Kocha wa timu ya soka ya taifa ya Uganda, Sebastien Desabre, amesema timu ya taifa ya soka ya Zimbabwe ina nafasi finyu katika kundi ‘A’ kwenye michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) baadaye mwezi Juni, mwaka huu.

Uganda itakabiliana na mwenyeji wa michuano hiyo, Misri, DR Congo na Zimbabwe katika kundi ‘A’.

Kocha huyo kwa upande mwingine amekiri kuwa Misri na DR Congo ni kati ya timu zitakazomtia changamoto, lakini akiidharau Zimbabwe akisema ni timu isiyo na bahati kwenye kundi hilo.

“Zimbabwe inaonekana ndiyo timu isiyo na bahati kwenye kundi letu, lakini ninafahamu ubora wa kikosi chao. Kundi hili ni gumu licha ya kwamba Misri inapewa nafasi kubwa kuongoza, timu yetu itapambana vilivyo kupata nafasi ya pili,” amesema Desabre katika  mahojiano yake na mwanahabari Michael Madyira wa mtandao wa michezo wa Goal.

“Kupambana na Misri ni kazi ngumu licha ya kwamba tunayo fursa ya kuifahamu timu hiyo kimchezo.

“Tuliwahi kuwashinda kwa bao moja katika uwanja wetu wa nyumbani na kisha tukapoteza mechi ya marudio kwao kwa tofauti ya goli moja. Kila mmoja anajua kwamba tunao wachezaji wapya mahiri wanaochipukia kwa nguvu na hakuna mtu makini anayeweza kuthubutu kuwabeza, itakuwa vigumu kupata ushindi dhidi ya timu yetu,” amesema.

Kocha huyo amesema wanaijua vema timu ya taifa ya Congo na kwamba wachezaji wa timu hiyo wamekuwa na vipaji vinavyojitosheleza kwa kila mmoja wao, na kwamba watakuwa wanakabiliana na wapinzani wenye ubora mkubwa, kwa hiyo ni lazima wajiandae kikamilifu.

Uganda na Misiri walikuwa katika kundi moja kwenye michuano ya fainali za Afcon mwaka 2017, mafarao hao wakiitandika Cranes 1-0.

Baadaye mwaka huo huo, Uganda iliitandika Misri 1-0 kuelekea michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018, katika mchezo huo Uganda ilishinda dhidi ya Misri kwenye uwanja wao wa nyumbani, kisha kupoteza wakiwa ugenini 1-0.

By Jamhuri