Sisi bodaboda wao wachukue madini

Wiki iliyopita niliandika maono yangu juu ya kifo cha Tanzania. Nimepata ujumbe wa maandishi na simu nyingi. Wapo walioniunga mkono, wengine wamenishambulia. Kwangu, yote ni heri, kwani hiyo ndiyo faida ya demokrasia na uhuru wa kutoa mawazo.

Nilipenda sana niendelee na mjadala huo, lakini naomba kwa leo niuweke kiporo, hasa kuwajibu wale wanaodhani busara kama za kina Mzee Jaji Bomani, ni za maana sana kwa mustakabali wa Tanzania na Afrika kwa jumla.

 

Mjadala wangu leo unajikita kwenye Bajeti ya Serikali iliyosomwa bungeni wiki iliyopita. Tayari yamezungumzwa mengi, lakini hayakumalizwa! Nami naomba nishiriki japo kidogo tu.

 

Aliyeisikiliza au kuisoma, hatasita kuamini kuwa ni bajeti iliyotokana na ushawishi wa wafanyabiashara wakubwa. Misamaha ya ushuru na kodi kwenye bidhaa na huduma mbalimbali vimelenga kuwabeba matajiri na kuwaumiza makabwela. Unapofuta ushuru kwenye biashara ya pampasi unalenga kumsaidia nani? Mama au baba gani wa maisha haya ya kawaida anayeweza kumudu kununua pampasi? Utaona hapa walengwa wa manufaa hayo ni watu wa maisha ya kati na matajiri.

 

Kwa mara nyingine ushuru kwenye mafuta ya mawese yanayoingizwa kutoka Asia, umekuwa sifuri. Hapo hapo unataka wananchi walime alizeti na mazao mengine ya mbegu za mafuta ili wapambane na waagizaji mafuta wasiolipa hata senti ya ushuru! Hoja hafifu zinazotolewa na mabingwa wetu wa uchumi ni kwamba tuna upungufu mkubwa wa mafuta ya kula nchini! Kama ni hivyo, upungufu huo utamalizwa vipi na wakulima wetu kama mafuta ya mawese yataendelea kuingizwa bila ushuru wala kodi? Kilimo Kwanza kitafanikiwa kwa muujiza upi? Hapa utaona hii bajeti ni ya kuwanufaisha matajiri tu.

 

Kwenye bajeti hii kumepandishwa bei ya mafuta. Kwenye uchumi, mafuta yakishapanda bei, maana yake ni kwamba maisha yote kwa kabwela ni balaa. Wanaobeba mzigo wa kupanda kwa bei za mafuta ni masikini wanaohitaji kusafiri na kusafirisha mazao kutoka mashambani. Mafuta yanapopanda bei, hiyo haimuumizi mwenye basi, bali yule anayehitaji kusafiri. Mafuta yanapopanda bei, msafirisha vyakula kutoka mashambani haumii, isipokuwa kiama ni kwa mlaji.

 

Sasa kuna suala hili la kufuta ushuru na kodi kwenye bodaboda. Sijui nchi hii tumepigwa laana na nani? Inakuwaje hawa wachumi na wabunge wetu waamini kuwa bodaboda na bajaji ni chanzo muhimu cha kupunguza umasikini? Hivi kweli tunaweza kuubadili uchumi wa Tanzania hata uweze kupaa, kwa fikra dhaifu za kuhamasisha vijana kuendesha bodaboda na bajaji? Wataalamu wetu wote wa uchumi wenye shahada za juu wanaamini kabisa kuwa bodaboda ni kitu cha maana sana kwenye uchumi kuliko trekta? Nchi hii inahitaji dua!

 

Kibaya zaidi, wameondoa ushuru kwa kigezo kwamba hatua hiyo itawasaidia vijana! Itawasaidia vipi wakati vijana hawa wanafundishwa kujiona kuwa ulipaji kodi na ushuru mbalimbali kwa nchi ni jambo la hisani? Kama ushuru ulikuwa Sh 100,000 kwa mwaka, kwanini usingepunguzwa walau hadi Sh 5,000 tu ili kuwajengea nidhamu ya kutambua umuhimu wa ulipaji kodi?

 

Viwango vya kodi viwe “rafiki”. Viwashawishi watu kulipa. Tufanye kama Charles Keenja alipokuwa Mwenyekiti wa Jiji la Dar es Salaam. Hakuongeza kodi mpya. Alisimamia ndogo iliyotozwa, akahakikisha inalipwa na wengi. Tanzania yetu sasa inataka wachache ndiyo walipe kodi kubwa, badala ya wengi walipe kodi kidogo kidogo ili ipatikane kubwa. (Kwa wale wa siku nyingi kuna msemo maarufu jijini Tanga wakati ule, wa Kibaniani, unaosema

 

“Dododogo mingi sinda kuba moja). Matokeo yake ni ukwepaji kodi uliopindukia.

Isitoshe, nani kawahadaa wakubwa hawa serikalini na bungeni hata wakaweza kujiaminisha kuwa bajaji ni za vijana na si za matajiri walionunua nyingi na kuwaajiri vijana hao? Je, wanatambua kuwa wapo watu wanamiliki pikipiki au bajaji zaidi ya 30? Huyu anaondolewa ushuru na kodi kwa kigezo gani? Mapato ya tajiri huyu kwa mwaka hayamwezeshi kweli kulipa kodi? Iweje mfanyakazi anayelipwa Sh 300,000 kwa mwezi alipe kodi, lakini anayeingiza Sh milioni 30 kwa kipindi kama hicho asilipe kodi?

 

Kibaya zaidi, wakubwa hawa wanajua namna bodaboda na bajaji zinavyosababisha maafa katika nchi yetu. Wanajua Hospitali ya Muhimbili ya jijini Dar es Salaam na nyingine nchini zilivyolemewa  na wagonjwa wa viungo. Wanatambua pasi na shaka kwamba kuna idadi kubwa ya watu wanaopata ulemavu wa viungo kutokana na ajali za pikipiki hizi.

Tena basi, wanatambua kuwa vijana wanaoendesha vyombo hivi hawana mafunzo rasmi. Kama hivyo ndivyo, kwanini hawakuwekewa msamaha wa kodi kwenye matibabu ya viungo? Je, madhara ya hewa yanayosababishwa na pikipiki hizi ambazo nyingi hazikidhi viwango, yatafidiwa kwa namna gani na nani atatoa fidia hiyo?

 

Serikali kupitia kwa waziri mwenye dhamana ya ajira nchini, Gaudence Kabaka, mwaka juzi, kwa mbwembwe kabisa ilisema ajira imeongezeka kwa asilimia moja na ushei! Mbwembwe za Serikali kuhusu ajira zimeelekezwa zaidi kwa vijana wanaoendesha bodaboda na bajaji.

 

Ukubwa wa tatizo la ukosefu wa ajira nchini hauhitaji takwimu kuutambua. Kwa kutazama tu, tatizo linaonekana. Ukiwaangalia vijana waliotapakaa mitaani na kando ya barabara wakiuza sidiria, njiti za meno, leso, wanasesere, jojo, visu, manati, na kadhalika; huwezi kuwa na sababu ya kutafuta takwimu za ukosefu wa ajira nchini.

 

Kama yupo anayetaka kujua upana wa tatizo hili (mfano kwa Dar es Salaam pekee) apite Manzese, Kwa Mtogole, Tandika, Ubungo Darajani, Msasani, Mwananyamala, Jangwani, na kwingineko. Huko atapambana na kabari za mbao, visu, bisibisi, rungu na kila aina ya silaha. Uporaji unafanywa hadharani bila kujali ni muda gani na nani anayekabwa. Hii ni hatari kubwa.

 

Suala la ajira lilitazamwa kwa jicho pana na Serikali mwanzoni mwa miaka ya 1960 na 1970. Zilikuwapo juhudi kubwa za kupanua ajira kwa wakati huo.

 

Elimu ya kujitegemea haikulenga jambo jingine, isipokuwa kutengeneza ajira nyingi kwa vijana kwa kuwabadili kifikra. Kuanzishwa kwa viwanda na mashirika ya umma kulilenga kupunguza tatizo hilo. Tutakumbuka kwamba hadi Awamu ya Kwanza inamaliza ngwe yake ya uongozi, Tanzania huru ilikuwa na mashirika ya umma na viwanda zaidi ya 400. Mashirika hayo yalitoa ajira kwa maelfu ya Watanzania.

 

Mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani vilichangia kufa kwa mashirika yetu. Viongozi wasio weledi na wanafiki wakashiriki kuyaua na hatimaye kuyauza kwa bei chee. Tuliamua kuyakubali masharti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) na ya Benki ya Dunia, ya kubinafsisha na kupunguza wafanyakazi. Miaka karibu 30 sasa baada ya kuridhia sera za wakubwa hao, hali inazidi kuwa mbaya.

 

Ni laana kwa Tanzania kuwakuta watu tukilia ukosefu wa ajira. Hii ni laana na kwa kweli Mwenyezi Mungu anastahili kutuadhibu. Tunazidi kuwaabudu wafadhili na wezi wageni tuliowapa jina zuri la “wawekezaji” ilhali ni “waporaji”. Tunapandisha kodi kwenye soda huku waporaji wakifutiwa au wakipewa misamaha mikubwa ya kodi. Watalii wanaokuja kutumbua maisha, wanaondolewa VAT, huku makabwela wakipozwa kwa kushushiwa asilimia moja kwenye kodi ya “Lipa Kadiri Unavyopata (PAYE)”.

 

Nchi yenye ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha kila zao linalostawi duniani, nchi yenye maziwa makubwa – Tanganyika, Victoria, Rukwa, Nyasa, Eyasi, Manyara, Natron na mengine mengi, nchi yenye bahari yenye urefu wa kilometa 1,000; nchi yenye madini ya kila aina yakiwamo yasiyopatikana kwingineko duniani; nchi yenye hifadhi za taifa zaidi ya 10; nchi yenye vivutio vya utalii visivyopatikana kwingineko Afrika; nchi yenye gesi na madini ya thamani kama urani; nchi yenye vyote hivyo inawezaje leo kuwahimiza vijana kutafuta maisha kwa kuhangaika na bodaboda? Si bure, kuna laana hapa. Haiwezikani.

 

Matokeo yake sasa Tanzania imefanywa kuwa shamba la bibi. Wageni wa kila aina wanaingia na kupewa uraia. Wanachuma mali na kuzipeleka kwao kadiri wanavyotaka. Ni Tanzania pekee ambayo mtu anaweza kuingia dukani akabadili fedha bila hata kuulizwa amezipata, au anazipeleka wapi! Ndiyo nchi ambayo husikii wanaokamatwa na nyara za Serikali wakifungwa!

 

Tufanye nini? Tatizo la ajira linaweza kupunguzwa endapo tutaamua kubadili mfumo wetu wa elimu na maisha yetu. Elimu yetu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu ni lazima iwaandae watoto kupenda kujiajiri. Ninaposema ajira, si za bodaboda! Ajira za kilimo na kwenye madini ndiyo mkombozi.

 

Tuwakatae viongozi na wataalamu wetu wa uchumi wanaotaka kutuaminisha kuwa vijana wetu kuacha shughuli za kilimo na kuwapofusha kwa mikopo ya bodaboda, ni ukombozi wao na kwa Taifa. Fedha za bodaboda haziwezi kujenga shule. Haziwezi kumfanya anayeendesha asomeshe watoto wake kwa kiwango cha dunia ya leo.

 

Wasomi wanaotoka vyuoni wakiwa na elimu ya kilimo na ufugaji, waipende kazi hiyo na Serikali ijielekeze kwao kwa kuwaandalia mikopo na uwezeshwaji mwingine. Misri ya Mubarak walikuwa na sera hiyo. Tujifunze kutoka kwao.

 

Waziri, mbunge au yeyote awaye anapoamua kuwapa vijana pikipiki hana nia ya dhati ya kuwasaidia. Pikipiki haziwezi kuondoa umasikini. Zinaondoa njaa tu ya leo. Pikipiki ziwe ni matokeo ya maendeleo. Huu ni ulimbo wa kuwanasa vijana kwa ajili ya maslahi ya kisiasa.

 

Ajira inatengenezwa kwa kuwakopesha vijana zana, mashamba, pembejeo, masoko, elimu ya ujasiriamali na mitaji. Kama vijana wakulima wakichimbiwa mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji wa mbogamboga, na kama watakuwa na miundombinu ya kufikisha kwenye masoko hicho wanacholima, ni wazi kuwa Tanzania itasonga mbele kimaendeleo.

 

Mwalimu alisema kuwa ili tuweze kuendelea tunahitaji watu, ardhi, siasa Safi na uongozi bora. Je, katika haya manne, tumekosa lipi? Bila shaka hili la mwisho ndilo linalotusumbua.