shahada. Nadhani kwa uchache nitakuwa nimekidhi kiu ya wasomaji wengi walioniuliza na wale ambao hawakubahatika kuwasiliana nami.

Ningependa pia kutambua baadhi ya michango ya wasomaji. Jackson Mashimba kutoka Mwanza ameandika, “Hongera Sanga kwa makala zako zinazotufungua sana. Inabidi ufanye utaratibu uandae semina uje utuelimisha hapa Mwanza, tutafurahi sana kukuona”. Rashid Farouk kutoka Wete Zanzibar aliniandikia, “Big up, nakupata vizuri sana.”

Mama Jane kutoka Mvumi-Dodoma alinipigia na tukazungumza kwa kirefu sana, lakini baadhi ya mazungumzo yake yalikuwa kama hivi: “Ni kweli ulivyosema, ndiyo maana kama sisi walimu unakuta tunapochukua hata mikopo hatufanyii mambo ya kiuzalishaji. Mwisho wa siku unakuta mshahara unakatwa hela hazitoshi na mkopo umepeleka kwenye mambo yasiyo na msingi…”

Kwenye makala yangu ya wiki iliyopita kuna mambo kadhaa nanayopenda wafanyakazi mjifunze. Kwanza ni uwezo wa kubaini fursa zilizopo katika eneo uliloajiriwa. Natambua kuwa si kila sehemu wanalima vitunguu, lakini kuna fursa nyingine nzuri tu.

Unaweza kupanda shamba la miti, unaweza kufungua banda la video, unaweza kuanzisha kampuni ya ushereheshaji, unaweza kununua hisa au hata kuwa mwanahisa katika kampuni mojawapo kwenye eneo lako au sehemu nyingine. Jambo la kwanza ni kutengeneza ‘interests’ kwa jambo unalotaka kulifanya.

Nitoe rai pia kwa wale ambao huwa wanayakataa maeneo ya vijijini  wanapopangiwa kazi. Hakuna haja ya kukataa maeneo ya vijijini kwa sababu ninaamini na nimethibitisha kuwa kwa mtu unayejituma, vijijini ndiko kwenye fursa nzuri na nyingi kuliko hata mijini; ni suala la kubadilisha mtazamo tu.

Binafsi nakumbuka wakati nikiwasili Shule ya Sekondari Karatu nilikuta mikondo ya sayansi kwa kidato cha tano na sita ikiwa na wanafunzi takribani 900, lakini kulikuwa hakuna mwalimu hata mmoja wa Kemia wala Baiolojia. Nililazimika kubeba jukumu la kufundisha wanafunzi 900 masomo mawili; mikondo zaidi ya 16! Nilimuuliza mkuu wa shule kulikoni hali iwe hivyo?

Akanieleza kuwa walimu wanaopangwa kwenda pale ni wengi, lakini wengi wao wakifika na kuyatazama mazingira huaga kuwa wanakwenda kufuata familia au mizigo, na hawarudi tena! Mkuu wa shule akanieleza tena kuwa kama walimu wote waliowahi kupangiwa shule ile wangekuwa wameripoti, kusingekuwapo na upungufu mkubwa kama uliokuwapo.

Leo ninaandika kwa ujasiri kuwa mahali ambako wengine walipaona kuwa ni kijijini na kukataa kwenda; ndipo mahali kulikoniwezesha kuzalisha fedha hadi kuanzisha biashara ya chuo! (Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni). Nawasihi sana wafanyakazi muwe makini na wachunguzi wa ‘mawe’ kabla ya kuyakataa kwani huenda yakawa ni mawe makuu ya maisha yenu!

Unaweza kujiuliza; “Huyu Sanga anayetuandikia uchambuzi huu ni nani kwa sasa? Anafanya nini? Na ana mafanikio gani kiuchumi hadi anathubutu kutuandikia mambo ‘makali’ namna hii?” Kwa kujua kuwa watu wengi watajiuliza hivyo, ndiyo maana nimetoa simulizi yangu ya ‘ualimu’ nikiwa kule Karatu.

Kimsingi sina mambo makubwa ya kujivunia kiuchumi, lakini kwa yale machache niliyopata kuyapitia ninaona ni hekima kuyashirikisha kwa wengine. Najua hayawezi kumfaa kila mmoja, lakini kama alivyonifundisha mama yangu, ninaamini wapo wenye ‘mitazamo tofauti’ na ambao wapo tayari kujifunza; hao ndiyo ninaoamini watasaidika kwa maudhui ya makala hii.

Jingine nalitamani ulidake kutokana na makala yangu ni changamoto za kupanga na kutekeleza malengo. Ukiangalia jinsi nilivyosimulia, namna nilivyopigana na biashara ya vitunguu, unaweza kudhani ilikuwa ni ‘one-touch business’. Ukweli ni kwamba kabla ya kuipatia biashara ya vitunguu, kuna biashara lukuki nilizipanga na kujaribu.

Kuna ambazo ziliangukia pua nikiwa ndiyo naanza, kuna nyingine zilinitoa jasho kabla hata sijaanza, na kuna nyingine hazikuzalisha faida, badala yake zikaniachia madeni. Hili nalo litakuwa somo tunavyoendelea na uchambuzi mbalimbali.

Lakini ninachotaka mbaini kwa sasa ni hiki; “Maisha ni kupanga na kujaribu; ukijaribu ukashindwa panga tena na ujaribu, usiache kupanga na kujaribu hadi siku utakapoona umepata unachokitafuta.” Wakati mwingine unahitaji kufanya uamuzi mgumu na kuthubutu mambo makubwa.

Natambua kuwa kuna mambo ambayo yanawagharimu wafanyakazi wengi. Mambo haya ni pamoja na hali ya kupenda ukawaida, hali ya kuridhika, kushikilia tamaduni mfu, imani zinazofisha kuhusu fedha pamoja na hali ya kupenda na kufurahia ‘usalama’.

Kuna kitu wafanyakazi wengi mnachokipenda kinaitwa “Job Security”. Kitu hiki ni ile kiu anayokuwa nayo mfanyakazi kutazamia kutoondoka/kutofukuzwa kazini na wakati huo huo sheria za kazi ziwe zisizobana na marupurupu yawe mazuri.

Hali nyingine inayofurahiwa inaitwa “comfort zone”. Hii ni hali ambako mfanyakazi hapendi kufanya jambo ambalo litamuondolea ‘utulivu’ hata kama jambo hilo linahusisha kukuwa kwake kiuchumi au kimtazamo.

Ili kujilinda na kubaki katika “comfort zone”, wafanyakazi wengi huwa wanaona suala la kuhangaika na vitegauchumi ama biashara ni kujichosha pasipo sababu. Ni kweli kuwa biashara na vitegauchumi wakati mwingine huambatana na hasara, lakini kuogopa hasara ni kuogopa kukua.

Hata mtoto mchanga hulia sana akiwa mchanga kwa sababu mifupa huwa inatanuka na kusababisha maumivu wakati akikua. Ule mtazamo wa kutarajia ajira ifanye kila kitu unachelewesha malengo yako. Na kutokana na kukosa mbinu za uanzishaji vitegauchumi na biashara katika njia zilizo halali; ndiyo maana tuna rundo la wafanyakazi ambao wanatatua matatizo yao kifedha kwa kuiba na kufanya ufisadi kazini.

Hili ni hatari kwa sababu fedha unayoipata kwa ufisadi au wizi haiwezi kukupa furaha ya kweli katika maisha. Dunia haina mchezo katika hili kwani mabaya humrudia mbaya. Unaweza kuiba fedha ukajenga hekalu, lakini malipo ukayapata kwa kupata mgogoro katika ndoa.

Unaweza kufanya ufisadi na kujitajirisha, lakini watoto wakawa ni wahuni na wanaokuumiza kichwa na kukunyima furaha duniani. Zipo njia nyingi na nzuri za kutajirika kiasi ambacho hakuna umuhimu wa kuwa fisadi au mwizi. Hata hivyo, zipo ajira ambazo mwajiriwa hana nafasi ya kuiba wala kufisadi.

Ndiyo maana wengi wanaendelea kuishi kwa mshahara hadi mshahara (pay-check to pay-check). Asilimia kubwa ya wafanyakazi huwa wanaishiwa na akiba za mishahara kabla ya tarehe ya kupokea mshahara mwingine. Kinachofuata hapo huwa ni kukopa na kuishi na madeni yasiyoisha. Niwakumbushe kuwa ipo tofauti kubwa kati ya mkopo na deni.

“Job security” na “comfort zone” ni magonjwa hatari sana kwa wafanyakazi ambayo yanasababisha vidonda viitwavyo uhaba wa kifedha (financial scarcity). Kwa mshahara wowote anaolipwa mfanyakazi sioni sababu ya kuishi maisha ya uhaba wa kifedha.

Mimi si daktari wa “magonjwa” yote yanayowakabili wafanyakazi, lakini kwa haya mawili angalau nazijua dawa zake kwa sababu niliwahi “kuugua” nikajitibu na kupona. Mimi si nyuki, lakini ukinifuata angalau naweza kukupa asali ya maarifa ninayoyajua.

Kwa haraka haraka kabla sijawaageni kwa leo nimalizie la mwisho mnalotakiwa kulielewa kutoka katika kisa changu nilichokieleza. Ili mtu ufanikiwe kiuchumi kuna wakati unatakiwa kuweka kando aibu, hadhi (status) na kujidharau.

Kinachowatesa wafanyakazi wengi (ambao sehemu kubwa ni wasomi) ni kulinda hadhi (status protection). Msomi wa chuo kikuu; licha ya mshahara wake kuwa kiduchu, hataki kufuga ng’ombe au kuku; kisa? Ataonekana ‘mshamba’! Ofisa hataki kufungua banda la chipsi hata kama lina faida kiasi gani, kisa? Mabanda ya chipsi yanamilikiwa na waliochoka! Shauri yenu!

Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi!

[email protected], 0719 127 901

By Jamhuri