Waziri-Mkuu-Mstaafu Fredrick-SumayeMkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sincon, Peter Siniga amemwandia barua Rais Dk. John Magufuli akimtaka kuingilia kati sakata la dhuluma dhidi yake iliyodaiwa kusukwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Barua yenye Kumb. Na. SN/PRE/2015/11/01 kwenda kwa Rais Dk. Magufuli iliyoandikwa na kusainiwa na Siniga, Novemba 26, 2015 inazungumza dhuluma katika biashara ya ubinafsishaji wa Shirika la vyuma-National Steel Corporation (NSC).

Siniga anasema ameonewa na kufanyiwa utapeli wa wazi, huku akitishiwa kuuawa na watu anaowaita wanahisa wenzake katika biashara hiyo.

“Dhumuni hasa la barua ni kutaka wewe binafsi kuweza kuingilia kati haki zangu za kumiliki kampuni iliyouzwa National Steel Corporation Limited [kuona] zinarejeshwa,” anasema Siniga.

Katika mahojiano na JAMHURI, huku akitoa vielelezo, Siniga anasema, “Jambo la kusikitisha [ni] kwamba aliyekuwa Waziri Mkuu Frederick Sumaye ameniruka ili kunidhulumu haki yangu.”

Anasema Sumaye na ndugu yake, John Fissoo walimshawishi kulipa fedha kunununua hisa za NSC, lakini kwa sasa wamemgeuka.

Anadai ushawishi wa Fissoo na Sumaye ulianzia mwaka 2011 ambako walikutana kwa faragha nyumbani kwa Sumaye Kiluvya-nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Aliambiwa NSC iliyoanzishwa mwaka 1966, ilikuwa katika mpango wa kubinafsishwa au kuuzwa mwaka 1996.

Majadiliano (fast track) yalifanyika serikalini baina ya mawaziri chini ya Sumaye Waziri Mkuu na kuamuliwa NSC iuzwe kwa wananchi na wafanyakazi.

Barua ya Sumaye ya Agosti 20, 1996 kwenda Ofisi ya Rais ilielekeza mpango wa kuwajumlisha watu wasio wafanyakazi wa shirika katika uwekezaji na inaelezwa kuwa Rais Benjamin Mkapa (wakati huo), alikubali azima ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa fursa kwa wazawa kumiliki uchumi.

JAMHURI limewasiliana na Sumaye ambaye, anasema: “Aah unamzungumzia mtu mmoja anaitwa Peter?… Huyu achana naye.” Akaongeza: “Huyo bwana kama anadhani mimi nimemsababishia matatizo akatafute haki mahakamani. Aende mahakamani. Ameshindwana na wenzake, naona anahangaika magazetini.

“Mimi nadhani mpe ushauri tu aende mahakamani. Maana amefika huko zaidi ya mara sita, na ameshindwa, nadhani aende tena. Mimi sina mpango naye, naona ni mfa maji,” anasema.

Siniga anawafahamu ni wafanyakazi wa zamani wa iliyokuwa NSC ambao ni Fissoo, Makika Kasuga, Ali Magwa, Jumanne Abdallah, Salum Mahingira, Eshi Kweka, Verynice Tesha, Richard Ndugai, Exavier Kaisi, Fatuma Makuka, Abdallah Mohammed na Said Mkonge kuwa ndio walikuwa wanahisa wenzake.

 

Wanahisa hao walikuwa na jumla ya hisa 60,000 kwani kila mmoja alikuwa na hisa 5,000 ambazo hata hivyo hazikulipiwa kwa mujibu wa Siniga.

Anasema wafanyakazi hao walianzisha Kampuni mpya ijulikanayo kama New National Steel 2000 iliyopata hati ya usajili Na. 39976; Septemba 12, 2000.

Pamoja na kuanzisha kampuni hiyo ili kuinunua NSC kupitia Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) wakati huo, lakini wanahisa hao walishindwa kupata fedha ya kununua hisa zote-asilimia 100.

Siniga anasema wakati huo alikuwa amepanga ofisi za NSC – ofisi alizokuwa nazo kuanzia Septemba 1, 1998 katika mkataba wa awali uliofikia Agosti 30, mwaka 2000.

Anasema akiwa hapo, Machi, 1999 viongozi na wafanyakazi hao walimuomba mkopo wa Sh milioni 27 kwa ajili ya kununua nondo na kufanya biashara kwa masharti baada ya kuuza, ndani ya miezi mitatu atalipwa msingi na asilimia 75 ya faida itakayopatikana na wao kubaki na asilimia 25.

“Lakini hadi leo hii (Machi 20, 2016) sijalipwa,” anasema Siniga na kutoa taarifa mpya kuwa baada ya wanahisa hao kukwama kurudisha mkopo wenye nyumba wakaibuka na hoja kwamba wamepewa nafasi ya kununua kampuni hiyo kupitia mpango wa Mebo-yaani Kampuni ya Wafanyakazi na Menejimenti.

“Hivyo wakati huo hawakuwa na fedha za kulipa kiasi cha Sh milioni 400, hivyo wakaomba tuungane kwa pamoja ili tuweze kununua hisa zote asilimia 100 kutoka serikalini na baada ya kuinunua tutagawana asilimia 50 kila upande,” anasema.

Anasema baada ya majadiliano marefu kati ya Serikali kupitia PSRC, Wizara ya Viwanda na Biashara  pamoja na Waziri Mkuu Sumaye ambaye alimwaminisha Siniga kuwa angepata hisa asilimia 50 na asiwe na wasiwasi.

Aliambiwa Sumaye amekwisha andika barua yenye Kumb. Na. 20/8/1996 kwenda kwa Rais Mkapa kwa wakati huo na kukubaliwa kupitia barua yenye Kumb. N. PMC/2/1/30/10 ya Machi 3, 1997 iliyobeba ujumbe wa sera ya CCM kuhakikisha wananchi wanamiliki uchumi.

Siniga anajinasibu kuwa ni mwanachama wa CCM mwenye kadi Na. A 716239 iliyotolewa Mei 14, 1977 kabla ya kupewa mpya Na. 382319 ya Machi 10, 2000, aliamini hiyo itakuwa nafasi kwake kuendeleza uchumi wake na nchi kupitia kodi.

Kadhalika Siniga anadai mbali ya fedha hizo kuna kiasi cha Sh milioni 105.9 alizozitoa baada ya wanahisa wenzake kumshawishi kufanya hivyo zitumike kama kiinua mgongo kulipa mafao kwa wafanyakazi ambao hawakutaka kubaki kwenye kampuni mpya ya NNSL. Wafanyakazi hao waliongozwa na Peter Inano.

“Lakini hadi leo hii Machi 20, 2016 siku nazungumza na JAMHURI, sijalipwa na hata baada ya kupeleka shauri Na. 64/2013 kesi hiyo ilitolewa uamuzi wa kutolipwa. Hii inatokana na rushwa kwa ushahidi wa maandishi uliotolewa mahakamani,” anasema na kuongeza:

“Hii ni kwa sababu ya unyonge, dhuluma na rushwa.”

Anasema katika gharama ya kununua kiwanda hicho, kwa upande wake alianza kulipa Sh milioni 40 ikiwa ni asilimia 10 ya ununuzi wa NSC kwa PSRC kupitia hundi ya benki Na. 01687 ya Januari 30, 2001. Anasema alifanya hivyo baada ya kupata barua yenye Kumb. Na. NNS/MD/1/2001 ya Januari 25, 2001 kutoka kwa Fissoo.

Mbali ya malipo hayo kwenda PSRC pia alilipa Sh milioni 34 kupitia hundi Na. 000171105 ya Novemba 29, 2002; kisha akalipa Sh milioni 24 kupitia hundi Na. 009139 ya Desemba 04, 2002 na malipo ya mwisho aliyafanya ni Sh milioni mbili.

Mchanganuo huo unafanya Siniga kuwa amelipa jumla ya Sh milioni 100, lakini baada ya hapo anasema Fissoo na Mhasibu Mkuu Makika Masuga walitoa na kusaini hati ya hisa 500,000 (share certificate) Na. 0013, Februari 12, 2004 na kusajiliwa Brela baada ya wanahisa wote kuridhia.

Fedha hizo Sh milioni 100 ndizo zilizolipwa kama malipo ya awali kwa PSRC mkataba ukasainiwa na pande zote mbili-serikali na NNSC.

Kwa upande wake, Fissoo anasema: “Hili jambo sasa lipo kisheria zaidi na uamuzi wa kimahakama na Siniga aseme ukweli. Wakati analalamika na kutaja kesi mbili au tatu, ataje kwanza kesi ya kwanza na ya msingi. Huyu bwana kabla hatujamaliza deni PSRC, alikiuka mkataba.

“Kwanza nadhani kuna watu walimdanganya. Eti anaweza kuuza kiwanda cha Serikali kabla hajamalizana na Serikali. Hilo lilishindikana na sisi tukaamua kwenda kortini kuzuia mipango yake.

“Mahakama iliamua kumuondoa kabisa kwenye hisa. Na ndiyo maana sisi tunasimamia kwenye uamuzi wa mahakama. Lakini alipoondolewa kwenye hisa, hakukataa rufaa. Nini maana yake. Maana yake ni kwamba aliridhia uamuzi wa mahakama.

“Kesi zote ameshindwa na kama anadhani ana haki, aende kortini tena,” anasema Fissoo aliyezungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki.

By Jamhuri