Ufisadi wa zaidi ya Sh bilioni 6 katika Chama Cha Akiba na Mikopo (Wazalendo Saccos) mkoani Kilimanjaro, umeendelea kuibua mapya kwa utoaji wa mikopo kwa watu ambao si wanachama wakiwamo marehemu.

Wizi wa fedha zilizokopwa kutoka taasisi mbalimbali za fedha ulihusisha fedha taslimu na kuwalipa watu ambao hawakuwa wanachama wa chama hicho, na kukiuka taratibu za uendeshaji wa vyama vya ushirika.

Licha ya Mrajis wa Vyama Vya Ushirika, Dk. Audax Rutabanzibwa, kubaini upotevu wa kiasi hicho cha fedha katika ripoti yake, bado analalamikiwa na wanachama wa chama hicho kwa kutochukua hatua mapema ama kuzembea na kuwaacha wahusika wakitamba mitaani.

Dk. Rutabanzibwa alipohojiwa na JAMHURI wiki iliyopita kuhusu tuhuma hizo za kuwalinda wahusika wa ufisadi huo, alimtaka mwandishi kuwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod Mutafungwa, kwamba ndiye mwenye taarifa zote kuhusu suala hilo.

Kamanda Mutafungwa licha ya kusema hafahamu kwa undani suala hilo kutokana ugeni wake katika mkoa huo hadi atakapowasiliana na wasaidizi wake, amesema mtuhumiwa Maghimbi Mbonea, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za wizi wa fedha hizo.

Anasema Mbonea alifunguliwa kesi mbili za jinai (CC Na. 354/2012 na CC 324/2014) ambazo zinaendelea kusikilizwa. 

“Kuhusu watuhumiwa ambao umedai wanaendelea kuripoti polisi, ninafanya ufuatiliaji kwa watendaji walio chini yangu ili kujua ukweli na hatima ya watuhumiwa hao kwa mujibu wa taratibu za kiupelelezi na kisheria,” anasema Kamanda Mutafungwa.

Akizungumza na JAMHURI, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, Alex Kuhanda, anasema vyama vya kuweka na kukopa zaidi ya 20 kikiwamo cha Wazalendo Saccos, vinachunguzwa kutokana na tuhuma za ufisadi.

“Tunazichunguza Saccos zaidi ya 20 katika Mkoa wa Kilimanjaro, ikiwamo hiyo ya Wazalendo. Tukikamilisha uchunguzi wetu wahusika watachukuliwa hatua za kisheria,” anasema Kuhanda.

Naye Afisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi, Amerita Bureta, anasema ni kweli kulitokea na upotevu wa fedha hizo na kusababisha kufilisika kwa chama hicho na wanachama kuachana nacho.

Bureta anasema wizi huo ulifichuliwa kuanzia mwaka 2012, na kwamba ulisababishwa na uongozi uliopita. Wizi huo ulikuwa umegawanyika katika maeneo mawili ukihusisha fedha taslimu na utoaji wa mikopo kwa watu ambao si wanachama.

Anasema chanzo cha wizi huo kilitokana na ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa vyama vya ushirika, ikiwamo kutokufanya vikao na mikutano na hivyo kuwapa nafasi wahusika kufanya tukio hilo.  

Marejesho ya mikopo kwenda nje kwa mwezi ni Sh 146,527,175.76 ambazo chama hicho kimeshindwa kulipa huku kikiwa na uwezo kurejesha Sh milioni 45 tu, nazo kimeshindwa kuzilipa na kuwakwepa wadai kwa kuacha kuweka fedha katika akaunti yake iliyoko katika Benki ya CRDB, tawi la Jengo la Kahawa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mrajis wa vyama vya ushirika, miamala  ya fedha isiyozingatia utaratibu ilifanywa na waliokuwa viongozi wa Wazalendo Saccos kwa kumtumia Reuben Mwandambo, huku wakigawana fedha hizo kwa kuorodhesha wanachama hewa ambao walipewa mikopo ya mamilioni nje ya ofisi za chama hicho.

Hisa za wanachama zaidi ya 300 zinazofikia Sh milioni 600 nazo zimepotea na kwamba wakifuatilia wanazungushwa kwa muda mrefu bila mafanikio yoyote.

Wanachama hao wanasema, wanapohoji kuhusu upotevu wa fedha hizo na wahusika kuachwa wakiendelea na kazi kama hakuna kilichojitokeza, uongozi wa chuo umekuwa ukitishia kuwafukuza kazi.

Fedha hizo zilikopwa na Wazalendo Saccos kwa udhamini wa chuo hicho kuanzia mwaka 2008 hadi 2012 kutoka CRDB, KCBL, SELF, PPF na Oiko Credit na kusababisha upotevu uliotajwa.

Mrajis wa Vyama Vya Ushirika nchini katika ripoti yake baada ya kufanya ukaguzi katika chama hicho, anasema chama kilikopa kiasi kikubwa cha fedha kutoka katika taasisi za fedha kilichofikia jumla ya Sh 6,803,610,000 bila kufanya tathmini kutoka taasisi mbalimbali.

Aidha, katika ripoti hiyo ya Mrajis, mwaka 2008 hadi 2011 Wazalendo Saccos ilikopa tena kiasi cha Sh 4,243,700,000/- kutoka katika taasisi hizo za fedha huku mikopo yote kwa asilimia 50 ikitolewa bila kuzingatia taratibu, huku asilimia 11.8 ya mikopo hiyo ikitumika katika urejeshaji wa mikopo kutoka taasisi moja na kwenda nyingine.

“Bodi, Menejimenti na Kamati ya Usimamizi waliokuwapo kati ya 2008 hadi 2012 ilihusika na upotevu wa Sh 3,381,899,103 ikiwa ni mikopo ama malipo yasiyozingatia taratibu, yanayofikia Sh 3,099,102,303 na upotevu wa Sh 254,516,890 na kusababisha kiasi hicho kikubwa cha fedha kuwa nje na kutorejeshwa,” inasomeka ripoti ya Mrajis.

Waliotajwa na ripoti hiyo kuhusika na upotevu wa fedha hizo ni Mbonea Maghimbi, Mwandambo, Emrode Kimambo, Dk. John Haule, Jasinta Tarimo, Ibrahim Shughuru, Gloria Chuwa na Paul Kibiriti ambaye ni askari polisi akihusishwa pia na uchukuaji wa fedha zilizokabidhiwa kwa Maghimbi.

Kutokana na uchunguzi wa Polisi uliochukua kipindi cha miaka mitano sasa, wanachama wa Saccos hiyo wanasema uchunguzi uliofanywa na Mrajis haukuwa na sababu za msingi za kuwataka baadhi ya watuhumiwa wa wizi huo kuendelea kuripoti Kituo cha Polisi kila mwezi.

Wanasema kitendo cha kuchelewesha uchunguzi huo kina nia ya kuchelewesha, ama kuvuruga mashauri yaliyoko mahakamani na hivyo kupoteza haki zao ikiwa ni pamoja na hisa ambazo hadi sasa hawajapewa gawio kwa kisingizio cha upotevu wa fedha hizo.

By Jamhuri