246_manyanyaVigogo wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wamedaiwa kutengeneza vitabu bandia vya kukusanyia mapato ya ushuru na leseni za  uvuvi kwa wafanyabiashara wa samaki katika Ziwa Rukwa, JAMHURI inaripoti.
 Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba vitabu hivyo vimetengenezwa na baadhi ya wakuu wa idara ndani ya manispaa hiyo, kwa lengo kujiingizia mapato yanayokadiriwa kufikia zaidi ya Sh. milioni 100 ambazo hazifikishwi ndani ya manispaa husika wala Wilaya ya Sumbawanga ambako fedha hizo zinakusanywa.
Wavuvi na wafanyabiashara ya samaki katika Ziwa Rukwa wameeleza kusikitishwa na vitendo hivyo vilivyodumu kwa muda mrefu, vya kupewa stakabadhi hizo ‘feki’ kutoka manispaa wakati wao wako halmashauri.


 Wanasema hata kwa upande wa leseni za uvuvi vitabu vya stakabadhi za malipo vimechanganywa, wanapewa vya Manispaa ya Sumbawanga na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, jambo linaloonesha wazi mapato yanayokusanywa yanaingia katika mifuko ya wajanja wachache.
  Mfanyabiashara mmoja wa samaki kutoka kambi ya wavuvi ya Nankanga (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama), anasema matumizi ya vitabu bandia yamekithiri katika maeneo ya uvuvi ziwani humo.
  Anasema ni mradi haramu wa wakuu wa idara wa halmashauri hiyo akiwamo Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Dennis Maghalla, Ofisa Uvuvi wa Wilaya, Kulwa Lukuba, na Mhasibu wa Mapato wa Wilaya, Thobias Shija.
Anasema mapato yote yanayokusanywa kwa kutumia stakabadhi za Manispaa ya Sumbawanga hayapelekwi huko na badala yake yanaingia katika mifuko ya watendaji hao wanaodaiwa kumiliki vitabu vyao vya kukusanyia mapato.
 “Hili jambo ni la muda mrefu sana na mwaka 2014 liliwekwa wazi kwamba kwa nini halmashauri itumie vitabu vya manispaa kukusanya ushuru kwenye maeneo yasiyowahusu? Hakuna majibu yanayoeleweka yaliyotolewa na wahusika zaidi ya kuendeleza ubabe huu wa kutuibia,” anasema.
  Chanzo chetu kingine kimeeleza kwamba kwa muda wa wiki mbili tu vitabu feki vinatumika kukusanya zaidi ya Sh. milioni 100 ambazo haziingii katika Manispaa ya Sumbawanga.


 Chanzo hicho kinaongeza kwamba tuhuma hizo ziliibuliwa katika vyombo vya habari kwamba halmashauri inatumia vitabu vya manispaa kukusanya ushuru na leseni za uvuvi, lakini bado utaratibu huo unaendelea na wahusika kama wako ndani ya nchi nyingine si Tanzania.
“Huu ni wizi wa aina yake ambao umeendelea kwa muda mrefu sana ukiwahusu baadhi ya watendaji wa manispaa na halmashauri hiyo na baadhi ya maofisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wanaodaiwa kupelekewa sehemu ya mapato hayo ambayo hayaingii serikalini,” kimeeleza chanzo hicho.
Imeelezwa kuwa wahusika wa wizi huo wamejiwekea himaya yao kiasi kwamba hawawezi kuguswa kwa namna yoyote ile; na watu wanaothubutu kuhoji wanajiweka katika wakati mgumu katika kazi zao ama biashara zao.
 
Idara ya Mifugo na Uvuvi
JAMHURI imezungumza na Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Dennis Maghalla, kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwake kuhusu matumizi ya vitabu ‘feki’ vya malipo ya ushuru na leseni za uvuvi wilayani Sumbawanga, lakini amekana kwamba hahusiki navyo.
Maghalla amedaiwa kuwa miongoni mwa maofisa wa wilaya hiyo wanaotumia vitabu bandia kukusanyia ushuru na malipo ya leseni za uvuvi, huku mapato hayo yakiishia katika mifuko ya wajanja wachache badala ya kuingia serikalini.
  Maghalla anasema suala la vitabu hivyo lilikuwapo na taarifa zilitolewa katika vyombo vya habari na hatua iliyofuata ni kuondolewa kwa vitabu hivyo katika matumizi ya kukusanyia mapato yatokanayo na uvuvi katika Ziwa Rukwa.
 “Hili suala la kuchanganya vitabu vya manispaa na halmashauri ya wilaya kukusanya mapato ya uvuvi lilishapatiwa ufumbuzi, labda kama kuna baadhi vilibaki na anayeweza kulielezea hilo ni mweka hazina wa halmashauri au msaidizi wake,” anaeleza Maghalla.
 
Mweka Hazina
Naye Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Credo Nduhie, alipotafutwa kuelezea suala hilo hakupatikana. Hata hivyo, gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na mhasibu wa mapato ambaye ndiye mhusika mkuu kwa upande wa mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi katika ziwa hilo, Thobias Shija, aliyejibu kwa ukali, “Mimi siyo msemaji wa halmashauri, mtafute DED.”
Hata alipoulizwa kwamba yeye anadaiwa ni miongoni mwa watu hao walioamua kutengeneza vitabu hivyo kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi badala ya mapato hayo kuingia serikalini, hakutaka kuzungumza chochote.
 
Ofisa Uvuvi
Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Sumbawanga, Kulwa Lukubi, alipohojiwa kuhusu tuhuma hizo za kutumia vitabu vya stakabadhi vya Manispaa ya Sumbawanga kukusanyia ushuru wa uvuvi na ununuzi wa samaki kutoka Ziwa Rukwa wilaya humo, amesema hiyo siyo sheria na wala hairuhusiwi.
Wakati akiieleza JAMHURI kuhusu kutokuwapo kwa vitabu hivyo feki, Lukubi amesaini moja ya risiti hizo ambazo zinadaiwa kuwa zinatoka katika vitabu hivyo vinavyotumika kuiibia mapato halmashauri ya wilaya hiyo.
 “Labda kama kuna baadhi ya watu wameamua kuingiza vitabu hivyo kwa lengo la kuiibia mapato halmashauri, tunafuatilia suala hilo ili tufahamu kinachofanyika,” anasema Lukubi.
 
Mkurugenzi Mtendaji
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Adamu Missana, amekana kuhusika na vitabu hivyo feki vya mapato, ambayo huishia kunufaisha mifuko ya wajanja wachache badala kuingia serikalini.
 “Mimi sielewi, silifahamu suala hilo, niache nilifanyie kazi, nasema sihusiki na vitabu hivyo,” anasema Missana.
 Lakini alipotakiwa kufafanua taarifa za kuwapo vitabu hivyo feki vya Manispaa ya Sumbawanga na Halmashauri ya Wilaya kwa matumizi ya kukusanyia ushuru na leseni za uvuvi wa samaki, hakutaka kueleza chochote huku akitaka apatiwe maeneo wanakotoka walalamikaji hao.
 
Manispaa ya Sumbawanga
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu, alihojiwa na JAMHURI kuhusu vitabu vya kukusanyia mapato vya manispaa hiyo kutumika kukusanyia mapato ya ushuru wa samaki na leseni za uvuvi halmashauri, aliishia kumtishia mwandishi wa habari.
 “Hakuna kitu kama hicho, nasema hakuna, wewe andika tu tutaonana mahakamani,” anasema Njovu ambaye pia ni Mweka Hazina wa Manispaa ya Sumbawanga.
 Matumizi ya vitabu vya kukusanyia mapato vya Manispaa ya Sumbawanga kutumika na halmashauri ya wilaya, yanadaiwa kushika kasi kuanzia Desemba 2014 baada ya kujitokeza vurugu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na baadhi ya wasimamizi kuchukuliwa hatua kwa kusimamishwa kazi akiwamo Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Shimwela.
Katika kipindi hicho, Njovu amekuwa akikaimu nafasi hiyo. Hata hivyo, chanzo chetu cha habari kimesema kwamba mchezo huo wa kuiibia Serikali mapato, umeendelea kujitokeza mara kwa mara huku vitabu vya halmashauri vikichanganywa na kupelekwa katika maeneo mengine na lengo kubwa likiwa ni wizi unaofanywa na baadhi ya wakuu wa idara waliokosa uaminifu.

 

By Jamhuri