Taasisi ya Uhusiano wa Umma Tanzania, (PRST) inatarajia kufanya maadhimisho ya wiki ya Mawasiliano Afrika, iliyoanza tokea Mei 21 na kilele chake kinatarajiwa kuwa Mei 25, 2018 na Tanzania watafanyia kwenye Ofisi ndogo ya Bunge iliyopo Posta Jijini Dar es Salaam. 
 
 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Chama hicho hapa Tanzania, Ndege Makura, amesema ili kufanikisha siku hiyo wameamua kuweka mezani maada inayoendana na agenda kuu ya siku hiyo Kitataifa ya Uchumi wa pamoja barani Afrika, wao wamekuja na Tanzania ya Viwanda. 
 
 Amesema takribani ya Mataifa yote yamekua katika kusherekea siku hiyo ya mawasiliano ambapo jumla ya miji 60 Barani Afrika wanasherekea ikiwemo na Tanzania. Aidha amesema kuwa katika kongamano hilo, yapo malengo bainishwa Kimataifa huku Bara la Afrika wakijadili uchumi wa pamoja lakini kwa Tanzania watajadili suala la mchango wa Maafisa Uhusiano wa Umma ni kwa jinsi gani wanaweza kuchangia kuleta maendeleo ya uchumi hususani katika suala zima la kutangaza sera ya Tanzania ya Viwanda. 
 
 “Hii ni siku muhimu kwetu watu wa Uhusiano wa Umma , kwani tutajadili vitu vingi vinavyotokana na Sera za maendeleo ya Taifa, wapo watu wengi hawaelewi nini maana ya Viwanda, dhumuni lake na njia za kufikia ndoto hiyo ya Rais wetu, hata Bungeni tumeona Wabunge wakikinzana kuhusu viwanda, tunaleta mjadala huu ili kujadili kwa kina na wataalamu wetu , Wizara ya Viwanda, Afisa uhusiano wa umma kutoka Serikalini na Taasisi binafsi, waandishi wa habari, ili kusaidia ndoto ya Taifa letu kufikia malengo ya Tanzania ya viwanda ifikapo 2025” amesema Makura. 
 
 Nae Rais wa PRST, Loth Makuza amesema kuwa umefika wakati wa kwenda kumkwamua afisa habari wa taasisi au shirika binafsi ili aweze kujitambua na kutambua malengo ya serikali yake kwa kujua umuhimu wa kazi yake. “Kuna Maofisa Habari wengi hawajitambui hasa kwa kuwa nyuma kabisa kwa vile wengine hawajui hata malengo ya serikali au mashirika yao, matokeo yake wao huishia kuandika taarifa za kuambiwa badala ya kuwa wao wawe miongoni mwa watu wanaoweza kuzitokea ufafanuzi zaidi na kwa kina,” amesema Makuza.
 
 Ameongeza kuwa changamoto nyingi za kutokukamilika kwa Sera mbali mbali za maendeleo hapa nchini kutofikia lengo ni kutokana na kutoshirikishwa hivyo watu wamekuwa wakichelewa kupata taarifa na kujua kwa kina juu ya utungwaji wa Sera hizo. , Amewaomba wadau wajitokeze kwa wingi ili kuchangia mambo ya msingi yanayohusu maendeleo ya Taifa letu pamoja na uchumi wa pamoja katika Bara letu la Afrika. 
 
 Barani Afrika Makao Makuu ya Taasisi ya Uhusiano wa Umma yapo mjini Lagos Nigeria na duniani hapo uingereza Taasisi ya Uhusiano wa Umma Tanzania, (PRST) ilizinduliwa rasmi mwaka jana Novemba 2, mwaka 2017, Jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Benki kuu ya Tanzania, huku ikitimiza zaidi ya wanachama 200, ambapo miongoni mwao wametokea kwenye Taasisi binafsi walizo ajiriwa na wengine kutoka Vyuoni.
Katibu wa Taasisi ya Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST) Ndege Makura, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Mei 22, 2018 jijini Dar es Salaam wakati akielezea maadhimisho ya wiki ya Mawasiliano Afrika inayotarajiwa kufanyika katika Ofisi ndogo ya Bunge iliyopo Posta. Pembeni yake ni Rais wa PRST, Loth Makuza.
Rais wa Taasisi ya Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST), Loth Makuza akitoa msisitizo kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono katika maadhimisho ya wiki ya Mawasiliano Afrika inayotarajiwa kufanyika katika Ofisi ndogo ya Bunge iliyopo Posta. Kushoto ni Katibu wa PRST, Ndege Makura. Picha zote na Cathbert Kajuna – Kajunason/MMG. Na Cathbert Kajuna – Kajunason/MMG. 
2520 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!