Polisi wangeweza kuepusha mauaji ya Mwangosi

Nianze kwa kutoa salamu za rambirambi na pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na watu wote walioguswa na kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, amina.

Kwa ukweli usiopingika, askari polisi walikuwa na uwezo wa kutosha kuepusha mauaji ya mwanahabari huyo, yaliyotokea Septemba 2 mwaka huu, katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.

 

Pamoja na kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndiyo chanzo cha mkusanyiko wa watu katika eneo la tukio hilo kinyume cha amri iliyokuwa imetolewa na Jeshi la Polisi, bado Tafakuri ya Hekima inajiridhisha kuwa uhai wa Mwangosi ulikuwa mikononi mwa askari polisi.

 

Mwangosi aliuawa katika mazingira ya ukatili uliovuka mipaka na uliozusha simanzi na huzuni kubwa kama si hisia, mawazo na mitazamo tofauti katika jamii. Hakika Jeshi la Polisi haliwezi kukwepa lawama za mauaji ya mwanahabari huyo. Hata hivyo, tusisahau kuwa kifo cha mwanahabari huyo ni sehemu ya vifo lukuki vya raia wasio na hatia vinavyokuwa vikitokea katika mazingira na maeneo mbalimbali nchini.

 

Habari za kifo cha Mwangosi zimesambaa sana kwa vile alikuwa mwanataaluma ya uandishi wa habari ambayo ni kisemeo cha jamii. Lakini kumekuwa na matukio mengi ya vifo vya watu wasio na hatia ambayo hayakutangazwa katika vyombo vya habari.

 

Turudi kwenye mada ya leo, ninaposema askari polisi walikuwa na uwezo wa kutosha kuepuka mauaji ya Mwangosi ninajikita katika sababu kuu tatu kama ifuatavyo:

 

Kwanza, Jeshi la Polisi ni chombo cha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichokabidhiwa dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao. Kwa hivyo, askari polisi wana jukumu la kuhakikisha kuwa uhai wa mtu haukatishwi na mtu mwingine yeyote katika himaya yao. Kimsingi nchi yetu ni himaya ya Jeshi la Polisi katika suala zima la ulinzi wa usalama wa raia na mali zao.

 

Askari polisi waliokwenda kudhibiti mkutano wa Chadema katika Kijiji cha Nyololo walipaswa kuhakikisha Mwangosi anaendelea kubaki hai mikononi mwao, hasa ikizingatiwa kwamba hakuwa na silaha yoyote ya kukabiliana nao. Lakini pia, ushahidi wa awali, zikiwamo picha zilizopigwa eneo la tafrani, unaonesha kuwa Mwangosi hata kama alituhumiwa kufanya kosa, tayari alikuwa ameshadhibitiwa, alikuwa ameshazingirwa na kundi la askari polisi wenye silaha.

 

Swali moja linatosha kujiuliza. Kulikuwa na sababu gani ya polisi kushindwa kuepusha mauaji ya mwanahabari huyo ambaye walikuwa ameshamdhibiti kwa nguvu kubwa? Maelezo ya awali ya Jeshi la Polisi yanaeleza kwamba Mwangosi aliuawa na kitu kinachodaiwa kurushwa kutoka katika kundi la raia waliokuwa wakifanya vurugu za kuwarushia mawe askari polisi, ambacho kilimlipua hadi kufumua utumbo wake.

 

Ingawa tume kadhaa zimeshaundwa kuchunguza chanzo na mazingira halisi ya kifo cha Mwandosi, Tafakuri ya Hekima haishawishiki kuamini kwamba askari polisi wanaweza kukwepa lawama za kushindwa kuepusha mauaji ya mwandishi huyo.

 

Pili, askari polisi, kama ilivyo kwa watu wengine, wanafahamu jukumu kuu la waandishi wa habari kwamba ni kuhabarisha jamii. Mbali ya kujitambulisha, Mwangosi alijidhihirisha wazi kuwa ni mwandishi wa habari kutokana na kamera ya kurekodi matukio aliyokuwa amebeba.

 

Kwa mantiki hiyo, askari polisi walipaswa kumpatia ushirikiano wa dhati na hasa kumwimarishia Mwangosi ulinzi wa usalama wa maisha yake katika harakati zake za kufuatilia mwenendo wa tafrani baina yao na kusanyiko la wananchi.

 

Pengine habari ambazo zingetangazwa na Mwangosi katika Televisheni ya Channel Ten zingesaidia kuonesha uhalisia wa vurugu zinazodaiwa kufanywa na wananchi dhidi ya askari polisi. Lakini katika hali ya kushangaza, askari polisi walimtazama mwandishi huyo kama adui kiasi cha kumgeuzia kibao kwa kumshambulia kwa virungu kabla ya kuangamizwa kikatili na kitu kinachodhamiwa kuwa bomu!

 

Kitendo cha askari polisi kumshambulia kwa virungu mwanahabari huyo hata baada ya kutii amri ya kuwa chini ya ulinzi, kinadhihirisha kuwa nia yao ilikuwa ni zaidi ya kuona usalama wa maisha yake unaendelea. Huo ni uvunjifu wa haki za binadamu na utawala bora. Kama Mwangosi alituhumiwa kufanya kosa lolote siku hiyo, kwanini askari hao hawakufuata utaratibu wa kumpeleka katika kituo cha polisi ili kumhoji na kumwandalia mashitaka ya kumfikisha mahakamani, badala ya kutumia nguvu kubwa kiasi hicho?

 

Tatu, askari polisi walipaswa kuongozwa na hekima zaidi katika kudhibiti mkutano wa Chadema, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanaimarisha ulinzi wa usalama wa watu mkutanoni madhali kazi yenyewe ilikuwa ya ufunguzi wa tawi la chama hicho. Kabla ya kuchukua hatua yoyote, polisi walipaswa kupima au kulinganisha vitu viwili; kubaini kilicho bora zaidi kati ya kutawanya mkutano huo kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi na kulinda usalama wa wananchi waliohudhuria ufunguzi wa tawi hilo.

 

Kimsingi hatua ya Jeshi la Polisi kuzuia vyama vya siasa ikiwamo Chadema kufanya mkutano ya hadhara ili kupisha shughuli za sensa ya watu na makazi nchini ni nzuri. Lakini kitendo cha kutumia nguvu kubwa kukabiliana na raia ni cha kikandamizaji. Hivi kulikuwa na ugumu gani kwa askari polisi kulinda usalama wa mkutano huo badala ya kuchukua hatua ya kupiga wananchi virungu na kuwafyatulia mabomu ya machozi kuwatawanya?

 

Kwa upande mwingine, kulikuwa na ugumu gani kwa Chadema kutii amri ya Jeshi la Polisi ya kutohamasisha mkusanyiko wa watu siku hiyo? Chadema nayo haiwezi kujiweka kando katika mazingira yaliyochangia kutokea kwa mauaji ya Mwangosi. Lakini kikubwa zaidi, askari polisi hawawezi kukwepa mzigo wa lawama za mauaji hayo kwa kuwa walikuwa na uwezo wa kuyaepusha.

 

Wakati Jeshi la Polisi likibeba mzigo huo, vyama vya siasa navyo vinapaswa kujenga dhana ya kuheshimu na kutii sheria za nchi bila shuruti, kwa kuzingatia kuwa nchi yetu inaendeshwa kwa utawala wa sheria. Dhana hiyo itasaidia kuepusha migogoro isiyo ya lazima baina ya polisi na raia. Ndugu, jamaa na rafiki yetu Daudi Mwangosi amekatishwa maisha yake duniani, ametangulia mbele ya haki. Nitaendelea kuamini kuwa askari polisi walikuwa na uwezo wa kutosha kuepusha mauaji yake na si vinginevyo.

 

0765 649 735

gamainac@gmail.com

1131 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!