Muda mfupi baada ya Wema Sepetu kutangaza kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM), chama hicho kimesema hakina taarifa rasmi kuhusu Wema kutaka kurudi.

Hayo yamesema na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ambapo kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika kuwa, katika kujenga nidhamu ya chama, na kuepuka kukifanya chama daladala kwamba unapanda na kushuka wakati unaotaka, kuna taratibu za kufuatwa mtu anapotaka kujiunga na chama, na sio kutangaza mitandaoni.

“Nimesikia habari mitandaoni, napenda kuweka rekodi sawa, chama chetu sio daladala ambayo mtu anaweza panda na kushuka wakati wote apendao. Chama chetu kina misingi, imani, masharti ya uanachama, na zaidi ya yote ahadi ya mwanachama ambayo ni moja inasema, Nitakuwa Mwananchama mwaminifu wa CCM.”

Aidha, Polepole amesema kwamba, ni heri Wema Sepetu akabaki huko huko (CHADEMA) ama akaanzie kwenye shina la chama ambapo ndipo alipochukulia kadi kabla ya kuhama.

“…kukosa uaminifu kwa chama inatosha kumkataa mtu kuwa mwanachama wetu,” aliandika Polepole akisema kwamba katika kuijenga CCM mpya sio kazi ndogo na kwamba inahitaji viongozi wanyenyekevu na watumishi na wanachama waaminifu.

Mapema jana jioni, Wema Sepetu alitangaza kujiengua CHADEMA na kurejea CCM akidai kuwa, hawezi kuendelea kuishi kwenye nyumba inayomkosesha amani, kwani kwake yeye utulivu wa akili ni kila kitu.

Baada ya Polepole kuandika hayo kwenye ukurasa wake wa Instagram, Steve Nyerere kwa upande wake amemtolea povu Polepole akimtaka kutoleta ubinafsi kwenye chama kwa kumkatisha moyo Wema aliyeonesha nia ya kurejea kwenye chama chake cha zamani (CCM)

“Hiki chama hujakiunda wewe wala kukianzisha wewe, umekikuta kama tulivyokikuta wote, kina waasisi wenye uchungu nacho na wako kimya, wewe ni nani ukatishe watu moyo kukitumikia kama vile ndio unakimiliki, tulia polepole chama cha wote hiki.”

Steve Nyerere alimwambia Polepole kuwa, katika kujenga nyumba, hauwachukui wale tu wenye nondo na saruji pekee, bali pia wenye mawe wanatakiwa kushirikia, lengo likiwa ni kukamilisha nyumba.

 

NINI MAONI YAKO NA WEWE?

By Jamhuri