“Ushirikina huku Geita ni mkubwa, wachimba madini wengi wanaamini hawawezi kufanikiwa bila kufanya ushirikina, ndio maana kuna vitendo vya mauaji ya alibino na kukata viungo vyao.”

Hiyo ni kauli ya mchimbaji mdogo wa dhahabu katika mgodi wa Nyarugusu alipozungumza na JAMHURI hivi karibuni, kuhusu ukubwa wa imani za ushirikina kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita.

Hata hivyo, mchimba madini huyo aliyeomba kutotajwa jina gazetini, anasema hasara ya vitendo vya ushirikina migodini ni kubwa kuliko faida yake.


“Nimekuwa mchimbaji wa dhahabu kwa zaidi ya miaka 13 sasa, lakini nimebaini kuwa mara nyingi wachimbaji wanaojihusisha na vitendo vya uchawi na ushirikina hapa mgodini (Nyarugusu) hupata hasara badala ya faida waliyotarajia,” anasema.


Anasema yeye binafsi haamini kuwa ushirikiana una faida yoyote zaidi ya kuwasababishia wahusika hasara ya mali na dhambi ya kuabudu mizimu badala ya Mungu.


Mchimba madini mwingine katika eneo la Maumeru mgodini hapo, aliyejitambulisha kwa jina la Samwel Matutu, anasema kuwa mara nyingi matambiko ya ushirikina migodini hufanywa kwa siri, hasa nyakati za usiku.


Nyakati za usiku zinaaminika kuwa ndio muda mzuri wa kufanya matambiko migodini kwa vile wakati huo msongamano na mwingiliano wa wachimbaji huwa umepungua ikilinganishwa na mchana.

Katika tukio lisilo la kawaida, mwarabu mmoja anatajwa kuwa miongoni mwa wachimbaji waliojihusisha na vitendo vya matambiko ya ushirikina kwa matarajio ya kupata dhahabu nyingi mgodini hapo, lakini mwisho wa siku aliishia kupata hasara na kuahirisha uchimbaji.


“Mwarabu huyo alikodi maeneo ya Mtukula na Iririka kwa ajili ya kuchimba dhahabu na kabla ya kuanza uchimbaji alifanya matambiko ya kuchinja karibu kila aina ya mnyama na ndege, lakini hakupata mafanikio, hivyo alikata tamaa na kulazimika kuahirisha uchimbaji,” anasema Matutu bila kutaja jina la mwarabu huyo.


Inaelezwa kuwa mwarabu huyo alikata tamaa na kuahirisha uchimbaji huo baada ya kuona muda alioahidiwa na mganga wa mitishamba umetimia bila kupata alichokikusudia (dhahabu).


Lakini, ni kitu gani hasa kinachowahamasisha wachimba madini kujiingiza katika vitendo vya matambiko ya uchawi na ushirikina migodini?


Mustapha Tingo ni mchimbaji mdogo wa dhahabu katika eneo la Maumeru.

Anasema tamaa ya kupata dhahabu na utajiri wa haraka ndiyo husababisha wachimbaji wengi kujiingiza katika vitendo hivyo, hasa baada ya kuona wengine wanapata dhahabu kwenye mashimo yao.


“Kwa kawaida kila mtu anatamani kutajirika, hivyo basi, hata huku Nyarugusu watu wakiona hawapati dhahabu kwenye mashimo yao huku wengine wanapata, huingia katika majaribu kwa kwenda kutafuta waganga wawasaidie ili nao wapate madini na hatimaye utajiri.


“Lakini cha kushangaza ni kwamba wachimbaji wengi huenda kuwaomba waganga wa kienyeji wawafanyie matambiko ili dhahabu iliyopo kwenye mashimo ya wengine ihamie kwenye mashimo yao, kitu ambacho kwa kweli si rahisi,” anasema Tingo.


Inaelezwa kwamba wachimbaji wengi ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ushirikina migodini wameishia kuyumba kiuchumi na kimaisha kwa jumla baada ya kutumia fedha nyingi kutambika bila mafanikio.


John Minyaru ni mchimbaji mdogo wa dhahabu katika mgodi wa Majengo, Geita.


Ni miongoni mwa wachimbaji wasioamini ushirikina huleta mafanikio machimboni.


“Kwanza nikwambie kuwa binafsi ninachukia sana ushirikina na ninaamini kuwa vitendo hivyo vinaweza kutowesha dhahabu mahali ilipokuwa kwa sababu kufanya hivyo ni kukiuka mapenzi ya Mungu,” anasema Minyaru na kuendelea:


“Mimi siku zote ninamtegemea Mungu katika shughuli zangu za uchimbaji dhahabu na ninapata mafanikio, ninapata fedha za kujikimu na familia yangu ya mke na watoto sita.”


Akisisitiza zaidi, Minyaru anasema anaamini ushirikina hauwezi kuhamisha wala kupeleka madini mahali ambapo hakuna dhahabu.


“Kama kweli ushirikina ungekuwa na uwezo wa kupeleka madini sehemu ambapo hayapo watu wangekuwa wanaomba kupelekewa madini kwenye maeneo yao wanayoyamiliki, hivyo kusingekuwepo na ulazima wa kuyafuata sehemu nyingine kama huku Majengo,” anasisitiza.


Kwa upande wake, mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Penina Masimba anayejishughulisha na uchimbaji mdogo ngodini hapo, anasema kuna haja ya viongozi wa dini kuelekeza mafundisho katika maeneo ya migodini kuwahimiza watu waache imani potofu za ushirikina.


“Wachimbaji wengi wamesahau uwepo wa Mungu, wengi wao wanaamini kuwa hawawezi kufanikiwa kupata madini na utajiri bila kutambika, hiyo ni imani potofu, ni kwenda kinyume cha mapenzi ya Mwenyezi Mungu,” anasema Penina.


Katibu Mkuu wa Chama cha Watafiti na Wachimba Madini mkoani Mwanza (MWAREMA), Golden Hainga, yeye anasema teknolojia ya utafiti na uchimbaji pamoja na vifaa bora vya uchimbaji ndivyo humwezesha mtu kupata madini, na siyo imani ya ushirikina iliyojengeka miongoni mwa wachimba madini.


“Ili uweze kupata madini mengi ni lazima uwe na teknolojia ya utafiti na uchimbaji, lakini pia uwe na zana bora za uchimbaji ikiwa ni pamoja na mashine, komplesa, na vifaa maalumu vya kuchimba, kuponda, kusaga na kuosha mawe yenye madini.


“Hiyo ndiyo njia pekee ambayo humwezesha mchimbaji kuvuna madini mengi na kupata utajiri.

Masuala ya kuua albino na kunyofoa viungo vyao, kuchinja kuku na kwenda kwa waganga ili kupata madini halipo, ni imani potofu tu,” anasisitiza Hainga.


Uchunguzi zaidi umebaini kuwa baadhi ya wachimba madini mkoani Geita wameanza kubaini kuwa imani za uchawi na ushirikina hazina tija yoyote katika shughuli hizo zaidi ya kuwasababishia wahusika hasara zisizo za lazima.


Hata hivyo, kuna haja ya viongozi wa madhehebu ya dini kuelekeza mahubiri katika maeneo ya machimboni kuwabadilisha wachimba madini waliojenga dhana potofu ya kutegemea ushirikina badala ya Mungu wakisaka mafanikio katika shughuli hizo.


Serikali nayo inapaswa kuelekeza nguvu ya kuwaelimisha wachimba madini mbinu na njia thabiti za kuwawezesha kufanikiwa katika shughuli hizo, lakini pia kuwakopesha mitaji na vifaa bora vya uchimbaji madini.


Utafiti huu umefanyika kwa msaada wa Mfuko wa Kusaidia Vyombo vya Habari Tanzania (Tanzania Media Fund – TMF).


2198 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!