Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amelieleza Bunge kuwa, kuna hazina ya kutosha ya mafuta ghafi ya kula.

Kwa mujibu wa Waziri Mwijage, kwenye hifadhi ya matenki ya mafuta ghafi ya kula jijini Dar es Salaam kuna mafuta ya mawese takribani tani 40,000.

Amesema, meli zilizoegeshwa nje ya bandari ya Dar es Salaam zina mafuta ghafi ya mawese takribani tani 50,000.

Mwijage amewaeleza wabunge kuwa, kwa kuzingatia kiwango kilichopo kwenye hifadhi na yaliyopo kwenye meli kuna mafuta ghafi tani 90,000.

“Kinacholeta tatizo ni kutokubaliana katika viwango vya kodi” amesema.

Ametoa ufafanuzi huo baada ya Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia kutaka kauli ya serikali kuhusu uweli wa taarifa za kwenye vyombo habari kuhusiana na mafuta ya kula.

Waziri Mwijage amesema, kwa mujibu wa sheria, muagizaji wa mafuta kutoka nje anatozwa kodi asilimia 10 lakini vipimo vinamuoesha Kamishna wa Forodha kwamba mafuta hayo ni ghafi na si yaliyosafishwa hivyo anayachukulia ni mafuta safi na kutoza kodi asilimia 25.

Amesema, Serikali inalifanyia kazi jambo hilo na wataalamu wake watatoa majibu kati ya leo kesho kwamba ni mafuta ghafi au yamesafishwa ili kufahamu yatozwe kodi kiasi gani.

Awali Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba alilieleza Bunge kuwa, Serikali inalifanyia kazi suala la mafuta ya kula ili wananchi wasiyakose au yasipande bei sana.

Amesema, Serikali inaruhusu mafuta ghafi kutoka nje ili kukidhi mahitaji ya walaji kwa kuwa kiwango kinachozalishwa nchini hakitoshi.

By Jamhuri