Wiki iliyopita nilisikia malumbano kati ya Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, na wabunge wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania. Wabunge kutoka Tanzania wakiongozwa na Shy-Rose Bhanji wanasema Serikali kupitia wizara hiyo haiwapi mwongozo wa nini wanapaswa kufanya.

Baada ya kauli hiyo ya Shyrose, Sitta ameibuka kama mbogo aliyejeruhiwa na kuwashambulia vilivyo wabunge hawa. Akasema wakiwaita kwenye vikao hawaendi na wengi ni wafanyabiashara wenye kudai posho. Baada ya kauli hizi za kupishana nimeamua kuchimba ukweli wa mambo.

 

Sitanii, niliyobaini ni aibu tupu. Miezi 10 tangu wabunge wa Afrika Mashariki wachaguliwe, wamekutana na wizara mara moja tu katika semina elekezi. Januari mwaka huu, pia walikutana kama zali huko Bujumbura. Wizara haiwapi mwongozo wa masilahi ya Tanzania EAC ni yapi.

 

Tangu wachaguliwe hawana ofisini. Wanahudhuria vikao vya Bunge na wakimaliza wanakaa nyumbani kwao. Hawana vitendea kazi, wasaidizi na wizara haijawakutanisha na wadau katika wizara nyingine kujadili masilahi ya Tanzania katika bunge hilo.

 

Wabunge hawa wanahitaji msaada wa watafiti kutoka wizara nyingine. Kwa kuwa hawana ofisi, kwa sasa kila mmoja anazungumza kinachoingia kichwani mwake. Ndiyo maana mbunge mmoja kati ya waliomaliza muda aliwasilisha muswada wenye kukinzana na masilahi ya Tanzania juu ya mipaka na mazingira. Hadi leo Rais Jakaya Kikwete amekataa kusaini muswada huo uwe sheria.

 

Wabunge wa nchi nyingine kama Uganda wamepewa ofisi, mikopo ya magari, lakini kwa Tanzania huu ni mwezi wa 10 hakuna kitu. Semina waliyofanyiwa waliambiwa wangekuwa na masilahi kama wabunge wa Jamhuri ya Muungano, lakini leo kuna baadhi wanaomba hadi chumvi. Wako hoi.

 

Sitanii, hatari inayolikabili taifa letu ni kwamba kila mbunge wa EAC anatoka nyumbani kwake, anaingia ukumbi wa bunge na kuwasilisha mwazo yake – si ya nchi. Shy-Rose alitaka wizara iweke mipango, uwepo ushirikiano na maelekezo ya Tanzania kwa wabunge hawa, jambo ambalo halipo.

 

Mawaziri tuliowatuma huko ndiyo usiseme. Inaelezwa kuwa Naibu Waziri, Dk. Abdulla Juma Abdulla, kazi anayoifanya anaijua yeye. Sitamjadili huyu, maana hajajiingiza kwenye malumbano. Sitta anatajwa kuwa asilimia 95 ya muda wa vikao anayo kazi moja tu; kusinzia.

 

Hoja ya Sitta kwamba wabunge wanadai posho, ni kichekesho. Alipowaalika bungeni Dodoma, wizara haikuwapa posho, wala kuwalipia usafiri. Lakini ajabu, Mwenyekiti wa wabunge hao, Alhaj Adam Kimbisa, yeye inaelezwa aligharamiwa na wizara.


“Mimi namheshimu [Sitta] kama mzazi wangu na kama kiongozi, lakini anakuja kusema uongo? Amenisikitisha sana. [Rais wa Kenya Mwai] Kibaki anakuja nchini [wabunge wa EALA] tunasoma kwenye media. Katibu Mkuu wa EAC anakuja nchini tunasoma kwenye media. Hatupewi taarifa,” amesema Shy-Rose.


Sitanii, Jumuiya ya Afrika Mashariki ya sasa haipo kwenye mioyo ya Watanzania. Kabla ya mwaka 1977, kila mwananchi alikuwa na fursa ya kufanya biashara. Kwa sasa wafanyabiashara ni wale wale na pato linakua kwa wachache kwenye Jumuiya bila kuwaeleza wananchi fursa zilizopo.


Enzi hizo zilikuwapo taasisi zinazowaonesha wananchi uhai wa Jumuiya. Lilikuwapo Shirika la Posta na Simu, Reli ya Afrika Mashariki, Shirika la Ndege la Afrika Mashariki na mambo mengine mengi yanayoonesha uhai wa Jumuiya hii kwa macho ya wananchi. Siku hizi tunasikia siasa tu.

 

Hatari kubwa ninayoinusa ni kwamba Sitta anatuchezesha makidamakida Afrika Mashariki na wenzetu watatuacha solemba. Pengine anadhani EAC nako kuna siasa za urais, na hivyo ameamua kuendesha kampeni za majitaka.


Kitendo cha wabunge wetu kila mmoja kutokea nyumbani kwake kwenda kutuwakilisha bila kukutana na kupewa mwongozo hakikubaliki. Serikali yetu sikivu iufanyie kazi mvutano huu.

1085 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!