Nimekuwa nikiandika makala za hamasa kuhusu ujasiriamali, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi ambapo kuna upungufu mkubwa wa ajira, lakini pia kuna mfumko wa gharama za maisha kiasi kwamba hata walioajiriwa wanapata wakati mgumu kumudu vema maisha ya kila siku.

Moja ya swali ambalo nimekuwa nikiulizwa mara kwa mara ni hili, “Sanga unataka kila mtu awe mjasiriamali?” Jibu langu katika swali hilo limekuwa ni hili siku zote: “Ndiyo, natamani kila Mtanzania awe mjasiriamali”.


Nafikiri ipo haja tuangalie kinagaubaga dhana hii ya ujasiriamali kwa mtazamo mpana. Ujasiriamali umegawanyika katika makundi mawili. Mosi, ni ujasiriamali wa kibiashara (entrepreneurship) na pili ni ujasiriamali wa kikazi (intrepreneurship).

 

Kundi la kwa linahusisha wajasiriamali waliojiajiri na kundi la pili linahusisha wajasiriamali walioajiriwa. Wajasiriamali walioajiriwa wanaitwa “Wajasiriakazi” na wajasiriamali waliojiajiri walipaswa kuitwa “Wajasiriabiashara”.

 

Wataalamu wa Kiswahili itabidi waliweke sawa hili kwa sababu neno “ujasiriamali” linatumika kiupendeleo kwa kuwalenga wale tu waliojiajiri wakati linatakiwa kuyafaa makundi yote mawili. Nadhani sasa utaelewa ni kwa nini ninasema natamani kila Mtanzania awe mjasiriamali. Leo katika makala haya nitajikita kueleza dhana ya ujasiriamali kazini.

 

Hivyo basi, kila ninapohamasisha watu kuwa wajasiriamali, haimaanishi huwa ninawananga wale walioajiriwa, la hasha! Mtu yeyote aliye mweledi wa uchumi na kiimani, anafahamu umuhimu wa kila mtu kusimama katika nafasi yake kutimiza kusudi la taifa na kusudi la Mungu. Hakuna aliye bora zaidi ya mwenzake; aliyeajiriwa ama aliyejiajiri, mfanyakazi ama mwajiri, wote wana umuhimu sawa.

 

Kwa sababu hakuna ujasiriamali kama hakutakuwa na watendakazi. Kwa hiyo waajiri (wajasiriamali wa kibiashara) wanahitajika kwa wingi na wafanyakazi (wajasiriamali wa kikazi) wanahitajika pia. Kwa maana hii, taifa linahitaji kuwapata wafanyakazi ambao watawiana na ndoto za taifa na wajasiriamali katika kujenga uchumi na kuleta maisha bora.

 

Miaka ya karibuni dhana ya ujasiriakazi imekuwa ikipata umaarufu mkubwa, ingawa ni watu wachache ambao wanaielewa vema dhana hii. Watafiti wengi wanakubaliana kuwa dhana ya ujasiriakazi, ni jamii ya dhana ya ujasiriamali (entrepreneurship) lakini hii ikiwa inafanyika ndani ya taasisi, kampuni, na serikalini ikihusisha “usimamizi wa rasilimali kiubunifu”.

 

Dhana ya ujasiriakazi inaonesha kuwa ilijitokeza na kushika kasi duniani miaka takribani thelathini iliyopita. Ujasiriakazi unahusisha uundaji, uendelezaji na utekelezaji wa mawazo na tabia mpya katika maeneo ya kazi. Ubunifu unaweza kuhusisha kubuni bidhaa mpya ama huduma, kubuni mfumo mpya wa utawala ama mpango mpya ama mikakati inayohusiana na wafanyakazi katika eneo husika.

 

Wajasiriakazi ni watu ambao si lazima wawe wagunduzi wa bidhaa ama huduma mpya, isipokuwa ni watu ambao wanabadilisha mawazo ama fikra kwenda kwenye uhalisia wenye faida. Ni watu ambao ukiona huduma ama bidhaa basi ujue kuwa wapo nyuma yake.

 

Ni watu ambao huunda timu za kiutendaji ili kuhakikisha kuwa wanafanya juhudi kushughulikia mawazo yao kuwa katika uhalisia. Wajasiriakazi si lazima wawe watu wenye uwezo wa juu sana kiakili, lakini ni watu wa upeo wa kawaida kiakili.

 

Kwa mtazamo huu tunaona kuwa dhana ya ujasiriakazi, inajikita zaidi katika kutoa msukumo mpya na kuwezesha maeneo ya kazi kuwa na ubunifu na njia mbadala za kutekeleza majukumu yake. Muunganiko wa wafanyakazi katika maeneo husika yanasababishia kutengenezwa kwa sura mpya ya taasisi, ama kampuni ama kitengo cha serikali.

Wafanyakazi wajasiriakazi ni wale wanaohitaji uhuru na urahisi wa kutumia rasilimali za maeneo yao ya kazi, wenye hamasa kutoka ndani (self-motivated) na wanaoguswa kwa mafanikio chanya ya maeneo yao ya kazi. Mara nyingi hawa huwa wana ujuzi na maarifa mazuri ya kurasimisha madaraka, wanajiamini, wanafanya utafiti wa kimasoko na kihuduma, hawaogopi kufukuzwa makazini na wanajikita katika kuthamini kuwapo kwa wateja ama watu wanaowahudumia.

 

Kiujumla mahitaji ya dhana ya ujasiriakazi yanajikita katika kuibuka kwa mambo yafuatayo. Kuwapo kwa kampuni mengi ya kibiashara yanayoshindana kwa mbinu za kisasa pamoja na watu kupoteza imani na mifumo iliyozoeleka na kikiritimba ya kiutawala na kiuongozi katika taasisi mbalimbali (binafsi na serikalini).

 

Vile vile ujasiriakazi unapata mashiko kutokana na kuibuka kwa watu wenye akili na uwezo mkubwa, ambao wanaanzisha kampuni kwa kutumia mbinu zilizoibwa kutoka kampuni kongwe. Lakini kubwa kuliko yote ni kiu ya watu kuona kuwa kila eneo la biashara ama huduma linakuwa na ufanisi.

 

Mfumo wa dunia wa sasa unalazimisha kutekelezwa kwa vitendo dhana ya ujasiriakazi katika maeneo mbalimbali kutokana na sababu mbalimbali. Kwa upande wa kampuni za kibiashara, inaonekana kuwa ushindani wa kibiashara kwa sasa umekuwa ni mkubwa na uliotete mno, kiasi ambacho kila mfanyakazi anahitajika kuwa mbunifu kwa ajili ya kuzisaidia kampuni husika.

 

Viongozi wa kisiasa nao wanajikuta katika mbinyo wa kutimiliza dhana hii ya ujasiriakazi katika mifumo wanayoiongoza, kutokana na matakwa ya wapiga kura wao. Wananchi katika miaka ya sasa ambayo inaongozwa na mageuzi ya utandawazi, wamekuwa makini mno katika kubaini mahitaji yao halisi. Wapo makini sana na ahadi wanazopewa na viongozi wao, wapo makini na muda, na wapo makini sana na mienendo ya kiutekelezaji wa ahadi mbalimbali zinazotolewa.

 

Miaka ya sasa wananchi wamechoshwa na ukiritimba uliokuwa kama utamaduni katika ofisi mbalimbali za serikali. Mtindo wa mtu kufuatilia faili mwezi mzima, kisa anashinikizwa kutoa rushwa “kiaina” umewachosha sana wananchi. Wengi wa wananchi wamebahatika kupata elimu, wanawasiliana na dunia, wanajifunza huko kwingine mambo yanaendaje, wanahoji, wanataka kujua kwa nini huku kwetu mambo yawe hivi?

 

Ni jambo lililo dhahiri kabisa kuwa kutekelezwa kwa dhana hii ya ujasiriakazi katika maeneo mengi (hasa ya serikali), kunaweza kuleta shida na kuchukua muda mrefu sana kukamilika. Hata hivyo, wadau wa maeneo ya kazi ni vema wakaungana na mtaalamu katika masuala ya ubunifu wa kijasiriakazi – James Brian Quinn – ambaye alibaini vigezo vifuatavyo katika kuwawezesha wafanyakazi kuwa wabunifu katika maeneo ya kazi.

 

Anataja vigezo hivyo kuwa ni mazingira mazuri ya kufanyia kazi na maono, mtazamo katika masoko yanayohudumiwa na mwisho ni muundo wa taasisi husika. Quinn anasema kuwa kampuni na taasisi zilizofanikiwa zimekuwa na maono kamili na yanayotekelezeka kwa huduma na bidhaa wanazozalisha, wanatengeneza na kutoa huduma kwa kuzingatia mahitaji kamili ya mteja.

 

Kigezo kingine ni kuwa na mibadala mingi katika kushughulikia mambo yahusianayo na majukumu yao. Kwa mfano, kitengo cha elimu katika wilaya ama mkoa kinaweza kuwa na mkakati wa kutatua tatizo la upungufu wa walimu na uhaba wa madarasa.

 

Ikiwa afisa elimu wa ngazi husika atakuwa ni mjasiriakazi atahakikisha kuwa anakuwa na njia zaidi ya moja, kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinatatulika kwa ukubwa. Mbali na pengine kusubiri kuletewa tu fungu kutoka serikalini atakuwa na plan B na C ya ama kuitisha harambee ama kutafuta ufadhili. Huyu ndiyo mjasiriakazi kazini.

 

Yapo mambo ya msingi ambayo yanapaswa kufanywa katika maeneo ya kazi, ili kufanikisha kusimika ujasiriakazi. Mambo hayo ni kujiwekea malengo ambayo ni lazima yajadiliwe na kukubalika na wafanyakzi wote pamoja na viongozi wao. Kuwapo mfumo unaoelekeza na kushughulikia mirejesho ili wajasiriakazi wajisikie kutambulika na kuthaminiwa.

 

Jambo jingine ni kwa viongozi wa maeneo ya kazi kuhakikisha wanasisitiza kuwapo kwa majukumu ya mtu mmoja mmoja. Mara nyingi kutoa majukumu kiujumla, huwa kunapunguza uwajibikaji kwa sababu kila mmoja anahisi hahusiki moja kwa moja.

 

Ili kuinua ari na hamasa ya wajasiriakazi kufanya kazi kwa bidii, ni lazima kutoa zawadi na tuzo kulingana na ufanisi wa kazi.

0719 127 901,

stepwiseexpert@gmail.com


1111 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!