Siri za Ponda kupigwa risasi zavuja

Siri nzito zimevuja juu ya sababu za Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda kupigwa risasi mjini Morogoro mwishoni mwa wiki. Wakati Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, akiliambia gazeti la Daily Telegraph la Uingereza Jumamosi usiku kuwa polisi ndio waliompiga risasi Ponda wakati anajaribu kukimbia, magazeti ya Tanzania Shilogile ameyaambia hajui kilichotokea.

“[Ponda] Alifanikiwa kuwakwepa polisi hapa Morogoro, alipigwa risasi na maafisa wetu [wa polisi], lakini bado tunamtafuta,” Shilogile aliliambia gazeti la Daily Telegraph.

 

Shilogile huyu huyu gazeti la Mtanzania Jumapili aliliambia hivi: “Hakuna mtu aliyefikishwa hosplitali akiwa na majeraha ya risasi. Katika mazingira kama yale ya vurugu si rahisi risasi za moto zikafyatuliwa pasipo kujeruhi au kumpata mtu au watu.”

 

Ijumaa ya wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai nchini (DPP), Elieza Feleshi, aliagiza Ponda akamatwe kwa maelezo kuwa amevunja masharti aliyopewa ya kifungo cha nje.

 

Ponda alikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uchochezi na kuharibu mali ikiwamo kuchoma makanisa huko Mbagala, Oktoba mwaka jana, lakini aliachiwa Mei, mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kufungwa kifungo cha nje mwaka mmoja.

 

Moja ya masharti ilikuwa ni kumpiga marufuku asijihusishe na vurugu zozote au kufanya uchochezi wowote wa kidini ndani ya muda huo, sharti analodaiwa kulivunja alipokwenda Zanzibar wiki mbili zilizopita kwa kuchochea Waislamu dhidi ya Wakristo na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi anayodai kuwa inajiendesha kwa mfumo Kristo.

 

Wakati Ponda akidai Serikali iliyopo madarakani ni ya mfumo Kristo, wachambuzi wa mambo wamekumbusha kuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wake wote wawili; Maalim Seif Shariff Hamad na Balozi Seif Idd ni Waislmu, hoja wanayosema haina mashiko.

 

“Hivi leo kama ingekuwa viongozi hao wakuu ni Wakristo Ponda angesemaje?” alihoji Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuongeza: “Kimsingi waliopaswa kulalamika ni Wakristo kwani vyeo karibu vyote vya juu katika nchi hii vimeshikiliwa na Waislamu.”

 

Ponda inaelezwa kuwa baada ya kupigwa risasi, alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ambako alipofika ghafla alitoroshwa na kupelekwa Msamvu kwenye Hospitali ya Islamic Foundation, ambako nako alihamishwa usiku na kukimbizwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

JAMHURI limedokezwa kuwa kutokana na taarifa mbalimbali za kiinteligensia zilizopo, Sheikh Ponda ni mshirika wa kundi hatari la al-Qaeda linalotaka kusambaza Uislamu duniani kote kwa nguvu na kwamba alipokwenda Zanzibar juzi alikutana na viongozi wa kundi la Uamsho waliojadili nia hiyo ya kuendeleza Uislamu kwa nguvu zote.

 

Miongoni mwa masheikh wa Uamsho aliokutana nao Sheikh Ponda ni pamoja na Sheikh Farid Hadi Suleiman, Mselem Ali Mselem, Musa Juma Issa , Suleiman Majisu na Haji Sadifa ambaye ni Mkuu wa Usalama wa Uamsho.

 

Masheikh hao wanashirikiana na kundi la al-Qaeda kupitia mtandao wa Kiislamu uliopo Kenya uitwao Al Hijira, ambao uliasisiwa na kundi la vijana wa Kiislamu nchini Kenya lijulikanalo kama Muslim Youth Centre.

 

Taarifa ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyochapishwa ikiakisiwa na Barua ya Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya Julai 12, 2013 inalihusisha kundi la al-Qaeda na kundi la Ansar Muslim Youth Centre la Tanzania, lenye makao makuu yake Dar es Salaam ambalo Ponda anadaiwa kuliongoza.

 

Gazeti la the Mirror la Uingereza toleo la Jumapili, lilisema Ponda alikwenda Zazibar mwishoni mwa Julai kufanya mazungumzo na viongozi wa kundi la Uamsho Zanzibar wanaopokea misaada kutoka kundi la Al Hijira la Kenya ambalo ni tawi la al-Qaeda.

 

Linamtuhumu kuwa kati ya mambo waliyopanga ni kuwamwagia tindikali mabinti wa Uingereza; Kirstie Trup na Katie Gee, wakitumaini kuwa tukio hilo litatangazwa kwa nguvu kimataifa na kulipa nguvu mpya kundi la Uamsho lililokuwa linaelekea kupotea katika ramani ya ugaidi.

 

Sheikh Ponda na viongozi wa Uamsho, wanatuhumiwa kusaidiwa fedha na viongozi wa al-Qaeda, ambao ni Sheikh Abubakar Shariff Ahmed “Makaburi” wa Kenya na raia wa Uingereza, Jermaine John Grant, ambaye yuko gerezani lakini anaendeleza harakati zake za kigaidi kwa kutumia washirika hao.

 

Hadi sasa, polisi wanaendelea kumtafuta Ponda lakini kubwa inaelezwa kuwa ndio hilo wanalenga kusambaratisha mtandao wa al-Qaeda kabla haujajenga mizizi nchini na kukomaa kupitia kundi la Uamsho, Ponda na Ansar Sunni, wanaovaa suruali fupi wakiwa tayari kukimbia likitokea la kutokea, huku wakitambuana kwa ishara ya kufuga mzuzu ulionyooka sawa na ndevu za beberu.

 

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutambua hatari ya Ponda katika Bunge la Bajeti lililopita ilitoa tamko rasmi la kumzuia Ponda kuingia visiwani Zanzibar na kwamba alipoingia tu mwezi Julai, ilitangazwa rasmi akamatwe na kufikishwa mahakamani, lakini alitoroka kwa njia zisizofahamika hadi alipoibukia Morogoro mwishoni mwa wiki. Tamko la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar la kumpiga marufuku Ponda kwenda Zanzibar lilitolewa na Balozi Idd.