*Muhtasari wa kikao wachakachuliwa, jina la Dk. Nagu laingizwa

Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Hanang’ mkoani  Manyara, kinakabiliwa na mpasuko unaosababishwa na uhasama ulioibuka kati ya Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye.

Wachunguzi wa mambo wanaona msuguano kati ya miamba hiyo miwili ni maandalizi ya kujiimarisha kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Wakati Sumaye bado hajaweka bayana nia yake ya kuwania urais mwaka huo, kuna habari kwamba Dk. Nagu naye anajiandaa kuhakikisha anawania kiti hicho.

 

Lakini wengine wanasema anachokifanya sasa mwanamke huyo wa kwanza nchini kuongoza shirika la umma, ni kumwandalia mazingira mmoja wa wanachama wanaotajwa kuutaka urais mwa udi na uvumba mwaka 2015. Vikumbo vya uvunjifu wa maadili ya uchaguzi vimetawala katika uchaguzi wa nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Wilaya ya Hanang’. Nafasi hiyo ilikuwa na wagombea watano, wakiwamo Sumaye.

 

Kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Hanang’ kilifanyika Septemba 2, mwaka huu chini ya Katibu wa CCM wilaya ya Hanang’, Allan Kingazi, kwa sababu Mwenyekiti Goma Gwaltu, anatetea nafasi yake kwa hiyo kikanuni haruhusiwi kuendesha kikao. Jina la Dk. Nagu lilienguliwa kutokana na kile kinachoelezwa kutokuwa na sifa kama kanuni za chama hicho zinavyoelekeza.

 

Baada ya kupitia majina ya wanachama hao watano, wajumbe walifanya mchujo na kubakiza majina ya wajumbe wawili – Sumaye na Leonsi Marmo. Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, kikanuni jina au majina ya waliopitishwa hupaswa kupelekwa ngazi ya mkoa yakiwa pamoja na muhtasari wa kikao kilichopitisha. Kamati ya Siasa ya Mkoa huyapitia kabla ya kuyapeleka katika ngazi ya Taifa.

 

Hata hivyo, kwa Hanang’ mambo yamekwenda tofauti. Kabla Kamati ya Siasa ya Mkoa haijaanza kupitia majina hayo, taarifa kutoka ndani ya ofisi ya Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang’ zinasema kuwa Katibu huyo alibadilisha muhtasari uliotoka kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya. Muhtasari huo ambao nakala yake inaelezwa kuhifadhiwa katika ofisi ya Ofisa Usalama Wilaya ya Hanang’ (DSO), Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang’, Kingazi, anadaiwa kuingiza jina la Dk. Nagu kama mmoja wa wagombea waliopitishwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya.

 

Kuna habari kwamba Kingazi alibadili muhtasari kutokana na shinikizo zito lililoambatana na ushawishi. Akatakiwa pia ahakikishe “salamu” hizo anazifikisha kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Nden’gaso Ndekubali. Baada ya kuvuja kwa taarifa hizo, Dk. Nagu amejitokeza kukanusha kuendesha njama za kubadili muhtasari, akisema kwamba kilichopo ni uamuzi wa Kamati ya Siasa ya Wilaya.

 

Wajumbe 12 kati ya 15 wa Kamati ya Siasa ya Wilaya walihudhuria kikao kilichomwengua Dk. Nagu. Baadhi ya wajumbe wanasema ilikuwa kazi ngumu kweli kweli kuliondoa jina la Dk. Nagu, hasa kutokana na utetezi mkubwa alioupata kutoka kwa Kingazi.

 

“Tulipokuwa tukijadili majina ya wagombea, wengi wetu tulionekana kukubali kuondolewa kwa jina la Dk. Nagu, lakini Katibu alionekana kumtetea na hata kudai kuwa amepokea barua kutoka kwa Katibu wa CCM Taifa, Wilson Mukama, ikimuagiza mgombea huyo apitishwe kwa kuwa alikuwa akitayarishwa kwa ajili ya nafasi ya urais,” anasema mmoja wa wajumbe hao.

 

Anasema baada ya malumbano makali, wajumbe walitakiwa kupiga kura za siri. Wajumbe saba walipiga kura ya kumwondoa Dk. Nagu, huku wajumbe watano wakitaka jina lake lipitishwe.

“Muhtasari huu ulioghushiwa ambao sisi hatukuujadili umeonesha jina la Dk. Nagu kama mmoja wa wajumbe waliopendekezwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya, na unaonesha kinyume, yaani kura tano zilimkataa huku kura saba zikimpitisha, jambo ambalo si la kweli,” anasema mjumbe huyo.

 

Kwa upande wake, Kingazi anakanusha taarifa za kubadili muhtasari akisema taarifa za Kamati ya Siasa ni siri, na kwamba mjumbe anayetoa taarifa za aina hiyo anavunja maadili. Anasema taarifa za waliopitishwa kugombea nafasi ya NEC zitatolewa baada ya Kamati ya Siasa ya Mkoa kupitia majina yaliyopendekezwa. Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndekubali, hakatai wala hakubali madai ya kuwapo mchezo mchafu.

 

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Mukama alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kujibu madai kwamba amewataka wajumbe wapitishe jina la Dk. Nagu,  alijibu kwa kifupi, “Sihusiki na lolote linalotokea au kuendelea kutokea Hanang’.”

 

Dk. Nagu alipotumiwa ujumbe wa maandishi ili aeleze sakata hili linalomhusu, hakujibu. Matumizi ya fedha katika uchaguzi huu yamekuwa makubwa mno kiasi cha kuibua mjadala miongoni mwa wana CCM.  Juhudi za Dk. Nagu kuwania nafasi hiyo zimekuwa pia zikihusishwa na mpango wake wa kusimamia mgawo wa mkopo wa matrekta kwa wakulima wilayani Hanang’.

 

“Alianza kujipanga mapema lakini inawezekana watu walimshtukia. Alianza kugawa matreka ya mkopo na alionekana wazi kuwasaidia baadhi ya wanachama wa CCM wakiwamo viongozi kukopeshwa matrekta,” amesema mwanachama mwingine wa CCM.

 

Katibu wa Uenezi CCM Taifa,  Nape Nnauye, anakiri kusikia taarifa za kuenguliwa kwa Dk. Nagu, lakini hata hivyo anasema taarifa zaidi atazipata baada ya kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa. Anasema CCM haiwezi kufanyia kazi taarifa za rushwa kupitia vyombo vya habari, na kutoa wito kwa watu wenye uhakika wa matukio ya rushwa katika kampeni wazifikishe kwenye vyombo vinavyohusika.

 

“Napokea taarifa nyingi za kuwapo kwa suala la rushwa, hata hizo za Hanang’ pia tumezisikia, lakini hatuwezi kufanyia kazi kila taarifa, endapo mtu ana ukweli atufikishie hizo taarifa na sisi tutachunguza na ikibainika ukweli tutachukua hatua kali,” anasema.

 

Ushauri wangu kwa viongozi wa juu ndani ya CCM ni kuteua timu maalumu ya kufuatilia madai ya rushwa ambayo yamekuwa yakitolewa sehemu mbalimbali. Mfano mzuri ni suala la ufisadi ambalo limekuwa likishika kasi kila kukicha nchini.

 

Hili ni jambo ambalo awali lilionekana dogo, lakini kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo sasa matokeo yake yanavyozidi kuonekana. Ni wazi kwamba kama wagombea wenyewe ndiyo watoa rushwa, kamwe hawataweza kupambana na mfumo wa rushwa unaojengeka kwa kasi kubwa katika jamii.

 

[email protected]

By Jamhuri