Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeanza kufanya uchunguzi wa kina kwa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuthibitisha habari za kiuchunguzi zilizofanywa na gazeti hili la JAMHURI na kubaini kuwa TBL wanatumia udhaifu wa sheria kukwepa kodi nchini.

Uchunguzi huo ulioanza kuchapishwa Machi 1, mwaka huu, unaonesha kuwa TBL wanakwepa kodi kwa njia ya kujiuzia bidhaa kama Konyagi na bia kwa bei ndogo, hali inayoshusha mapato yao. Wakati wanauza Konyagi kwa kampuni ya Kapari Limited ya Kenya kwa dola 24.78 kwa katoni moja, wakijiuzia kwa kampuni yao ya Crown Beverage hushusha bei hadi dola 15.52.

Kwa maana hiyo, kiasi cha dola 9.27 wanakipata bila kukilipia kodi. Kwa kufanya hivyo, wanapunguza kiwango cha faida wanachoonekana kupata mwisho wa mwaka na hivyo kuishia kulipia kodi ndogo ya Sh bilioni 95. Mchezo huo wa kujiuzia bidhaa zao kwa bei rahisi wanaufanya kwa bia, Konyagi na bidhaa zote wanazozalisha.

Baada ya JAMHURI kuchapisha taarifa hizo, Takukuru wamekwenda TBL na kuanza uchunguzi wa kina. “Tumekwenda pale, tumechukua mikataba waliyoingia. Tunaisoma kujiridhisha kama kuna jinai waliyotenda TBL… wote waliohusika si muda mrefu kama tukibaini wana hatia utawaona mahakamani. Hata kodi waliyokwepa kama ipo, italipwa yote bila kubakiza hata senti tano,” mmoja wa maafisa waandamizi wa Takukuru ameiambia JAMHURI.

Hatua hii, imekuja baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwenda ofisi za Konyagi hivi karibuni wakachukua kompyuta tatu kwa nia ya kuchunguza mauzo na mapato ya TBL. Taarifa zilizoifikia JAMHURI zinasema uchunguzi unaelekea kukamilika na TBL watapaswa kulipa mabilioni kwa hesabu walizokwishafanya.

Wakati gazeti la JAMHURI likifanya uchunguzi huo, uongozi wa TBL ulikataa kutoa ushirikiano kwa gazeti hili, kwa kudai kuwa TBL inalipa kodi zake kwa usahihi hivyo haina tatizo lolote, lakini uchunguzi unaonesha kinyume chake.

JAMHURI inaendelea kufuatilia kwa kina uchunguzi unaofanywa na Takukuru na TRA, ambapo taasisi zote hizi zimebainisha kuwa si muda mrefu zitakamilisha uchunguzi na kuhakikisha haki inatendeka ama kwa TBL au kwa Watanzania kupata kodi inayopotea.

By Jamhuri