Ugonjwa wa moyo umeendelea kuwa tishio nchini, licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wa afya kutoa elimu kwa wananchi  juu  ya  namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ni miongoni mwa taasisi ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na ugonjwa huo ili kuupunguza kama siyo kuumaliza kabisa.
Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, ameliamia JAMHURI uwepo wa taasisi hiyo iliyoanzishwa Septemba 2015 imepiga hatua kubwa kwa kuokoa maisha ya watu wengi.
Prof. Janabi amesema licha ya jitihada zinazofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kujaribu kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo, lakini bado watu zaidi ya milioni 12 wamekuwa wakipoteza maisha kila mwaka.
“Ugonjwa huu umekuwa ukiongezeka kila mwaka kutokana na aina ya vyakula vinavyotumika katika jamii zetu,” amesema Janabi.
Amesema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo takribani miaka miwili sasa, wamefaulu kufanya upasuaji wa aina nyingi kwa wananchi ambao wangelazimika kwenda kutibiwa nje ya nchi.

“Katika miaka michache ya uwepo wetu nchini tumekuwa karibu na Serikali ya Israel kupitia mpango wake wa Save a Child’s Heart (Okoa moyo wa mtoto) ushirikiano na nchi hiyo imetusaidia kubadilishana utaalamu na vifaa,” amesema Janabi.
Amesema taasisi nyingine wanazoshirikiana nazo ni Open Heart international ya Australia, Mending Kids Heart ya California, Madaktari Africa ya South Carolina, Almutada ya Saudi Arabia, Sharjah International ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Madras Medical Mission and BLK ya nchini India.
Amesema ushirikiano huo mzuri na taasisi hizo za kimataifa umewawezesha madaktari katika taasisi ya JKCI kufanya upasuaji kwa mafanikio na hivyo kuwasaidia watu ambao wangetakiwa kwenda India kutibiwa.

“Ushirikiano huo umetuwezesha kufanya ‘operation’ nyingi zikiwamo za kuhamisha mishipa kutoka sehemu yoyote ya mwili na kuhamishia kwenye moyo,” amesema.
Amesema shinikizo la damu liko katika kiwango cha juu zaidi duniani, na kuathiri karibu nusu ya watu wazima barani Afrika, hali hiyo inatokana na ulaji wa vyakula visivyokuwa na manufaa mwilini.
Ripoti ya WHO ya Desemba 2016 inaonesha kuwa ugonjwa wa shinikizo la damu ndiyo ugonjwa  unaoathiri watu wengi duniani ambapo katika Bara la Afrika asilimia zaidi ya 10 ya Waafrika wameshapata ugonjwa huo.
Prof. Janabi ameliambia JAMHURI, sababu za kuongezeka ugonjwa huo ni watu kutopenda kufanya mazoezi, matumizi ya tumbaku, sigara, pombe na ulaji wa vyakula usiozingatia ushauri wa kidaktari.

Ugonjwa huo pia unawapata watoto wadogo ambapo inakadiriwa kuwa kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa kila siku duniani, wanane miongoni mwao wanazaliwa wakiwa na ugonjwa wa moyo.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazojitahidi kudhibiti na kupambana na ugonjwa wa moyo ambao ni miongoni mwa magonjwa tishio kwa watoto wadogo,” amesema Janabi.
Naye Dk. Tulizo Shemu amesema wagonjwa 100 kati ya 1,000 wanaofika kupata huduma katika taasisi hiyo hulazwa kila wiki, hali ambayo imesaidia kupungua kwa vifo vinavyotokana maradhi ya moyo kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Amesema mwaka huu taasisi  imefanikiwa kuongeza idadi ya wagonjwa wanaohudhuria kliniki ya wagonjwa wa nje kutoka 100 na kufikia 200, hatua inayotokana na mwamko wa wananchi kuhusu ugonjwa wa moyo.

“Tumepunguza vifo vitokanavyo na maradhi ya moyo kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari ili kuwafanya wananchi kuyafahamu magonjwa ya moyo na jinsi wanavyoweza kuyaepuka na kukabiliana nayo,” amesema Shemu.
Amesema kuanzia mwaka 2016 taasisi imefanya uchunguzi wa tiba kwa wagonjwa 973, kati yao wagonjwa 620 walipatiwa matibabu ya moyo bila kufungua kifua na wagonjwa 353 walipatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua.
“Miaka ya nyuma upasuaji wa magonjwa ya kufungua kifua bila kufungua kifua ulifanyika nje ya nchi na kusababisha Serikali kutumia fedha nyingi kuwapeleka wagonjwa nchini India kutibiwa kwa kutumia gharama kubwa,” amesema Shemu.
Dk. Shemu amesema mwaka 2016 taasisi imefanikiwa  kuokoa zaidi ya Sh milioni 2.6 kwa wagonjwa kwani kila mgonjwa mmoja akienda kutibiwa nchini India atagharimu Sh milioni  27.

Dk. Shemu amesema katika kipindi cha mwaka huu, taasisi ina mpango wa kufanya upasuaji wa wagonjwa 1,700 wakiwamo wagonjwa 700 wa kupasua kifua na wagonjwa 1,000 kwa kutumia mtambo wa ‘catheterization’ usiohusisha upasuaji wa kufungua kifua.
Amesema taasisi imejipanga kutoa elimu kwa wananchi kwa kuanzia mashuleni kwa sababu ugonjwa huo unawakumba zaidi watu wenye umri mdogo.
Kwa kuwa mgonjwa anayefanyiwa upasuaji wa moyo anahitaji damu nyingi tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu na uchangiaji huu usifanyike kwa mara moja bali uwe endelevu,” amesema Dk. Shemu.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo licha ya kutoa huduma kwa gharama nafuu kwa Watanzania, lakini imekuwa ikipokea wagonjwa wa moyo kutoka nchi jirani kama Rwanda, Burundi, Visiwa vya Comoro, Uganda na nchi nyingine za Kiafrika.
“Wakati umefika kwa nyie watu wa habari na wadau wengine kujitoa  na kuanza kutoa elimu kwa wananchi hasa maeneo ya vijijini kujitokeza kupata huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo yanayotolewa na taasisi hiyo,” amesema Shemu.
Amesema watoto wadogo wenye matatizo ya moyo ambao kwa sasa wameanza kufanya matibabu ya kuziba matundu ya kwenye moyo bila kufanya upasuaji wanapatiwa huduma bure.
Amesema Watanzania hawana budi kujivunia uwepo wa taasisi hiyo imekuwa kimbilio kwa watu wengi wenye matatizo ya moyo na kuweza kuipunguzia mzigo wa kuwapeleka nje ya nchi.
“Pamoja na changamoto za hapa na pale lakini Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto husika imekuwa ikijitahidi kufanya kila liwezekanalo juu ya ustawi wa taasisi kwa manufaa ya Watanzania maskini,” amesema Shemu.

 

NA MICHAEL SARUNGI

By Jamhuri